Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kimataifa ya maandishi ya nukta nundu inaelezea njia muhimu ya mawasiliano kwa mamilioni-UN

Mshiriki akitumia kifaa chenye maandishi ya nukta nundu wakati wa mkutano wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu 2018
UN Photo/Manuel Elías
Mshiriki akitumia kifaa chenye maandishi ya nukta nundu wakati wa mkutano wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu 2018

Siku ya kimataifa ya maandishi ya nukta nundu inaelezea njia muhimu ya mawasiliano kwa mamilioni-UN

Haki za binadamu

Ikiwa inaadhimishwa kwa mara ya pili ulimwenguni, hii leo siku ya maandishi ya nukta nundu inakuza uelewa kuhusu umuhimu wa mfumo thabiti wa mawasiliano ya ulimwengu yanayosaidia kuwawezesha wasioona na wenye uoni hafifu kutambua kikamilifu haki zao za binadamu.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, inakadiriwa kwamba takribani watu bilioni 2.2 wana uoni hafifu au upofu, huku watu bilioni moja kati yao wakiwa pengine tatizo lao halijashughulikiwa au ambao ulemavu wao ungeweza kuzuilika.

Watu wenye upungufu wa kuona, wanakuwa zaidi katika nafasi ya kuwa na viwango vya juu vya umaskini kuliko wale ambao hawana tatizo hilo.

Kutotimizwa kwa mahitaji yao, au haki zao, kuna madhara mapana ambapo kupoteza uoni mara nyingi huwakilisha kukosekana kwa usawa katika maisha yao yote, afya duni, vikwazo vya kupata elimu na ajira.

Maandishi ya nukta nundu huleta lugha ya maandishi mbele kama sharti la muhimu kwa ajili ya kukuza uhuru wa msingi.

Mkataba wa mwaka 2006 kuhusu haki za watu wenye ulemavu, ambao umeboresha haki na ustawi wa watu wenye ulemavu, unatambua maandishi ya nukta nundu kuwa ni muhimu kwa elimu, uhuru kwa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na ujumuishwaji.

Katika ya agenda yam waka 2030 ya maendeleo endelevu, iliyoidhinishwa mwaka 2015, inaahidi zaidi kwamba hakuna mtu atakayeachwa nyuma, kwa lengo la kuhakikisha kila binadamu anaweza kuyafurahia maisha.

Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa uliidhimisha rasmi siku ya nukta nundu, tarehe kama ya leo mwaka jana 2019 kwa kutambua umuhimu wa machapisho ya nukta nundu kama njia muhimu ya mawasiliano kwa wasioona na pia kuwawezesha kundi hilo na wale wenye uoni hafifu kupata haki yao ya msingi ya mawasiliano.

Nukta nundu ni nini?

Nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.

Mbinu hii inatokana na mgunduzi wake Louise Braille kutoka Ufaransa ambaye aliigundua karne ya 19.