Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama shughulikieni mambo haya 5 kusaidia kukabili ugaidi Afrika- Guterres

Wakimbizi kutoka Nigeria wakikimbia ghasia huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria
© UNHCR/Hélène Caux
Wakimbizi kutoka Nigeria wakikimbia ghasia huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria

Baraza la Usalama shughulikieni mambo haya 5 kusaidia kukabili ugaidi Afrika- Guterres

Amani na Usalama

Hii leo jijini New York, Marekani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa ngazi ya juu kuhusu kukabili ugaidi barani Afrika kama hatua muhimu kwa ajili ya amani, usalama na maendeleo ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja mambo makuu matano ambayo ametaka Baraza hilo liyazingatie ili kusongesha harakati dhidi ya ugaidi barani Afrika.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed, Bwana Guterres amesema mambo  hayo manne ni muhimu kwa kuzingatia kuwa katika dunia ya sasa iliyounganika, kusambaa kwa ugaidi Afrika si hoja ya hofu kwa nchi za Afrika pekee, bali ni “ni changamoto kwetu sote na hivyo kukabili ugaidi wa kimataifa kunahitaji majawabu au hatua za kimataifa.”

Ugaidi umekuwa na madhara makubwa Afrika

Kikao hicho kiliongozwa na Rais Nana Akuffo Ado wa Ghana ambaye nchi yake ndio inashika urais wa baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba.

Kwa mujibu wa Guterres ugaidi unasalia kitisho kikubwa cha amani na usalama duniani na hakuna ambako kitisho hicho kimejikita na kuleta madhar kama barani Afrika.

“Magaidi na wenye misimamo mikali kama vile Da’esh na Al-Qaida na wafuasi wao wanatumia ukosefu wa utulivu na mizozo kuimarisha shughuli zao na mashambulizi kote barani Afrika,” amesema Katibu Mkuu.

Ametaja mambo hayo kuwa ni mosi, hatua za kinga kama ndio jawabu bora zaidi dhidi ya ugaidi, misimamo mikali na aina nyingine za vitisho vya amani na usalama.

“Lazima tushughulikie ukosefu wa utulivu na mizozo ambayo inaweza kugeuka na kuwa ugaidi pamoja na mazingira ambayo yanatumiwa na magaidi kuendeleza ajenda zao,” amesema Katibu Mkuu akikumbusha kuwa mara kwa mara hatua pekee za kijeshi na kisheria katika kukabili ugaidi hazijazaa matunda hivyo “ni lazima tuweke mizania bora na kuhakikisha kuna hatua za king ana vile vile za kisheria au kijeshi.”

Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza kwenye kituo cha kuhifadhi wakimbizi wa ndani huko Maiduguri nchini Nigeria
© UNHCR/Roland Schönbauer
Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza kwenye kituo cha kuhifadhi wakimbizi wa ndani huko Maiduguri nchini Nigeria

Jamii isienguliwe kwenye mikakati dhidi ya ugaidi

Jambo la pili ni kwamba kila mtu ashirikishwe akisema kutatua vichocheo vya ugaidi kunahitaji mtazamo wa jamii nzima na mtazamo unaozingatia jinsia.

“Hatua dhidi ya ugaidi zinakuwa na fursa zaidi ya kutatua mahitaji na shaka na shuku za jamii pale tu zinapobeba ajenda za kijamii na kuakisi sauti mbalimbali ikiwemo mashirika ya kiraia, makundi madogo, vijana na sekta binafsi,” amesema Guterres.

Suala la tatu ni kuhakikisha hatua zozote dhidi ya ugaidi zinaheshimu haki za binadamu akisema, “ukatili au manyanyaso yafanyikayo kwa kivuli cha kukabili ugaidi vinaturudisha nyuma. Sera fanikiwa dhidi ya ugaidi kama ilivyo kwa sera zozote zile, lazima zizingatie utawala wa sheria na kuheshimu sheria za kimataifa ikiwemo sheria ya haki za binadamu.”

Mipango dhidi ya ugaidi izingatie mazingira ya eneo husika

Mashirika ya kikanda yana nafasi kubwa katika kufanikisha vita dhidi ya kigaidi na ndio jambo la nne akisema changamoto zitokanazo na vikundi vya kigaidi na misimamo mikali zinaweza kutatuliwa pale tu majawabu yatakapozingatia mazingira ya eneo husika.

Kuna mipango mingi ya kikanda ya kukabili ugaidi Afrika kuanzia mpango wa kimataifa wa Ziwa Chad, hadi jeshi la pamoja la nchi 5 huko Sahel na mpango wa Accra na mchakato wa 

Nouakchott,” amesema KAtibu Mkuu akiongeza kuwa michakato yote hii inahitaji kuungwa mkono kwa kina kutoka jumuiya ya kimataifa.

Ni kwa mantiki hiyo amekaribisha kikundi kazi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa, UN na Muungano wa Afrika, AU kuhusu kuzuia misimamo mikali na kukabili ugaidi barani Afrika ambacho kinalenga kuongeza uratibu kati ya vyombo hivyo viwili kwenye kukabili ugaidi.

Amesema kama ilivyoombwa na Baraza la Usalama, “tunaandaa ripoti ya pamoja ya maendeleo ya ufadhili wa operesheni za amani za AU, ripoti ambayo inatakiwa kuwasilishwa mwezi Aprili mwaka 2023.”

Promesse Musole huyu alikuwa mpiganaji msituni, lakini mradi wa ujumbe wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO, wa kupunguza ghasia kwenye jamii umempatia stadi za kutengeneza simu janja na sasa anajipatia kipato halali Goma, jimboni Kivu Kaska…
UN Video
Promesse Musole huyu alikuwa mpiganaji msituni, lakini mradi wa ujumbe wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO, wa kupunguza ghasia kwenye jamii umempatia stadi za kutengeneza simu janja na sasa anajipatia kipato halali Goma, jimboni Kivu Kaskazini.

Uwekezaji wa kijasiri unahitajika kung’oa mizizi ya ugaidi Afrika

Ametamatisha jambo la tano akisema kuzuia na kukabili ugaidi kunahitaji rasilimali hivyo kunahitajika uwekezaji mkubwa na wa kijasiri ili kusaidia maeneo ambayo yako nyuma kiuchumi na yenye changamoto za kiuongozi.

“Nakaribisha mkutano ujao wa viongozi kuhusu kukabili ugaidi barani Afrika ulioandaliwa kwa pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili ugaidi na uhalifu pamoja na serikali ya Nigeria ambao utafanyika mwezi Oktoba mwaka 2023,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa mkutano huo utakuwa ni fursa ya kuzingatia za kuimarisha usaidizi wa Umoja wa Mataifa katika kukabili ugaidi barani Afrika.