Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upofu unaokabili watu bilioni 1 ungaliweza kuepukwa iwapo wangalipata tiba - WHO

Centrine akiwekewa dawa ya macho baada ya kuchunguzwa kwenye kliniki ya macho kwa ajili ya manusura wa Ebola mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
WHO/J. D. Kannah
Centrine akiwekewa dawa ya macho baada ya kuchunguzwa kwenye kliniki ya macho kwa ajili ya manusura wa Ebola mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Upofu unaokabili watu bilioni 1 ungaliweza kuepukwa iwapo wangalipata tiba - WHO

Afya

Takribani watu bilioni 2.2 duniani kote wana uoni hafifu au upofu, kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya, limesema shirika la afya duniani, WHO, hii leo katika ripoti yake ya kwanza kuhusu hali ya uoni duniani. 

Ripoti hiyo iliyozinduliwa leo huko Geneva, Uswisi kuelekea maadhimisho ya siku ya uoni duniani tarehe 10 mwezi huu wa Oktoba, inasema kuwa  wagonjwa bilioni 1 kati yao hao wangaliweza kupona iwapo wangalipatiwa tiba mapema au huduma za kinga.

WHO inasema watu hao wanakabiliwa na magonjwa kama vile kutoona mbali au karibu, mtoto jicho, macho mekundu na presha ya macho au glakoma.

Mkazi nchini Kenya akipatiwa huduma ya kupima macho
Sebastian Liste/NOOR
Mkazi nchini Kenya akipatiwa huduma ya kupima macho

Walio maskini zaidi wako hatarini kupata upofu- Dkt. Tedros

“Idadi kubwa zaidi  ya watu hao iko katika nchi za kipato cha chini na kati”, amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO akiongeza kuwa hali ni mbaya zaidi kwa wakazi wa vijijini ambako magonjwa ya macho hayatibiwi ipasavyo kwenye maeneo hayo kutokana na ukata.

Dkt. Tedros amesema haikubaliki watu milioni 65 wanapata upofu, au wanapata shida ya kuona ilhali tatizo hilo lingaweza kutibiwa kwa upasuaji wa siku moja tu wa mtoto wa jicho au watu milioni 800 wanahaha kila siku kutokana na kushindwa kununua miwani.

Ametaka serikali kujumuisha huduma za macho kwenye mipango ya afya akisema ni muhimu katika kufanikisha safari ya huduma ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Mipango ya afya kitaifa iangazie pia magonjwa ya macho

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matatizo  ya macho ambayo  yanaweza kusababisha upofu au uhafifu wa uoni kama vile mtoto wa jicho na ugonjwa wa vikope, yanapaswa kujumuishwa kwenye mikakati ya afya ya kitaifa ya kinga lakini magonjwa ya macho yasiyosababisha upofu kama vile jicho macho mekundu hayapaswi kupuuzwa kwa sababu ni miongoni mwa sababu ya watu kusaka huduma ya afya.

Ugonjwa wa kisukari aina ya II nao umetajwa kuathiri uwezo wa mtu kuona iwapo hautatambulika mapema ambapo ripoti inasema kuwa, “takribani wagonjwa wote wa kisukari watakuwa na ugonjwa wa macho katika Maisha yao na hivyo ni lazima wafanyiwe uchunguzi mara kwa mara ili kuepusha kuathiri uwezo wao wa kuona.”

Hata kama mtu ana shida ya macho basi asaidiwe aweze kumudu maisha yake

Mwanafunzi mwenye uoni hafifu akifanya mazoezi ya kutumia mashine ya nukta nundu kwenye shule ya watu wasioona ya Al-Noor  huko Mogadishu nchini Somalia.
UN Photo/Ilyas Ahmed)
Mwanafunzi mwenye uoni hafifu akifanya mazoezi ya kutumia mashine ya nukta nundu kwenye shule ya watu wasioona ya Al-Noor huko Mogadishu nchini Somalia.

Akizungumzia ripoti hiyo, Dkt. Alarcos Cieza, ambaye anaongoza harakati za WHO za kushughulikia upofu na uoni hafifu amesema, “mamilioni ya watu wana tatizo kubwa la kuona na hawawezi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii kwa sababu hawana uwezo wa kupata huduma za kuwajumuisha upya kwa kuzingatia hali mpya inayowakabilii.”

Dkt. Cieza amesema, “katika jamii ambayo imejikita katika uoni, huduma za macho ikiwemo ujumuishwaji lazima zisogezwe karibu na jamii ili kila mtu afikie uwezo wake wote.”

Ripoti inasema kuwa watu wote wenye shida ya macho na ambao hawawezi kupata  matibabu, bado wanaweza kuendesha maisha yao iwapo wakipatiwa huduma za kuwaweza kuishi katika mazingira mapya kwa kuzingatia uwezo wao wa kuona.

Mathalani kupatiwa mashine za nukta nundu waweze kusoma, miwani yenye kuongeza ukubwa wa taswira, simu janja za kuwawezesha kutembea na kuwaelekeza pa kwenda na kutembea kwa kutumia fimbo.