Skip to main content

Kupanda kwa bei ya mafuta na chakula kuongeza gharama za operesheni za WFP Afrika kwa dola milioni 136  

Mtoto akikula uji wenye virutubisho kwa ajili ya kuzuia utapiamlo Mauritania.
© WFP/Bechir Malum
Mtoto akikula uji wenye virutubisho kwa ajili ya kuzuia utapiamlo Mauritania.

Kupanda kwa bei ya mafuta na chakula kuongeza gharama za operesheni za WFP Afrika kwa dola milioni 136  

Ukuaji wa Kiuchumi

Gharama za uendeshaji za shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP,  kwa mwaka huu wa 2022 zitaongezeka kwa dola milioni 136 katika ukanda wa Afrika Magharibi pekee kutokana na athari za vita vya Ukraine ambazo zinaongeza bei ya chakula na mafuta duniani.  

Hii ni kwa sababu ya njaa kali katika eneo hilo ambayo imeongezeka mara nne katika kipindi cha miaka mitatu na kufikia kiwango cha juu zaidi kwa kipindi cha miaka 10 mwaka huu, huku wanawake, wanaume na watoto milioni 43 wakitarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula ifikapo Juni 2022. 

Gharama hii ya ziada kwa operesheni za WFP ingeweza kutumika kuwapa watoto wa shule milioni sita mlo wa kila siku wenye lishe kwa kipindi cha miezi sita.  

WFP inasema hili ni jambo la kusikitisha kwani mamilioni ya familia katika eneo hilo haziwezi kukidhi mahitaji yao ya msingi ya chakula kutokana na mgogoro wa chakula ambao haujawahi kushuhudiwa, unaosababishwa na mizozo, mabadiliko ya tabianchi, kuporomoka kwa uchumi kulikosababishwa na janga la COVID-19 na bei ya juu ya vyakula. 

“Kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta hakutaweka tu mamilioni ya watu katika hatari ya njaa pia kunailazimisha WFP kuwa katika hali isiyowezekana ya kuchukua chakula kutoka kwa wenye njaa ili kulisha wenye njaa," amesema Chris Nikoi, Mkurugenzi wa WFP wa Kanda ya Afrika Magharibi. 

Msaada wa chakula kwa wati wa kijiji cha Madjoari, Burkina Faso.
© WFP/Cheick Omar Bandaogo
Msaada wa chakula kwa wati wa kijiji cha Madjoari, Burkina Faso.

Nchi zilizoathirika zaidi 

Kwa mujibu wa WFP nchi za Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Burkina Faso, Cameroon, Mali na Niger kutokana na ufadhili mdogo, na kutokana na mzozo unaoendelea nchini Ukraine, bandari na wasambazaji bidhaa hawapatikani tena na shehena kutoka bahari nyeusi zikicheleweshwa au kufutwa tu, na hivyo kuathiri shughuli za WFP katika  eneo lote la Afrika Magharibi.  

Katika kukabiliana na mzozo wa chakula na lishe ambao haujawahi kushuhudiwa Afrika Magharibi, WFP inaongeza hatua zake ili kufikia watu milioni 22 kwa msaada wa kuokoa maisha na kujenga mnepo.  

Watu hao wanajumuisha wanawake, wanaume na watoto milioni nane wanaohitaji chakula kingi katika nchi za G5 Sahel ambazo ni Burkina Faso, Chad, Mali Mauritania, na Niger, wakati wa msimu wa kilimo duni na muambo unaoanza Juni, hadi kipindi cha baada ya mavuno mwezi Oktoba. 

Nini kifanyike 

 Ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mpango wake wa kukabiliana na njaa katika kanda hiyo, WFP inahitaji kwa dharura dola milioni 951 katika kipindi cha miezi sita ijayo. 

"Tunahitaji kuongeza msaada wetu wa kuokoa maisha ili kupunguza athari kwa familia zilizo hatarini. Lakini usaidizi huu muhimu wa dharura unapaswa kuambatanishwa na uingiliaji kati wa muda mrefu, kwa kuimarisha mifumo ya kitaifa na hifadhi ya jamii, ili kupunguza mahitaji ya kibinadamu kwa wakati na kuandaa mipango bora kuelekea suluhisho endelevu kwa matatizo ya njaa na utapiamlo. Tuna ushahidi kutoka kwa jamii yote ya kanda hiyo kwamba hili linafanya kazi," ameongeza Nikoi.