Tahadhari ya mapema inaokoa maisha wakati wa Tsunami:UNDRR

Tsunami inaweza kuwa moja ya hatari mbaya zaidi na inayokatili maisha ya watu wengi amesema mwakilishi wa Katibu Mkuu na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya upunguzaji hatari za majanga UNDRR Mami Mizutori.
Kupitia ujumbe wake wa siku ya uelimishaji kuhusu Tsunami Mizitori amesema “Licha ya uharibifu mkubwa unaoletwa na tsunami, onyo au tahadhari ya mapema na hatua za mapema zinasalia kuwa nyenzo zetu bora zaidi ya kulinda watu dhidi ya tsunami.”
Ameongeza kuwa maarifa haya ni ya thamani sana, kiasi kwamba jamii nyingi za asili za pwani zimeyapitisha kutoka vizazi hadi vizazi kupitia hadithi na nyimbo.
Ameongeza kuwa “Sasa tuna teknolojia na mbinu za kuhakikisha kila jamii ya pwani inalindwa na mfumo wa tahadhari za mapema dhidi ya tsunami, lingawa mapungufu bado yapo.”
Ametaja mambo matatu ya muhimu kuhusu tsunami na kuokoa maisha ya watu ambapo amesema
Kwanza, mifumo ya tahadhari ya mapema lazima ishughulikie kila mtu aliye hatarini, haijalishi anaishi umbali gani au anazungumza lugha gani.”
Pili, mifumo ya tahadhari ya mapema ya tsunami inapaswa kuwa ya tahadhari za hatari nyingi kwa sababu sio tsunami zote zinasababishwa na matetemeko ya ardhi.
Na Tatu, hata wakati mifumo imewekwa, jamii wakati mwingine hazijui hatari zinazowakabili au jinsi ya kukabiliana na maonyo au thahadhari. Jamii lazima ziwe tayari kuchukua hatua mapema.
Katika siku hii ya uelimishaji kuhusu Tsunami duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 5 Bi. Mizutotri amesisitiza kwamba “Hebu tujitolee kuziba mapengo haya kwa kufikia lengo G la mkakati wa Sendai ili kupanua tahadhari ya mapema na hatua za mapema kwa kila mtu. Hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma wakati tsunami inapopiga.”