Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 2.2 wana uoni hafifu au upofu duniani kote:WHO 

Baadhi ya matatizo ya ugonjwa wa kisukari ni upofu,kiharusi na kuharu figo.Roseane wa Brazil ana aina ya pili ya Kisukari.
WHO/Eduardo Martino
Baadhi ya matatizo ya ugonjwa wa kisukari ni upofu,kiharusi na kuharu figo.Roseane wa Brazil ana aina ya pili ya Kisukari.

Watu bilioni 2.2 wana uoni hafifu au upofu duniani kote:WHO 

Afya

Shirika la afya duniani WHO limetoa rai ya kuhakikisha fursa ya huduma za macho zilizo bora, jumuishi na kwa wote zinapatikana wakati huu ambapo takriban watu bilioni 2.2 kote duniani wanaishi na changamoto ya uoni hafifu au upofu. Taarifa zaidi inasomwa na Happiness Pallangyo wa Radio washirika Uhai FM. 

Kwa mujibu wa WHO ambayo leo inaadhimisha siku ya uoni duniani,nchi za Kusini Msashariki mwa Asia ndizo zilizoathirika zaidi na matatizo ya uoni hafifu au upofu zikibeba asilimia 30 ya watu wote bilioni 2.2 walio na matatizo ya uoni. 

Limezitaka nchi hizo kuongeza juhudi ili kuhakikisha kwamba kila mtu, kila mahali anapata ufikiaji sawa wa huduma za afya ya macho za viwango vya juu, na za kina, kulingana na mpango mpya wa utekelezaji wa kikanda wa mwaka 2022-2030 uliopitishwa kwa ajili ya huduma ya macho inayotoa kipaumbele kwa watu.  

Shirika hilo limeongeza kuwa angalau visa bilioni 1 vya ulemavu wa kuona vingeweza kuzuiwa au bado havijashughulikiwa. Shirika hilo la WHO limesisitiza kwamba matatizo ya macho yanaathiri watu wa aina zote za maisha , hata hivyo “Watoto wadogo na wazee ndio walio hatarini zaidi. Pia wanawake, watu wa vijijini na makundi ya walio wachache wana uwezekano mkubwa kuliko makundi mengine kuwa na uoni hafufu na ni nadra kwao kupata huduma zinazostahili za macho.” 

Mtoto wa miaka 4 Dinh akihudhuria shule ya watoto wenye upofu au uoni hafifu nchini Vietnam
UNICEF/Ehrin Macksey
Mtoto wa miaka 4 Dinh akihudhuria shule ya watoto wenye upofu au uoni hafifu nchini Vietnam

Takwimu za shirika hilo la afya duniani zinaonyesha kuwa "Mwaka 2020 makadirio ya hasara za kiuchumi zilizotokana na uoni hafifu au upofu duniani kote zilifikia dola bilioni 411, huku idadi ya watu wenye matatizo ya kutoona karibu ikitarajiwa kuongezeka kutoka watu bilioni 1.8 mwaka 2015 hadi kufikia watu bilioni 2.1 ifikapo mwaka 2030. "

Ili kusongesha haraka mchakato wa kukabiliana na changamoto hiyo ya macho WHO imependekeza mambo matatu ya kuzingatia, "Mosi kujumuisha huduma za macho katika huduma zilizopo za afya, pili kuimarisha nguvukazi ya wahudumu wa afya ya macho,  na tatu kuongeza fursa ya upatikanaji wa vifaa vya msaada, teknolojia mpya na kuchagiza utafiti. "

Siku ya uoni duniani huadhimishwa kila mwaka Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba na ilipitishwa kwa lengo la kutanabaisha kuhusu afya ya macho na upofu duniani.