Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN imezitunuku harakati 10 zinazorejesha mifumo ya ikolojia

Mwanamke nchini Mali anatunza shamba ya jamii ambayo ni sehemu ya mradi wa kujenga uwezo wa Chakula Duniani.
WFP/Simon Pierre Diouf
Mwanamke nchini Mali anatunza shamba ya jamii ambayo ni sehemu ya mradi wa kujenga uwezo wa Chakula Duniani.

UN imezitunuku harakati 10 zinazorejesha mifumo ya ikolojia

Tabianchi na mazingira

Muongo wa Umoja wa Mataifa juu ya Urejesho wa mfumo wa Ikolojia leo umetambua harakati 10 zinazoendelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kurejesha mazingira asilia

Harakati hizo zilizoshinda tuzo zimetangazwa leo katika kongamano la Umoja wa Mataifa la bayoanuai (COP15) huko Montreal Canada na tukio maalum lililofanyika mtandaoni na kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri na baadhi ya viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa. 

Tamasha hilo limeandaliwa na mwanajiografia kutoka India na mtayarishaji filamu wa wanyamapori Malaika Vaz. 

Lengo la harakati hizo 

Harakati hizo zilitangazwa kuwa ni bendera ya urejeshaji wa ikolojia ya dunia na inastahiki kupokea uchagizaji wa Umoja wa Mataifa, ushauri au ufadhili unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.  

Na harakati hizo zimechaguliwa chini ya bendera ya “Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kurejesha mfumo wa ikolojia”, ambalo ni vuguvugu la kimataifa linaloratibiwa na UNEP na FAO.  

Imeanzishwa ili kuzuia na kubadili mwenendo wa uharibifu wa maliasili katika sayari nzima 

Kwa pamoja, harakati hizo 10 bora zinalenga kurejesha zaidi ya ekari milioni 68 za eneo kubwa kuliko Myanmar, Ufaransa au Somalia na kuunda karibu fursa za kazi milioni 15. 

Katika kutangaza harakati hizo za urejeshaji ikolojia Ulimwenguni, Muongo wa Umoja wa Mataifa unataka kuenzi mifano bora ya urejeshaji wa mfumo ikolojia kwa kiwango kikubwa na wa muda mrefu, unaojumuisha kanuni 10 za urejeshaji za muongo wa Umoja wa Mataifa juu ya kurejesha mfumo wa ikolojia. 

Muongo wa Umoja wa Mataifa unatambua muda unaohitajika kwa juhudi hizo za kurejesha ikilojia ili kutoa matokeo.  

Jamii ya watu wa asili wanalinda msitu kama huu.
CIFOR/Terry Sunderland
Jamii ya watu wa asili wanalinda msitu kama huu.

Kauli za viongozi wa UN 

Mkurugenzi mtendaji wa UNEP Inger Andersen amesema"Kubadilisha uhusiano wetu na asili ni ufunguo wa kubadili migogoro mitatu inayoikabili sayari yetu ambayo ni mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayoanuwai, na uchafuzi wa mazingira na taka. Harakati hizi 10 za juhudi za urejeshaji bayoanuai Ulimwengu zinaonyesha kuwa kwa utashi wa kisiasa, sayansi, na ushirikiano wa kuvuka mipaka, tunaweza kufikia malengo ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa urejeshaji wa mfumo wa ikolojia na kuunda mustakabali endelevu zaidi sio tu kwa sayari bali pia kwetu sote tunaitiida sayari hiyo nyumbani.” 

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa FAO, Qu Dongyu amesema "FAO, pamoja na UNEP, kama viongozi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa urejeshaji wa mfumo wa ikolojia, tnafurahi kuzitunza harakati hizi 10 za urejeshaji wa mfumo wa ikolojia kama washindi wa mwaka 2022. Kwa kuhamasishwa na harakati hizi, tunaweza kujifunza kurejesha mifumo yetu ya ikolojia kwa uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora na maisha bora kwa wote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma.” 

Harakati 10 zilizotambuliwa na kushinda tuzo 

Mkataba wa asili wa msitu wa Atlantiki  

Msitu wa Atlantiki wakati mmoja ulifunika eneo la Brazil, Paraguay na Argentina. Lakini umepunguzwa vipande vipande kwa karne nyingi za ukataji miti, upanuzi wa kilimo na ujenzi wa jiji. 

Mamia ya mashirika yanafanya kazi katika juhudi za miongo kadhaa za kulinda na kurejesha msitu katika nchi zote tatu.  

