Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania kushirikiana na SADC kuzalisha nishati jadidifu

Mitambo ya sola katika ofisi za UNDP jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kama sehemu ya kuongoza kwa vitendo katika hatua za kulinda mazingira.
Sawiche Wamunza/UNDP Tanzania
Mitambo ya sola katika ofisi za UNDP jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kama sehemu ya kuongoza kwa vitendo katika hatua za kulinda mazingira.

Tanzania kushirikiana na SADC kuzalisha nishati jadidifu

Tabianchi na mazingira

Wakati wiki ya kwanza ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP27 unaondelea huko Sharm el-Sheikh nchini Misri ikiwa inaelekea ukingoni na masuala mbalimbali yakiwa yamejadiliwa ikiwemo ufadhili wa miradi ya tabianchi, malipo ya fidia kwa nchi maskini kutokana na hasara na uharibifu uliosababishwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeitisha mkutano na nchi wanachama Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC ili kuhimiza ushirikiano katika kuzalisha nishati jadidifu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais nchini Tanzania anayehusika na Muungano na Mazingira, Seleman Jafo akizungumza na Joyce Shebe mwandishi wa Habari wa Clouds FM ya nchini Tanzania ambao ni washirika wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema mkutano huo ulikuwa na umuhimu kwani wanalenga kuhamasisha uwekezaji wa pamoja kwenye uzalishaji wa nishati jadidifu.

“Miongoni mwa mambo tunayofanya kama serikali ya Tanzania ni uzalishaji wa nishati iliyo rafiki wa mazingira. Na Huu mkutano mkubwa tuliouandaa hapa chini ya Wizara ya Nishati, Rais (Samia Suluhu Hassan aliwaita viongozi wenzake wa SADC ili kujadili kwa pamoja upatikanaji wa nishati isiyoharibu mazingira kwa pamoja ili mosi kuendeleza uchumi wetu na pili kuhakikisha lengo la kupunguza gesi chafuzi kwa kati ya 30% hadi 55% ifikapo mwaka 2030 liweze kutimia. 

Tweet URL

Mabadiliko ya tabianchi yakiathiri nchi moja tunaathirika wote

Waziri Jafo amesema tayari baada ya mkutano huo wameanza kuona matokeo chanya n anchi kama Norway zimejitokeza kusaidia katika maeneo ya nishati, kilimo rafiki wa utafiti kwenye maeneo ya mazigira na maendeleo.

“Kuna mafanikio makubwa sana na mafanikio haya yakienda sambamba na kuwaeleza wananchi wote duniani kwamba Tanzania tumejipanga tuna será mkakati, kanuni na miongozo ya hewa ya ukaa ambayo makampuni mengi hususan kutoka Marekani na jumuiya ya Kiarabu wameanza kuonesha nia ya kuja kuchangamkia fursa hii.”

Waziri huyo wa Mazingir amesema kwakutambua umuhimu wa nishati ndio maana nchi yake ya Tanzania imeamua kuwa kinara wa kusaka umeme rafiki wa mazingira na kutoa wito kwa viongozi wenzake wa Afrika wanaohusika na mazingira.

“Jambo la sisi (SADC) kufanya kazi pamoja ni kubwa na zuri, sababu tukizungumzia mabadiliko ya Tabianchi hata nchi moja ikiathirika maana yake ni kwamba zimeathirika nchi zote kwasababu mabadiliko ya tabianchi hayajali mipaka kwahiyo suala zima la ajenda ya pamoja kuunganisha umeme ambao utasaidia katika nchi mbalimbali ni jambo jema sababu tutakuwa na nishati ya uhakika na yenye kujali mazingira.”

Tanzania imeeleza ina imani kuwa nchi zote zitaungana na mpango huo waliojadili na wanaamini watafanikiwa kwa pamoja kupata nishati iliyo nafuu na inayojali mazingira.

“Wamasai tufanye tamaduni za asili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Jamii za wafugaji pia zimewakilishwa katika mkutano huo wa COP27 ambapo mfugaji kutoka wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro Magharibi mwa Tanzania kutoka jamii ya wamasai amesema mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maisha yao na shughuli zao za kujipatia kipato.

Ole Mwarabu ni mmoja wa waliohudhuria mkutano huo na amesema kwa miaka mingi sasa wanakabiliwa na ukame unaosababisha mifugo kufa jambo linalowafanya wafugali, wakulima na wawindaji wa asili kuwa na shida.

“Ndio maana tumeona tujumuike kwenye mkutano huu tupaze sauti zetu na tunashukuru nchi mbalimbali zimetusikiliza kuwa athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zina matokeo hasi kwenye maisha yetu hivyo yafanyiwe kazi kwenye ngazi ya kitaifa, kimataifa na kikanda.”

Ole Mwarabu ameongeza kuwa kunahaja ya jamii kule wanapotoka kukaa chini na kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu yanasababisha athari katika afya za binadamu, wanyama, mimea na hata udongo na pia shida ya maji na mvua umekuwa kubwa.

“Tunatakiwa kufanya tamaduni za asili kuweza kudumisha maisha yetu yaweze kuendelea. Tunatakiwa kutunza misitu, vyanzo vya maji na katika vyakula vya asili tuone namna gani tunaweza kuweka akiba ya chakula kwa njia za asili ili tupambane na mabadiliko yanayotokea.”

Kuwe na Usawa kijinsia

Akiwakilisha vijana kutoka Tanzania Kijana Clara Kizito Benjamini alisema ujumbe wake kama kijana ni suala la usawa kijinsia katika masuala yote yanayofanyika kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

“Ujumbe wetu sisi kwa COP27 na pia dunia kwa ujumla ni kwamba ili kutatua tatizo la mabadiliko ya tabianchi tunatakiwa kuwaingiza wasichana na wanawake katika mijadala ya utatuzi wa changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi kwakuwa wanawake na wasichana ndio waathirika wakubwa.

Kuhusu COP27

Mkutano huo wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, COP27 umeanza tarehe 6 Novemba na utakamilisha shughuli zake tarehe 18 Novemba 2022.

Wakuu wa nchi, serikali, mawaziri, wasuluhishi pamoja na wanaharakati wa tabianchi, mameya, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, watendaji wa kuu wa kampuni wanakutana katika mji wa pwani ya Misri, Sharm el-Sheikh katika mkutano huo ambao ndio mkubwa kuhusu tabianchi.

Mkutano huu unasongesha yale yaliyokubaliwa kwenye CO26 na kutoa hatua zinazoendana na kutatua dharura ya tabianchi – kuanzia kupunguza hewa chafuzi, kutekeleza ahadi za kufadhili hatua kwa tabianchi katika nchi zinazoendelea.