Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya nchi zote duniani hazina mifumuo ya kutoa taarifa za mapema kuhusu majanga

Watoto katika shule nchini Bali wakishiriki mafunzo ya kujikinga wakati wa tsunami
UNDRR/Antoine Tardy
Watoto katika shule nchini Bali wakishiriki mafunzo ya kujikinga wakati wa tsunami

Nusu ya nchi zote duniani hazina mifumuo ya kutoa taarifa za mapema kuhusu majanga

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza hatari za majanga UNDRR na Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani WMO iliyochapishwa hii leo, imeonya kuwa nusu ya nchi zote duniani kuwa hazina mifumo ya kutoa taarifa za mapema kuhusu majanga.

Ripoti ya mashirika hayo iliyotolewa huko jijini Geneva Uswisi ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupunguza madhara ya majanga duniani imeeleza kuwa idadi hiyo ni kubwa zaidi kwa nchi za kipato cha chini ambazo pia ndio zinazokabiliwa zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo chini ya nusu ya mataifa yanayoendelea yana mifumo ya kutoa taarifa za majanga na kwa upande wa nchi za visiwa vidogo ni theluthi moja tu yenye mifumo ya kuonya wananchi wao iwapo majanga yatatokea.

Kwa mujibu wa ripotoi hiyo, nchi zisizo na mifumo thabiti ya kutoa taarifa za kuonya kabla ya kutokea kwa majanga zinapata athari mara nane zaidi ikilinganishwa na nchi zenye mifumo thabiti ya kuonya wananchi wake.

 Dunia haijawekeza kwenye hili

Waathirika wa mafuriko kwenye eneo la Balochistan, nchini Pakistani.
WFP Pakistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zipo katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa duniania akieleza namna tabaka la ozoni linavyozidi kuathiriwa na kuongezeka kwa majanga akitolea mfano mafuriko yaliyoikumba nchi ya Pakistan hivi karibuni.

Guterres amesema “Watu wanahitaji kupata taarifa za haraka za kujiandaa kukabiliana na hali mbaya ya hewa ndio maana natoa wito kwa nchi zote katika kipindi cha miaka mitano kuhakikisha zina mifumo ya utoaji tahadhari za mapema. Utoaji wa tahadhari mapema na kuchukua hatua za haraka imethibitika kusaidia kuokoa maisha. “

Kupitia ujumbe huo alioutoa kwa njia ya video Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa “Ulimwengu unashindwa kuwekeza katika kulinda maisha na riziki za wale walio mstari wa mbele. Watu wale ambao wamefanya angalau uharibifu kidogo wa kusababisha mzozo wa hali ya hewa dunaini ndio wanaolipa bei kubwa zaidi,” akimaanisha nchi nyingi hususan zilizopo Afrika ambazo sasa zinakabiliwa na majanga kama vile njaa na ukame mkali kuwahi kushuhudiwa.

Mtoto akichota maji kwenye chanzo ambacho kinamaji kidogo kutokana na ukame uliokausha maziwa huko Dollow Somalia
© UNICEF/Sebastian Rich

 Umuhimu wa kuwekeza kwenye mifumo ya tahadhari

Ripoti ya UNDRR na WMO imeonesha kuwa nchi zinazoendelea na za visiwa vidogo na nchi barani Afrika, zinahitaji uwekezaji mkubwa zaidi ili kuongeza utoaji wa tahadhari za mapema na kujilinda wananchi wake vya kutosha dhidi ya majanga.

“Wakati ripoti hii ilipokuwa ikitayarishwa, tunashuhudia Pakistan ikiwa inakabiliana na maafa mabaya zaidi ya tabianchi yaliyorekodiwa, na karibu maisha ya watu 1,700 wamepoteza”, amesema Mami Mizutori, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa UNDRR.

Hata hivyo Mizutori amesema licha ya vifo hivyo, idadi ya vifo ingekuwa kubwa zaidi ikiwa sio mifumo ya tahadhari ya mapema.

“Cha kusikitisha ni kwamba ripoti hii inaangazia mapungufu makubwa katika ulinzi kwani ni nusu tu ya nchi duniani zenye Mifumo ya Tahadhari ya Mapema ya Hatari", aliongeza. "Hii ni hali ambayo inahitaji kubadilika haraka, kuokoa maisha, riziki, na mali”.

Kwa upande wake Petteri Taalas, Katibu Mkuu wa WMO, amesema idadi ya majanga yaliyorekodiwa imeongezeka mara tano, “yakisukumwa kwa sehemu kubwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu na hali mbaya zaidi ya hali ya hewa. Hali hii inatarajiwa kuendelea. Mifumo ya hadhari ya mapema ni kipimo kilichothibitishwa na chenye ufanisi cha kukabiliana na hali ya hewa, ambacho kinaokoa maisha na pesa”.

Familia ya raia wa Burundi mbele ya nyumba yao iliyoharibiwa na kimbunga Gombe, katika makazi ya wakimbizi ya Maratane, Msumbiji.
© UNHCR/Juliana Ghazi

Mkuu huyo wa WMO ametoa matumaini kwakueleza dunia inaweza na lazima ifanye vizuri zaidi kuhakikisha kuwa maonyo ya mapema yanawafikia walio hatarini zaidi na yanatafsiriwa katika hatua za mapema. “Hii ndiyo sababu WMO inaongoza mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maonyo ya Mapema kwa Wote katika miaka mitano ijayo.”

 Ubinadamu upo hatarini

Katibu Mkuu António Guterres alionya katika ujumbe wake wa siku hii kuwa majanga yanayoongezeka yanagharimu maisha na mamia ya mabilioni ya dola kwa hasara na uharibifu mkubwa, na akasimulia jinsi alivyojionea mwenyewe, uharibifu uliosababishwa na mafuriko ya hivi karibuni baada ya ziara yake nchini Pakistan.

“Watu wanayahama makazi yao mara tatu zaidi kutokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kuliko vita”nusu ya wanadamu tayari wako katika eneo la hatari”.

Ameeleza kwa masikitiko kuwa watu wanafumbia macho majanga ya mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea bila ya kuwa na tahadhari za awali na akisisitiza kwamba "watu wanahitaji onyo la kutosha ili kujiandaa na hali mbaya ya hewa”.

Mkuu huyo wa UN alihitimisha ujumbe wake kwa kurejea wito wake wa utoaji wa onyo la mapema kwa muda wa miaka mitano ijayo. “Mifumo ya tahadhari ya mapema - na uwezo wa kuifanyia kazi - imethibitishwa kuokoa maisha”.