Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makato makubwa ya utoaji hewa chafuzi yahitajika ili kufikia malengo ya 2030- UNEP

mitambo ya nishati kisukuku kama vile petroli na dizeli ndio inayoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi
© Unsplash/Marcin Jozwiak
mitambo ya nishati kisukuku kama vile petroli na dizeli ndio inayoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi

Makato makubwa ya utoaji hewa chafuzi yahitajika ili kufikia malengo ya 2030- UNEP

Tabianchi na mazingira

Wakati huu ambapo madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanashika kasi duniani kote na kusongesha ujumbe kuwa utoaji wa hewa chafuzi lazima upunguzwe kwa kiasi kikubwa, ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP imebaini kuwa jamii ya kimataifa bado inashindwa kufikia viwango vya kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo Ripoti hiyo iliyotolewa leo jijini Nairobi, Kenya na  ikipatiwa jina Pengo la Utoaji hewa chafuzi: Dirisha linafunga – janga la tabianchi lataka marekebisho ya jamii, inabaini kuwa marekebisha ya haraka na mapana katika sekta za usambazaji umeme, viwanda, usafirishaji na ujenzi,  halikadhalika mifumo ya chakula na fedha yanaweza kusaidia kuepusha janga la tabianchi.

Mwaka uliopotea

Ripoti hiyo ya 13 inayotolewa kila mwaka na UNEP kuangazia viwango vya utoaji hewa chafuzi kwa mwaka 2030 na viwango vya sasa inasema licha ya uamuzi wa serikali kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa tabianchi, COP26 huko Glasgow, Uingereza, wa kuongeza viwango vya michango yao vya kitaifa, NDCs ili kupunguza hewa chafuzi, bado viwango havitoshelezi.

Michango iliyowasilishwa mwaka huu itapunguza tani za milioni 500 pekee za ujazo za hewa ya ukaa, kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia moja ya lengo la mwaka 2030.

Dunia inaenda mrama

Ripoti inasema kukosekana kwa maendeleo hayo kunamaanisha kuwa dunia inaelekea kwenye ongezeko la kiwango cha joto na kushindwa kudhibiti kuvuka nyuzi joto 2 au 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amesema, “ripoti hii inatueleza kisayansi kile ambacho mazingira yamekuwa yanatueleza mwaka mzima, kupitia mafuriko, vimbunga na mioto ya nyika isiyozimika. Lazima tuache kujaza hewa chafuzi kwenye anga letu na tusitishe hivyo mara moja na haraka.”

Ameongeza “tulikuwa na fursa ya kuleta mabadilika makubwa, lakini fursa hiyo haijatoweka. Marekebisho madogo ya uchumi wetu na jamii zetu unaweza kutuokoa dhidi ya janga tabianchi.”

Ripoti inasema kuwa ili kufikia viwango vya mkataba wa Paris, dunia lazima ipunguze utoaji wa hewa chafuzi kwa viwango visivyo vya kawaida katika kipindi cha miaka minane ijayo.

Ulaji kidogo wa nyama na ulaji zaidi wa vyakula vya mboga za majani unaweza kupunguza hewa chafuzi kwa kuwa kinyesi cha ng'ombe kinatoa hewa ya Methani inayoharibu mazingira
Unsplash/Jo-Anne McArthur
Ulaji kidogo wa nyama na ulaji zaidi wa vyakula vya mboga za majani unaweza kupunguza hewa chafuzi kwa kuwa kinyesi cha ng'ombe kinatoa hewa ya Methani inayoharibu mazingira

“Inaonekana ni kazi kubwa, wengine wanaweza kusema haiwezekani kufanyia marekebisho uchumi wa dunia na kupunguza kwa asilimia 50 utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2030, lakini lazima tujaribu,” amesema Bi. Andersen akiongeza kuwa hata kiwango kidogo cha hatua kikichukuliwa kina athari chanya kwa jamii zilizo hatarini na kwa kila mmoja.

Hatua za kuchukua

Ripoti inasema ingawa hatua zinachukuliwa kuelekea kuhakikisha hewa chafuzi inayozalishwa inaondolewa angani, au net zero émission kwa kiingereza kwenye sekta za  usambazaji umeme, viwanda, usafirishaji na kwenye majengo, bado kasi inahitajika zaidi.

« Usambazaji umeme umesonga mbele kiteknolojia, kwa kuwa gharama za umeme unaozalishwa kwa nishati rejelezi imepungua. Hata hivyo kasi ya kipindi cha mpito kuelekea nishati rejelezi iongezwe, » imesema ripoti hiyo.

Kwa upande wa mifumo ya uzalishaji chakula ambayo inachangia theluthi moja ya hewa chafuzi, ripoti inapendekeza uhifadhi wa mifumo anuai asilia, kubadilisha vyakula ambavyo watu wanakula na kuhakikisha uzalishaji wa vyakula mashambani hauzalishi hewa ya ukaa.

Kiuchumi, ripoti inasema harakati za uchumi zitoazo kiwango kidogo cha hewa chafuzi zitahitaji uwekezaji wa angalau dola trilioni  4 hadi 6 kwa mwaka.

Uchimbaji wa mafuta ghafi ni moja ya visababishi vikubwa vya utoaji wa hewa chafuzi. Hii ni sehemu ya mafuta kisukuku ambayo Katibu Mkuu wa UN anataka jamii ya kimataifa iachane nayo.
© Unsplash/Zbynek Burival
Uchimbaji wa mafuta ghafi ni moja ya visababishi vikubwa vya utoaji wa hewa chafuzi. Hii ni sehemu ya mafuta kisukuku ambayo Katibu Mkuu wa UN anataka jamii ya kimataifa iachane nayo.

Guterres asema tuzibe pengo kabla janga halijatuziba

Akizungumzia ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema dirisha la kuchukua hatua kwa tabianchi linafunga kwa kasi kubwa mno.

“Nchi zisipochukua hatua haraka kukabili janga la tabianchi, dunia itakumbwa na zahma kubwa ya kimataifa,” ameonya Katibu Mkuu.

Ripoti ikionesha kuwa harakati zote za kupunguza viwango ya joto duniani itaongeza kiwango cha joto duniani hadi nyuzi joto 2.8 katika kipimo cha selsiyasi badala ya 1.5 kinachotakiwa, Katibu Mkuu amesema  hali ni mbaya akitaka nchi zipitishe maamuzi ya kijasiri katika michango yao ya kitaifa, au NDSs ya kupunguza utoaji hewa chafuzi.

Kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, kila nchi inatakiwa kutangaza michango yake au NDCs na kuifanyia tathmini kila mwaka. Licha ya wito wa kutakiwa kufanya hivyo, ripoti inaonesha mwelekeo wa kurudi nyuma.

Mapendekezo yako wazi

“Mapendekezo ya ripoti ya leo yako dhahiri,” amesema Katibu Mkuu akiongeza “tuondokane na utegemezi wa mafuta kisukuku. Tuepuke kuanzisha miundombinu mipya ya uzalishaji wa mafuta kisukuku. Tuwekeza kwa wingi zaidi kwenye nishati rejelezi isiyoharibu mazingira.”

Katibu Mkuu amesema kuweka ahadi za kuhakikisha hewa chafuzi inayozalishwa inashughulikiwa, haina maana yoyote iwapo hakuna mipango, sera nah atua za kutekeleza.

Amekumbusha kuwa dunia haiwezi tena kukubali kuweko kwa kampuni zinazolaghai kuhusu udhibiti wa mazingira, “tunapaswa kuziba pengo la utoaji hewa chafuzi kabla janga la tabianchi halijatufunika sote.”