Je uliko kuna utangamano na wanyamapori au ndio mizozano ?
Je uliko kuna utangamano na wanyamapori au ndio mizozano ?
Leo ni siku ya wanyamapori duniani ambapo ujumbe ni Ubia katika uhifadhi wa wanyamapori ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema ni fursa ya kutathmini wajibu wa kila mtu katika kulinda upekee wa uwepo wa aina mbali mbali za spishi za uhai katika sayari duniani.
Binadamu na kasi ya kutowesha mimea na wanyamapori
Katika ujumbe wake wa leo Katibu Mkuu anasema tunatambua kushindwa kwetu katika wajibu huo kwa sababu shughuli za kibinadamu zinatowesha maeneo kama vile misitu ambayo iliwahi kuwa misitu minene, mashamba, bahari, mito na maziwa.
Spishi milioni za mioto na mimea iko hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa makazi yao, uchafuzi kutokana na mafuta kisukuku na janga la tabianchi linaloshika kasi kila uchao.
Katibu Mkuu anasema ni lazima kutokomeza vita hivyo dhidi ya mazingira na kwamba bahati nzuri mbinu tunazo, halikadhalika ufahamu na majawabu.
Mkataba wa kimataifa wa biashara ya viumbe vilivyoko hatarini kutoweka
Miongoni mwa mawajabu hayo anayosema Katibu Mkuu ni pamoja na Mkataba wa kimataifa wa biashara ya viumbe vilivyoko hatarini kutoweka, CITES ambapo amesema, “mwaka huu ni miaka 50 tangu upitishwe na umesaidia sana kulinda maelfu ya mimea na wanyama. Na mkataba wa mwaka jana wa Kunming-Montreal kuhusu Mfumo wa Bayonuai duniani uliashiria hatua muhimu kuelekea njia ya kuponya sayari yetu.”
Watu wa jamii ya asili wana ufahamu wa uhifadhi kuliko wanasayansi
Kwa Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP, pamoja na mikataba iliyoko, majawabu mengine ni kuimarisha ubia na watu wa jamii ya asili na jamii kwenye maeneo husika ili wasiwe tu washiriki bali pia waongoze, waamue na waoneshe njia inayotakiwa. “Kwa sababu hebu na tukubali kuwa watu wa jamii ya asili wanafahamu zaidi uhifadhi kuliko hata wanasayansi.”
Amesema UNEP inafurahia kufanya kazi kwa ushirikiano wa ubia kwa ajili ya usimamizi endelevu wa wanyamapori kwa kushirikiana na Sekretarieti ya CITES, CBD na Mkataba wa kimataifa wa ndege wanaohamahama pamoja na mashirika mengine yanayofanya kazi katika masuala hayo.
“Katika siku ya wanyamapori duniani hebu na tuahidi kuimarisha ubi ana mazigira. Kwa sababu mustakabali wetu na wa spishi zote duniani unategema ubia huo,” ametamatisha Bi. Ingersen.
UN tufanye kazi kwa ukaribu zaidi na serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi
Na kwa Guterres wito wake ni kwa Umoja wa Mataifa kufanya kazi na serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ili kubadili ahadi kuwa vitendo.
“Na tunahitaji hatua za kijasiri zaidi kupunguza hewa chafuzi, kuchochea matumizi ya nishati endelevu na kujenga mnepo kwa tabianchi. Kote kule tunahitaji Saudi za jamii na watu wa jamii ya asili ambao ndio walinzi fanisi zaidi wa bayonuai na wako mbele na katikati.”
Ametamatisha ujumbe wake akisema “leo na kila siku hebu na tutekeleze wajibu wetu wa kuhifadhi makazi ya asili na kujenga mustakabali unaochanua kwa viumbe vyote.”
Kwa nini 3 Machi?
Tarehe 20 mwezi Desemba mwaka 20213, mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliamua kutangaza tarehe 3 Machi kila mwaka kuwa siku ya wanyamapori duniani kusherehekea na kuinua uelewa wa wanyama na mimea duniani. Tarehe hiyo ndio siku ambayo mwezi Machi mwaka 1973 ulipitishwa mkataba wa kimataifa wa biashara ya wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka, CITES.