Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano ni muhimu kwenye dharura za kimataifa: Guterres

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akutana na Nguyen Xuan Phuc, Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam.
UN Photo/Minh Hoang
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akutana na Nguyen Xuan Phuc, Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam.

Ushirikiano ni muhimu kwenye dharura za kimataifa: Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa ili kukabiliana na dharura za hali ya hewa wakati wa ziara yake nchini Viet Nam.

Guterres aliyeko ziarani nchini humo amefanya mikutano na Rais, Nguyen Xuan Phuc, Waziri Mkuu, Pham Minh Chinh, na maafisa wengine wakuu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Bui Thanh Son, na Waziri wa Mazingira, Tran Hong Ha.

Katika mikutano hiyo amesema mshikamano unahitaji zaidi kipindi hiki kwakuwa ulimwengu uko hatarini kutokana na janga la COVID-19, athari za vita vya Ukraine, hitaji la haki, pamoja na mambo mengine yanayohitaji mshikamano na ushirikiano zaidi.

"Na hakuna mahali tunapohitaji zaidi na kwa haraka zaidi  kuliko katika mapambano yetu dhidi ya shida zinazoibuka kutokana na mabadiliko ya tabianchi," alisema. Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba hatua dhidi ya hasara na uharibifu ni sharti la kimaadili ambalo lazima liwe kipaumbele na kitovu cha mazungumzo katika COP27.

Mkuu huyo wa UN katika ziara yake nchini humo alitembelea kituo cha masuala ya hali ya hewa na nguvu za maji pamoja na kushiriki shughuli nyingine za utunzaji wa mazingira. 

Ulinzi wa amani

Katibu Mkuu aliwasili Viet Nam siku ya Ijumaa na kushiriki katika sherehe ya kuadhimisha miaka 45 ya nchi hiyo kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Alisifu ushirikiano mkubwa wa nchi hiyo na Umoja wa Mataifa, na "safari yake ya ajabu" katika kipindi hiki, ambayo alielezea kama hadithi ya mabadiliko na matumaini, iliyoandikwa na watu wa Vietnam.

"Zaidi ya kizazi kimoja kilichopita, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walikuwa nchini Viet Nam wakipeleka msaada wa chakula kwa nchi iliyoharibiwa na vita, iliyojitenga, na iliyokuwa kwenye ukingo wa janga la njaa," alikumbuka.  "Leo, ni walinda amani wa Kivietinamu wanaokuja kusaidia watu katika sehemu fulani za ulimwengu zilizokata tamaa."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameungana na vijana wa Kivietinamu katika ngoma ya kitamaduni ya Kireno katika Chuo cha Diplomasia cha Viet Nam.
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameungana na vijana wa Kivietinamu katika ngoma ya kitamaduni ya Kireno katika Chuo cha Diplomasia cha Viet Nam.

Mazungumzo na vijana

Katibu Mkuu pia alishiriki katika mazungumzo na wawakilishi wa vijana wa Vietnam na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini humo, mazungumzo hayo yalifanyika katika Chuo cha Diplomasia chini ya kaulimbiu ya ‘Uvumbuzi na Ushiriki kwa ajili ya Baadaye Jumuishi na Endelevu.’

Alisisitiza kuwa mshikamano ndiyo njia pekee ya kuondokana na janga la mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine zinazojitokeza sasa au zinazojitokeza duniani.

"Tunakabiliwa na hatari ya magonjwa mapya. Tunakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa duniani. Kuna njia moja tu ya kutoweza kushindwa na changamoto hizi, nayo ni kama tutajiunga na juhudi, ikiwa tutakuja pamoja. Na kwa hilo tunahitaji kuhisi mshikamano wa kweli.”

Akiwa katika Chuo hapo Guterres pia alipanda miti pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Viet Nam, Bui Thanh Son.