Zaidi ya watoto milioni 27 hatarini kuathirika na mafuriko duniani:UNICEF 

Mto Chari na Logone ikiwa imefurika na kusababisha mafuriko makubwa N'Djamena Chad
© UNICEF/Aldjim Banyo
Mto Chari na Logone ikiwa imefurika na kusababisha mafuriko makubwa N'Djamena Chad

Zaidi ya watoto milioni 27 hatarini kuathirika na mafuriko duniani:UNICEF 

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limetoa taarifa inayoeleza mwaka huu pekee takriban watoto milioni 27.7 duniani kote wameathirika na mafuriko makubwa.  

Idadi kubwa ya watoto hao walioathiriwa na mafuriko limesema shirika hilo ni miongoni mwa walio hatarini zaidi na wako katika hatari kubwa ya vitisho vingi ikiwemo kuzama majini na kufa, kupata magonjwa ya milipuko, kukosa maji safi na salama, utapiamlo, kushindwa kuhudhuria masomo na vurugu. 

Kwa mujibu wa Paloma Escudero mkuu wa ujumbe wa UNICEF kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP27 “Tunashuhudia kiwango kisicho cha kawaida cha mafuriko duniani kote mwaka huu ambacho ni tishio kubwa kwa maisha ya watoto. Mgogoro wa mabadiliko ya tabinchi tunao sasa. Katika maeneo mengi mafuriko ni mbaya sana kuwahi kushuhudiwa kwa vizazi kadhaa. Watoto wetu tayari wameathirika sana katika kiwango ambayo wazazi wao hawajawahi kukipitia.” 

Watoto wakiwa wanaelekea nyumbani wakipita kwenye maji machafu ya mafuriko katika eneo la Jacobabad, jimbo la Sindh , Pakistan.
© UNICEF/Saiyna Bashir
Watoto wakiwa wanaelekea nyumbani wakipita kwenye maji machafu ya mafuriko katika eneo la Jacobabad, jimbo la Sindh , Pakistan.

Matokeo ya mafuriko ndio hatari zaidi 

Taarifa hiyo ya UNICEF imesema matokeo ya mafuriko mara nyingi huwa hatari zaidi kwa watoto kuliko hali mbaya ya hali ya hewa iliyosababisha mafuriko hayo. Mwaka huu 2022, mafuriko yamechangia kuongezeka kwa vyanzo vikuu vya vifi vya watoto, kama vile utapiamlo, malaria, kipindupindu na kuhara . 

UNICEF inasema nchi zilizathirika zaidi ni Chad, Gambia, Pakistan, na Kaskazini Mashariki mwa Bangladesh na kiwango wanachikishuhudia cha mafuriko ni cha juu sana kwa zaidi ya miaka 30.  

• Mathalani nchini Pakistani, zaidi ya mtoto 1 kati ya 9 wa chini ya umri wa miaka mitano waliolazwa katika vituo vya afya katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko ya Sindh na Balochistan walionekana kuwa na utapiamlo mkali sana. 

• Nchini Chad, ekari 465,030 za mashamba ziliharibiwa, na hivyo kuzidisha hali mbaya ya uhaba wa chakula. 

• Nchini Malawi, mvua kubwa na mafuriko yaliyosababishwa na dhoruba ya kitropiki Ana mwezi Januari 2022 ilisababisha uharibifu mkubwa wa mifumo ya maji na mifereji ya maji taka, ambayo iliweka mazingira bora ya mlipuko wa kipindupindu. Mlipuko huo umegharimu maisha ya watu 203, kati yao 28 ni watoto. Hadi sasa, watoto 1,631 wameambukizwa kipindupindu. 

• Pamoja na majanga mengine ya mabadiliko ya tabianchi na migogoro, mafuriko yamesababisha makadirio ya idadi ya watoto nchini Sudan Kusini wanaokabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula kuzidi viwango vilivyoonekana wakati wa vita mwaka 2013 na 2016.  

Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulionya kwamba baadhi ya jamii zinakabiliwa na uhaba wa chakula na uwezekano wa kukabiliwa na njaa ikiwa msaada wa kibinadamu hautaendelezwa na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hazitaongezwa. 

watoto wakipita katika maji ya mafuriko huko Pakistan
© UNICEF/Saiyna Bashir
watoto wakipita katika maji ya mafuriko huko Pakistan

Huduma muhimu zimeathirika 

Shirika hilo la kuhudumia Watoto limesema mbali na kutishia maisha ya mamilioni ya watoto, maji ya mafuriko yametatiza huduma muhimu na kuhamisha familia nyingi. 

• Mafuriko ya hivi majuzi nchini Pakistan yaliharibu au kusambaratisha karibu majengo 27,000 ya shule, na kuwalazimu watoto milioni 2 kukosa masomo. 

