Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la chakula duniani: FAO yataka ushirikiano kila mtu apate lishe bora kokote aliko

Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima huko Taita nchini Kenya
© FAO/Fredrik Lerneryd
Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima huko Taita nchini Kenya

Janga la chakula duniani: FAO yataka ushirikiano kila mtu apate lishe bora kokote aliko

Msaada wa Kibinadamu

Shamrashamra zimefanyika hii leo huko Roma, Italia zikiwa na ujumbe wa Hakuna wa Kuachwa nyuma, katika kuhakikisha kila mtu anapata chakula tena chenye lishe bora, shughuli ambayo ni kuelekea siku ya kimataifa ya chakula duniani tarehe 16 mwezi huu wa Oktoba.

Maadhimisho yanafanyika huku hali ya uhakika wa kupata chakula ikizidi kutoweka duniani kote hususan barani Afrika na Asia.

Siku ya chakula duniani huadhimishwa kukumbuka kuanzishwa kwa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO tarehe 16 Oktoba mwaka 1945 ambapo wakati wa sherehe za leo kulikuwa na ujumbe kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Mkuu wa Kanisa katoliki duniani, Papa Francis na Rais wa Italia Sergio Mattarella.

Maeneo mbalimbali yaweka mabango ya kidijitali

Wito wa kuchukua hatua ulisambazwa kwa njia mbalimbali katika mataifa 150 duniani kote, kwingine wakiweka mabango ya kidijitali katika lugha tofauti tofauti, kuanzia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali, Rwanda, hadi sanamu ya Kristo Mkombozi iliyoko Rio de Janeiro, Brazil.

Mafunzo ya FAO mkoani Kigoma yamewezesha wanakikundi kutumia viazi lishe kutengeneza juisi, na kupika maandazi, chapati na kukaanga chipsi.
FAO Tanzania
Mafunzo ya FAO mkoani Kigoma yamewezesha wanakikundi kutumia viazi lishe kutengeneza juisi, na kupika maandazi, chapati na kukaanga chipsi.

Katika ujumbe wake Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema, janga la uhaba wa chakula likishamiri, “tunahitaji kutumia nguvu yetu ya mshikamano na umoja wetu kujenga mustakabali bora ambamo kwamo kila mtu anaweza kupata lishe bora na ya kutosha.”

Kando yaw tau 970,00 walio hatarini kukumbwa na baa la njaa Afghanistani, Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia na Yemeni, idadi ya watu wenye njaa duniani kote inaongezeka na kufikia watu milioni 828 mwaka 2021, kwa muijbu wa ripoti ya hivi karibuni zaidi ya FAO ya hali ya uhakika wa chakula na lishe duniani na watu bilioni 3.1 bado hawana uwezo wa kupata lishe bora.

Wanawake, vijana, watu wa jamii ya asili na wakulima wako hatarini zaidi

Na kama ilivyo kawaida, walio hatarini zaidi ndio wanaoathirika zaidi na sasa hivi imejidhihirisha wazi ni wanawake, vijana, watu wa jamii ya asili na wakulima. Hawa mara nyingi wanahaha kupata mafunzo, fedha, teknolojia na ubunifu ili kurahisisha kazi zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UN Bwana Guterres amesema siku ya chakula duniani inaadhimishwa kukiwa na janga kubwa la ukosefu wa uhakika wa chakula. “wadau tushirikiane ili tuachane na kukata tamaa badala yake tulete matumaini.”

Papa Francis katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake ametaka washiriki kutopoteza mwelekeo wa suala kwamba watu si idadi tu au takwimu, au mlolongo wa takwimu.