Juhudi zao ni kuunda upenyo wa a wanyamapori hususan kwa viumbe vilivyo hatarini kutoweka, kama vile jaguar na simba wa tamarin, kupata maji kwa ajili ya watu na asili, kukabiliana na kujenga mnepo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, na kuunda maelfu ya ajira. 

Baadhi ya ekari 700,000 tayari zimerejeshwa huku lengo la mwaka 2030 likiwa ekari milioni 1 na lengo la mwaka 2050 ni ekari milioni 15. 

Urejeshaji wa ikolojia bahari ya Abu Dhabi 

Kulinda aina ya wanyama wa baharini waitwao dugong ambao idadi yao ni ya pili kwa ukubwa duniani ni lengo la harakati katika Umoja wa Falme wa nchi za Kiarabu kurejesha chakula kinachopendelewa na dugong, miamba ya matumbawe na mikoko kwenye pwani ya Ghuba. 

Mradi huo Abu Dhabi utaboresha hali ya mimea na wanyama wengine wengi, ikijumuisha aina nne za kasa na aina tatu za pomboo.  

Jamii za wenyeji zitafaidika kutokana na kufufuliwa kwa baadhi ya aina 500 za samaki, pamoja na fursa kubwa zaidi za utalii wa mazingira. 

Abu Dhabi inataka kuhakikisha mazingira yake ya pwani yanakuwa na mnepo dhidi ya hali ya joto duniani na maendeleo ya haraka ya pwani katika kile ambacho tayari ni mojawapo ya bahari zenye joto zaidi duniani. 

Takriban ekari 7,500 za maeneo ya mwambao tayari zimerejeshwa huku ekari nyingine 4,500 zitarejeshwa katika ikolojia yake ifikapo mwaka 2030. 

Urejeshaji ikolojia ya ukuta mkubwa wa kijani na amani 

Ukuta mkubwa wa kijani ni harakati kabambe za kurejesha ikolojia ya savanna, nyasi na mashamba Afrika ili kusaidia familia na viumbe hai kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuzuia kuenea kwa jangwa kutokana na kutishia zaidi jamii ambazo tayari ziko hatarini. 

Ulizinduliwa na Muungano wa Afrika AU mwaka 2007, na harakati hizi zinalenga kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu katika eneo la Sahel kwa kuunda ukanda wa mandhari ya kijani na yenye tija katika nchi 11. 

Malengo ya mwaka 2030 ya ukuta mkubwa wa Kijani ni kurejesha ekari milioni 100, kuvuna tani milioni 250 za hewa ukaa na kuunda nafasi za kazi milioni 10. 

Ufufuaji wa mto Ganges 

Harakati nyingine ni kurejesha afya ya mto Ganges, mto mtakatifu wa India, ni lengo la msukumo mkubwa wa kupunguza uchafuzi wa mazingira, kujenga upya misitu na kuleta manufaa mbalimbali kwa watu milioni 520 wanaoishi karibu na bonde kubwa la mto huo. 

Mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu, ukuaji wa viwanda na umwagiliaji vimeharibu mto Ganges kwenye chanzo chake cha kilomita 2,525 kutoka Himalaya hadi Ghuba ya Bengal. 

Harakati hizi zilizinduliwa mwaka wa 2014, na ni mpango unaoongozwa na serikali. 

Pia inalenga kufufua aina kuu za wanyamapori, ikijumuisha pomboo wa mtoni, kasa wa ganda laini, siri, na samaki aina ya hilsa shad. 

Glaciers nchini Chile na Argentina zimepungua sana katika miongo miwili iliyopita.
WMO
Glaciers nchini Chile na Argentina zimepungua sana katika miongo miwili iliyopita.

Mpango wa nchi mbalimbali wa milima  

Nchi za milima zinakabiliwa na changamoto za kipekee. Mabadiliko ya tabianchi ni kuyeyuka kwa barafu, kumomonyoka kwa udongo na kusababisha aina mbalimbali za viumbe kupanda mlima na mara nyingi kuelekea kutoweka.  

Maji ambayo milima hutoa kwa mashamba na miji katika maeneo tambarare ya chini yanazidi kutokuwa ya kutegemewa. 

Mpango huo ulioko Serbia, Kyrgyzstan, Uganda na Rwanda unaonyesha jinsi miradi hiyo katika maeneo matatu tofauti inavyotumia urejeshaji ili kufanya mifumo ya ikolojia ya milimani kuwa na mnepo ili iweze kusaidia wanyamapori wao wa kipekee na kutoa manufaa muhimu kwa watu. 

Uganda na Rwanda ni nyumbani kwa mojawapo ya wakazi wawili waliosalia wa sokwe wa milimani walio hatarini kutoweka.  

