Mabadiliko ya tabianchi ni kichocheo tosha cha mizozo-UN

11 Julai 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuangazia masuala ya tabianchia na athari zake kwa usalama ambapo Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo amesema, “ni lazima tuelewe mabadiliko ya tabianchi kama suala moja katika mkusanyiko wa vichocheo ambavyo vinaweza kusababisha mzozo” akiongeza kuwa huongeza mzigo juu ya hali dhaifu ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Ni dhahiri kuwa mabadiliko ya tabianchi ni tishio la kweli na kwamba yanaongezeka kwa kasi kubwa.

Hiyo ni moja ya mada nne alizozungumzia Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina .J. Mohammed wakati wa hotuba yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja huo hapa New York, Marekani katika kikao kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi hii leo.

Bi. Mohammed amesema, wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zimetapakaa kwa viwango tofauti katika kila eneo, hamna nchi ambayo itaepuka athari za muda mrefu.

Kwa mantiki hiyo Naibu Katibu huyo amesema, “ni lazima tufanye kazi pamoja na kwa nia moja. Hii ndio fursa itakayotuwezesha kutafuta suluhu endelevu kwa changamoto hii.”

Hoja nyingine aliyozungumzia Bi. Mohammed ni athari za mabadiliko ya tabianchi kuathiri maeneo mengine zaidi ya mazingira pekee akisema kuwa nchi zilizo katika hatari ya mabadiliko ya tabianchi ndizo ziko katika hatari kubwa ya mizozo.

OCHA/Otto Bakano
Familia huko nchini Burkina Faso ikienda kusaka maji. Nchini humo zaidi ya watu 950,000 hawana uhakika wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame na hivyo kukwamisha shughuli za kilimo na ufugaji.

Ametolea mfano bonde  la ziwa Chad amesema, akisema eneo hilo linakabiliwa na mzozo uliosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na masuala ya kibinadamu na kimazingira, na kuongeza kuwa “kupungua kwa ukubwa wa Ziwa Chad kwa asilimia 90 tangu mwaka 1960 kumesababisha uharibifu kwenye mazingira, kutengwa kiuchumi na kijamii na ukosefu wa usalama na kuathiri watu milioni 45.”

Naibu Katibu huyo amesema athari za mabadiliko ya tabianchi pia zimesababisha uandikishwaji wa vijana kwenye vikundi vyenye misimamo mkali kwa mfano Boko Haram.

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa unakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika ngazi tofauti ikiwa hiyo ndio hoja yake ya nne mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama.

Ni lazima tuelewe mabadiliko ya tabianchi kama suala moja katika mkusanyiko wa vichocheo ambavyo vinaweza kusababisha mzozo

Amesema Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama huangazia suala hilo na ndio maana umoja huo unapatia Baraza hilo taarifa muhimu wakati wa kujadili suala hilo.

Bi. Mohammed ametolea mfano ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu Ofisi ya Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi na eneo la Sahel na kubainisha kuwa ripoti itaangazia maendeleo yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi na usalama katika eneo hilo.

Katika mada ya nne na ya mwisho Bi.Mohammed ametoa changamoto, nini kifanyike? akisema  “tunahitaji kuunga mkono programu zinazowaweka wanawake na vijana katika kiini cha juhudi zetu. Tunafahamu kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinaathiri wanawake kwa kiwango kikubwa.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud