Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kimataifa ni nguzo kwa dunia na kila mmoja:Guterres

 Ufunguzu wa  mkutano wa Mataifa ulifanyika Geneva tarehe 15 Novemba 1920
UN Photo/Jullien
Ufunguzu wa mkutano wa Mataifa ulifanyika Geneva tarehe 15 Novemba 1920

Ushirikiano wa kimataifa ni nguzo kwa dunia na kila mmoja:Guterres

Masuala ya UM

Ushirikiano wa kimataifa na diplomasia vimethibitisha kuwa na faida na huduma muhimu kwa watu wote duniani kuanzia masuala ya utekelezaji wa sheria za kimataifa, usawa wa kijinsia, ulinzi wa mazingira, hadi kuzuia uzalishaji wa silaha za maangamizi na hata magonjwa hatari duniani, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa maadhimisho ya kwanza ya kimataifa hii leo ya “siku ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani”

Katika ujumbe huo kwenye hafla ya maadhimisho hayo yanayofanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Guterres amesema maadhimisho haya ya kwanza yanadhihirisha tahamani ya ushirikiano wa kimataifa kwa ajili masuala mazuri ya pamoja. Ameongeza kuwa “kwa karibu miaka 75, mfumo wa ushirikiano ulioanzishwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia umeokoa maisha , umekuza uchumi na maendeleo ya kijamii, umedumisha haki za binadamu na pia kusaidia kuzuia zahma ya tatu ya kimataifa.”

Guterres amesisitiza hata hivyo kuwa ushirikiano huo hauwezi kuchukuliwa kirahisi, kwani dunia ya sasa inaangukia wakati ambao juhudi za ushirikiano wa kimataifa ziko katika shinikizo kubwa kuanzia kwenye migogoro isiyotatulika, mabadiliko ya tabianchi yanayokimbia kwa kasi, pengo linaloongezeka la kutokuwepo usawa na vitisho vingine duniani.

Maendeleo ya teknolojia

Katibu Mkuu amesema ingawa teknolojia imeleta fursa nyingi lakini pia imeleta uwezekano wa kuvuruga masoko ya ajiramahusiano ya kijamii na kufurahia haki za binadamu.”Tunaishi katika hali ambayo changamoto za kimataifa zimeshikamana lakini hatua zetu za kuzikabili zinaendelea kugawanyika. Tunashuhudia ongezeko la kupoteza Imani na serikali, wanasiasa, mashirika ya kimataifa na kuongezeka kwa wito kwa kukumbatia utaifana sauti za waliomashuhuri ambavyo vinaharibu na kugawanya. Hii ni hatari kubwa katika changamoto za sasa ambapo hatua zetu za pamoja ni muhimu sana”

Nini kifanyike

Guterres ameasa kwamba katika mtihani huu “tunahitaji kukumbuka haja ya haraka waliyoihisi waanzilishi wa Umoja wa Mataifa, na kuimarisha zana za shirika hili. Misingi ya kufanya kazi pamoja ili kufanikiwa, lakini lazima kutilia maanani dunia inavyobadilika haraka. “

Katibu mkuu amesisitiza kuwa dunia inahitaji ahadi imara zaidi za  kufuata mfumo wa sheria, na ufanisi katika Umoja wa Mataifa kuwa kitovu. Kunahitajika mtandao wa pamoja wa ushirikiano wa karibu miongoni mwa mashirika ya kimataifa na kitaifa ikiwemo benki za maendeleo. Na kwa kuwa serikali na mashirika ya kimataifa hawawezi kufanya hili peke yao basi”tunahitaji ujumuishwaji ambao miziz yake ni ushirikiano na jumuiya za biashara, asasi za kiraia, mabunge, wanazuoni , wanajamii na wadau wengine hususan vijana.” Hata hivyo amesema haitoshi kutangaza tu ushirikiano “Ni lazima tuthibitishe faida yake, na si jambo linalokubalika kuwapuuza wanaoutilia mashaka, ni lazima tuonyeshe kwamba ushirikiano wa kimataifa unaweza kukabiliana na changamoto za kimataifa na kuleta utandawazi wa kimataifa utakaokidhi matakwa ya wote.”

Muhimili wa Umoja wa Mataifa

Guterres amesema katiba ya Umoja wa Mataifa inaonyesha njia kwa watu nan chi kuishi kama majirani wazuri, wakitetea maadili ya kimataifa na kutambua mustakabali wetu wa pamoja.

Kwa kuimarisha ushirikiano kunamaanisha ni “kuimarisha jukumu letu la kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDG’s na kujenga dunia salama na yenye haki Zaidi kwa vizazi vijavyo. Na ahadi hiyo inahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote , kuanzia kwa Umoja wa Mataifa, kwa viongozi na raia kila mahali.”