Shukrani kwa ulinzi wa makazi yao, idadi ya sokwe hao imeongezeka maradufu katika miaka 30 iliyopita.  

Nchini Kyrgyzstan, wafugaji wanasimamia maeneo ya malisho kwa njia endelevu zaidi ili watoe chakula bora kwa mifugo na mbuzi wa Asia.  

Chui wa theluji wanarejea polepole. Nchini Serbia, mamlaka inapanua wigo wa upandaji miti na kufufua malisho katika maeneo mawili ya hifadhi.  

Dubu wa kahawia wamerejea misituni, ambapo urejeshaji pia unasaidia mifumo ya ikolojia kupona kutokana na moto wa nyika. 

Hifadhi ya marejesho ya ikolojia nchi za visiwa vidogo 

Hatakati hizi zinaangazia nchi tatu za visiwa vidogo vinayoendelea Vanuatu, St Lucia na Comoro. 

Harakati hizi zinakuza urejeshaji wa mfumo wa kipekee wa ikolojia na kugusa ukuaji wa uchumi wa buluu ili kusaidia jamii za visiwa kujinasua kutoka kwenye athari za janga la COVID-19

Malengo ni pamoja na kupunguza shinikizo kwenye miamba ya matumbawe, ambayo ni hatari kwa uharibifu wa dhoruba, ili akiba ya samaki iweze kupona. Mifumo ya ikolojia inayorejeshwa pia inajumuisha mwani wa baharini, mikoko na misitu. 

Harakati zingine zilizoshinda 

Harakati zingine zilizoshinda ni pamoja na mradi wa hifadhi ya mazingira wa Altyn Dala ulioko nchini Kazakhstan,ambao umekuwa ukifanyakazi tangu mwaka  2005 kurejesha mifumo ya ikolojia katika sehemu za jangwa na nusu jangwa  nchini humo. 

Harakati nyingine ni Ukanda kame wa Amerika ya Kati. Ikikabiliwa na mawimbi ya joto na mvua isiyotabirika, mifumo ya ikolojia na watu wa ukanda kame wa Amerika ya Kati wako hatarini zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi.  

Mwaka 2019, mwaka wa tano wa ukame uliwaacha watu milioni 1.2 katika eneo hilo wakihitaji msaada wa chakula. 

Kutumia mbinu za kitamaduni za kilimo ili kujenga tija ya mandhari, ikiwa ni pamoja na bayoanuwai, ndio kiini cha urejeshaji huu unaojumuisha nchi sita ambazo ni Costa Rika, El Salvador, Guatemala, Honduras, Nicaragua na Panama. 

Harakati za ujenzi mpya na asili Indonesia: Demak, jamii ya maeneo ya chini ya pwani kwenye kisiwa kikuu cha Java cha Indonesia, yamekumbwa na mmomonyoko wa ardhi, mafuriko na upotevu wa ardhi unaosababishwa na kuondolewa kwa mikoko kwa ajili ya mabwawa ya ufugaji wa samaki, ardhi ndogo na miundombinu. 

Badala ya kupanda tena miti ya mikoko, harakati hii bunifu ya kurejesha ikolojia imejenga miundo kama ua yenye nyenzo asilia kando ya ufuo ili kutuliza mawimbi na kunasa mashapo, na hivyo kutengeneza mazingira ya mikoko kurudi tena.  

Urefu wa jumla wa upenye uliojengwa ni kilomita 3.4 na ekari 199 za mikoko zimerejeshwa. 

Kwa ajili ya kuruhusu mikoko kuzaliana upya, wakulima wamefundishwa katika mbinu endelevu ambazo zimeongeza uzalishaji wao wa kamba.  

Pamoja na mikoko kutoa makazi kwa viumbe vingi vya baharini, wavuvi pia wameona upatikanaji wa samaki wao wa karibu ukiboreka. 

Na harakati ya mwisho ni mradi wa Shan-Shui nchini China: 

Mpango huu kabambe unachanganya miradi mikubwa 75 ya kurejesha mifumo ya ikolojia, kuanzia milima hadi miamba ya pwani, katika taifa lenye watu wengi zaidi duniani. 

ulizinduliwa mwaka wa 2016, na mpango huo unatokana na mbinu ya utaratibu ya kurejesha mifumo ya ikolojia.  

Miradi inaambatana na mipango ya kitaifa ya anga, inafanya kazi katika eneo au maeneo ya maji, inajumuisha maeneo ya kilimo na mijini na pia mifumo ya asili, na kutafuta kukuza tasnia nyingi za ndani na yote inajumuisha malengo ya bioanuwai.