Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ya ASEAN ‘yaliwekwa vyema’ kuendeleza haki za binadamu, uhuru na uchumi imara wa kimataifa

 Katibu Mkuu António Guterres ahudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN)-UN huko Phnom Penh, Cambodia.
© Nick Sells
Katibu Mkuu António Guterres ahudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN)-UN huko Phnom Penh, Cambodia.

Mataifa ya ASEAN ‘yaliwekwa vyema’ kuendeleza haki za binadamu, uhuru na uchumi imara wa kimataifa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakati “migawanyiko inayozidi” inatishia amani na usalama duniani, "mazungumzo ya hatari" yanazidisha mvutano wa matumizi ya nyuklia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameauambia mkutano wa viongozi wa Asia huko Cambodia siku ya Ijumaa.

Akizungumza katika Mkutano wa 12 wa ASEAN-UN, Katibu Mkuu António Guterres alichora picha ya watu wengi katika eneo la Kusini mwa Dunia, "lililoathiriwa" na COVID na mabadiliko ya tabianchi na kuzuia uhaba wa chakula, nishati, na fedha na pia ukosefu wa usalama duniani unaosababisha migogoro mipya huku hali ikizidi kuwa ngumu kumaliza zile changamoto za zamani.

Pia aliangazia uchumi wa dunia uliogawanywa katika sehemu mbili, zikiongozwa na Marekani na China - na seti mbili tofauti za sheria, sarafu, intaneti, na mikakati inayokinzana juu ya akili bandia. "Utengano huu lazima uepukwe kwa gharama yoyote", alisema, akibainisha kuwa nchi wanachama wa kila kikanda "zipo mahala pazuri kusaidia kupunguza utofauti huo".

Guterres alisisitiza haja ya kutafuta ufumbuzi wa kimataifa, kwenye dhoruba za kijiografia na kisiasa, na kurejesha kwenye mstari Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akisema kwamba "mashirika ya kikanda, ikiwa ni pamoja na ASEAN, yana jukumu muhimu la kutekeleza".

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN)-UN huko Phnom Penh, Cambodia.
© Nick Sells
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN)-UN huko Phnom Penh, Cambodia.

Myanmar

Hali ya kisiasa, usalama, haki za binadamu na kibinadamu nchini Myanmar "inazidi kuingia katika janga", mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliendelea kulaani ghasia zinazoongezeka, matumizi mabaya ya nguvu na "hali ya kutisha ya haki za binadamu" nchini humo.

Akikumbusha kwamba chini ya sheria za kimataifa, mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita, alirudia wito wake kwamba mamlaka ya Myanmar "iwaachilie wafungwa wote wa kisiasa na kuanzisha mchakato unaojumuisha mara moja kurejea kwenye kipindi cha mpito cha kidemokrasia" kama "njia pekee ya amani ya kudumu na ya usalama”.

Akikaribisha Makubaliano ya ASEAN yenye vipengele vitano, alihimiza nchi zote "kutafuta mkakati wa umoja" unaozingatia mahitaji na matarajio ya watu wa Myanmar na kutetea mipaka ya wazi, ulinzi, na usaidizi kwa wakimbizi.

"Hakuna mkimbizi anayepaswa kulazimishwa kurudi kwenye mateso na hatari", alisema, akisisitiza haja ya "hatua za haraka za mamlaka ya Myanmar" kuweka mazingira ya kurejea kwa hiari wakimbizi wa Rohingya karibu milioni moja.

"Hali ya kibinadamu nchini Myanmar bado ni ya kukatisha tamaa", aliendelea, akithibitisha uratibu wa karibu wa Umoja wa Mataifa na Kituo cha Kuratibu Misaada ya Kibinadamu cha ASEAN kinachohusika na Usimamizi wa Maafa kwa kushirikiana na washirika wengine wa kibinadamu.

Wanaharakati wa vijana wa Asia waandamana kuwataka viongozi kushughulikia hasara yao na jukumu la uharibifu.
UN News/Laura Quinones
Wanaharakati wa vijana wa Asia waandamana kuwataka viongozi kushughulikia hasara yao na jukumu la uharibifu.

Mabadiliko ya tabianchi

Akiwa ndio kwanza amewasili kutoka katika mkutano wa mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa COP27 nchini Misri, amewataka viongozi ambao nchi zao zinatoa hewa chafuzi lazima "ziangalie udharura wa wakati huu".

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikumbusha kuwa nchi zilizoendelea kiuchumi lazima zipunguze utoaji wa hewa chafu kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 ili kufikia kutoegemea upande wowote wa kaboni katikati mwa karne; kuhamasisha ahadi yao ya kila mwaka ya dola bilioni 100 kusaidia nchi zinazoendelea katika kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga ustahimilivu na kukabiliana na hali hiyo na kufikia makubaliano juu ya kulipa fidia kwa nchi "ambazo hazikufanya chochote kuleta mgogoro huu".

Pia alihamasisha Mkataba wa kihistoria wa Mshikamano wa tabianchi kati ya nchi zilizoendelea na zinazoibukia kiuchumi unaochanganya uwezo na rasilimali zao kwa manufaa ya wanadamu.

"Nchi tajiri zaidi, benki za maendeleo na makampuni ya kiteknolojia lazima yatoe usaidizi wa kifedha na kiufundi kwa kiwango kikubwa ili mataifa yanayoibukia kiuchumi yaweze kuhamia kwenye matumizi ya nishati mbadala", alisema.

Wakati akizipongeza nchi za ASEAN ambazo tayari zimejitokeza kukabiliana na changamoto ya mpito wa haki kwa bidhaa zinazoweza kurejeshwa, afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa alizitaka zile ambazo hazijaweza, kuinua matarajio yao ya tabianchi, kwa kuanzia na kuondoa uwekezaji mpya wa makaa ya mawe na kuacha nishati ya makaa ya mawe ifikapo 2030 kwa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) nchi, na 2040 kwa wengine wote.

Msamaha wa madeni

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa tatizo la upatikanaji wa chakula, nishati na fedha litakuwa kipaumbele chake katika mkutano wa kilele wan chi 20 tajiri zaidi duniani G20 utakaofanyika wiki ijayo mjini Bali, nchini Indonesia.

"Ninawasukuma viongozi wa G20 kupitisha kichocheo cha SDG ambacho kitazipatia serikali za ukanda wa kusini uwekezaji na ukwasi wanaohitaji, na kuharakisha msamaha wa madeni na urekebishaji wa madeni", alifahamisha mkutano huo.

"Pia tunafanya kazi na wadau wote kupanua Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, na kuongeza usambazaji wa mbolea, ambayo inagharimu hadi mara tatu zaidi kuliko kabla ya janga hilo".

ASEAN 'jukumu muhimu' Mwishoni, Katibu Mkuu alitoa shukrani kwa "ushirikiano madhubuti wa ASEAN na dhamira thabiti ya ushirikiano wa pande nyingi na ushirikiano wa kikanda".

Pia aliangazia "jukumu muhimu" la nchi katika kuendeleza haki za binadamu, uhuru wa kimsingi na ushirikishwaji wa kisiasa na vile vile katika maendeleo ya uchumi imara wa kimataifa. "Umoja wa Mataifa utasalia kuwa mshirika wenu thabiti katika changamoto zinazokuja," mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alihakikishia.