• Nchini Sudan Kusini, vituo 95 vya lishe vinavyoungwa mkono na UNICEF vimeathiriwa na mafuriko, na kukwamisha utoaji wa huduma za kuokoa maisha na kuzuia utapiamlo kwa watoto 92,000. 

• Takriban watoto 840,000 walihamishwa na mafuriko nchini Nigeria katika miezi ya hivi karibuni. 

• Mvua kubwa na mafuriko nchini Yemen yalisababisha mafuriko na kuleta uharibifu mkubwa kwa makazi katika maeneo ya watu waliohama makwao. Hadi kaya 73,854 ziliathiriwa, na kaya 24,000 zililazimika kuhamishwa. 

Paloma Escudero amesema "COP27 inatoa fursa ya kuchora ramani ya barabara inayoaminika na hatua za wazi za ufadhili wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na hali ya hewa na ufumbuzi wa hasara na uharibifu. Vijana kutoka sehemu zilizoathiriwa zaidi duniani wanazama katika kutochukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Imetosha. Maisha yako hatarini na watoto wanahitaji hatua sasa." 

Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko
© UNICEF/Aldjim Banyo
Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko

Wito wa UNICEF kwa viongozi wa nchi 

Pamoja na kushinikiza serikali na wafanyabiashara wakubwa kupunguza kwa haraka hewa chafuzi, UNICEF inawataka viongozi kuchukua hatua za haraka ili kuwalinda watoto dhidi ya uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi kwa kurekebisha huduma muhimu za kijamii wanazozitegemea.  

Hatua za kukabiliana na hali hiyo, kama vile kuunda mifumo ya maji, afya na elimu ambayo ina mnepo dhidi ya mafuriko na ukame, itaokoa maisha. 

Mwaka jana, nchi zilizoendelea zilikubali kuunga mkono maradufu ili kukabiliana na hali hiyo kufikia dola bilioni 40 kwa mwaka ifikapo 2025.  

“Katika mkutano wa COP27 nchi, lazima ziwasilishe ramani ya barabara inayoaminika yenye hatua za wazi za jinsi fedha zitakavyotolewa, kama hatua ya kutoa angalau dola bilioni $300 kwa mwaka kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ifikapo 2030. Angalau nusu ya fedha zote za kupambana na mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kupatikana kukabili changamoto hiyo” 

  UNICEF pia inazitaka pande husika kutafuta suluhu za kuwasaidia wale ambao watakabiliwa na upotevu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu unaovuka mipaka ambao jumuiya zinaweza kukabiliana nazo. UNICEF inatoa wito kwa serikali kuziba pengo la fedha kwa ajili ya kushughulikia mabadiliko haya yasiyoweza kuepukika kwa watoto.  

Mvulana akiwa amesimama kwenye mifuko ya mchanga iliyowekwa kukinga maji ya mafuriko N'Djamena, Chad.
© UNICEF/Olivier Asselin
Mvulana akiwa amesimama kwenye mifuko ya mchanga iliyowekwa kukinga maji ya mafuriko N'Djamena, Chad.

Wito wa UNICEF kwa washiriki wote 

1. ZUIA. Angalia upya mipango yao ya kukabili mabadiliko ya tabianchi ya kitaifa ili kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa kasi na kwa haraka ili kuzuia janga la mabadiliko ya tabianchi. 

2. LINDA. Hakikisha hatua za wazi za kukabiliana na hali hiyo zinazomlinda kila mtoto dhidi ya athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi kupitia Global Stocktake na Lengo la Kimataifa la Kukabiliana na marekebisho. 

3. JIANDAE. Kuendeleza elimu ya mabadiliko ya tabianchi na ushiriki wa maana ili kuwatayarisha watoto na vijana kupitia mpango kazi wa uwezeshaji wa masuala ya hali ya hewa (ACE) 

4. WEKA KIPAUMBELE, watoto na vijana kwa kuharakisha uwekezaji wa fedha za hmabadiliko ya tabianchi katika huduma za kijamii zinazostahimili hali ya hewa zinazowafikia watoto walio katika hatari zaidi, na kufungua mbinu za kukabiliana na hasara na uharibifu. 

5. Kujitolea kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa watoto kwa kuzingatia na kutekeleza azimio la watoto, vijana na hatua za hali ya hewa. 

Hatua za haraka za kibinadamu za UNICEF kwa nchi zilizoathiriwa na mafuriko zinajikita katika sekta zote afya, lishe, maji, usafi wa mazingira na usafi (WASH), ulinzi wa watoto, na elimu.  

UNICEF inasema ukosefu wa ufadhili, hata hivyo, umezuia hatua katika nchi nyingi, kwa mfano, pengo la ufadhili kwa hatua za kibinadamu nchini Pakistan kwa sasa ni asilimia 85.