Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kalobeyei ni mfano wa utekelezaji bora wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi- Grandi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi alipotembelea makazi ya wakimbizi ya Kalobeyeina kambi ya Kakuma  kaunti ya Turkana nchini Kenya na kujionea jinsi wakimbizi na wenyeji wanavyonufaika pamoja na mir…
© UNHCR/Pauline Omagwa
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi alipotembelea makazi ya wakimbizi ya Kalobeyeina kambi ya Kakuma kaunti ya Turkana nchini Kenya na kujionea jinsi wakimbizi na wenyeji wanavyonufaika pamoja na miradi inayofadhiliwa na UN.

Kalobeyei ni mfano wa utekelezaji bora wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi- Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi ambaye amezuru Kenya ameshuhudia ni kwa kiasi gani miradi inayoIenga wakimbizi na wenyeji inasaidia sio tu kuinua vipato vya pande zote bali pia kujenga utangamano, maelewano na amani kwenye makazi ya wakimbizi.

Wakati wa ziara hiyo ametembelea mtambo wa mdogo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya sola kwenye makazi ya wakimbizi ya Kalobeyei nje kidogo ya mji wa Kakuma, kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Bwana Grandi alipatiwa maelezo kuwa mradi huo wa sola unaofanikishwa na Benki ya Dunia unawezesha wenyeji na wakimbizi kujikwamua kiuchumi na kijamii kwa kupata umeme wa uhakika kwa saa 24.

Makazi ya wakimbizi ya Kalobeyei, ni mradi uliozinduliwa mwaka 2018 ili kutekeleza kivitendo azma ya kuwezesha wakimbizi kujitegemea, kujumuishwa katika huduma za kitaifa na kutumia pamoja na wenyeji huduma za kijamii.

Akiwa hapa Bwana Grandi ameshuhudia kushamiri kwa biashara za wakimbizi na wenyeji.

Mkimbizi kutoka Burundi aendesha biashara kwenye makazi ya wakimbizi Kalobeyei

Joel, mkimbizi kutoka Burundi ana duka la kunyoa nywele na pia anauza vipodozi ambaye anasema, “Nilifungua duka kama hili kwa sababu niliona kila siku watu wakihitaji vitu kama hivi wanaenda Kakuma. Hivyo nikafikiria nikaona nikifungua duka kama hili tutafaidika sote wakazi wa Kalobeyei, badala waende Kakuma. Ndio maana nikafungua duka hili la vipodozi vya wanawake. Stima imenisaidia sana kwa duka langu la kinyozi. Mpango wangu mwakani ni kununua vifaa vingine vikubwa vya kunyolea ili nifike kiwango ninachotaka.”

Mtambo wa sola unatupatia umeme saa 24- Mwenyeji Irene

Irene Kai mwenyeji mjasiriamali anaonekana akiwasha taa iliyoungwanishwa kwenye mradi wa nishati ya sola huku akiweka vinywaji kwenye jokofu anasema, “nashukuru sana kwani tangu wakimbizi waletwe hapa tumekuwa pamoja nao, manake hili eneo awali lilikuwa ni msitu na hakuna mtu alikuwa anaishi. Sasa hivi tunafanya biashara na wakimbizi. Na tangu huu umeme uletwe, kazi yetu imekuwa rahisi. Mimi nikiwa mfanyabiashara wa vinywaji, nauza  maji, soda, ninaweza pia kukamua matunda. Ninaweza kuchaji simu, redio yangu pia inaimba, televisheni inawaka, na nyumba nzima ina umeme kwa saa 24. Tunafanya biashara na wakimbizi na tuko na amani nao.”

Ziara yangu hapa imenifungua macho sana- Grandi

Kamishna Mkuu Grandi baada ya kuona na kusikia akafunguka ya kwamba, “mwaka 2018, Umoja wa Mataifa ulipitisha Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi. Hii ni mbinu ambayo Umoja wa Mataifa inapatia nchi wanachama kusimamia njia bunifu, zenye kanuni na majawabu mujarabu ya mienendo mikubwa ya wakimbizi. Naweza kusema kuwa uwepo wangu wa siku nzima Kakuma na hapa Kalobeyei kaunti ya Turkana na kwa ukarimu mkubwa na uwazi wa mamlaka za hapa na ushirikiano wa wadau wote, nilichoshuhudia ni utekelezaji wa Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi.”

Akiwa Kenya, Kamishna Mkuu Grandi alikutana pia kwa mara ya kwanza na Rais William Ruto wa Kenya ambapo amesisitiza tena azma ya UNHCR ya kushirikiana na serikali mpya ya Kenya katika kulinda na kusaka majawabu kwa wakimbizi sambamba na kuhamasisha usaidizi wa maendeleo kwa jamii za wenyeji.

Halikadhalika alitumia fursa hiyo kushukuru Kenya kwa kuendelea kupokea na kuhifadhi wakimbizi.