Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwezo na rasilimali za kushamiri mtoto wa kike ziko ndani yake: Mwandishi Yejide Aina

Yejide Aina, Afisa Mtendaji Mkuu wa The Illuminator, shule ya mtandaoni anayoitumia kupigania haki za mtoto wa kike.
Yejide Aina
Yejide Aina, Afisa Mtendaji Mkuu wa The Illuminator, shule ya mtandaoni anayoitumia kupigania haki za mtoto wa kike.

Uwezo na rasilimali za kushamiri mtoto wa kike ziko ndani yake: Mwandishi Yejide Aina

Wanawake

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya mtoto wa kike mwaka huu ikibeba mauadhui “Wakati wetu ni sasa, haki zetu, mustakbali wetu” tunafunga safari hadi Nigeria kwa mwanaharakati wa kuleta mabadiliko, mchagizaji wa masuala ya elimu, na mwandishi wa vitabu Yejide Aina.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watoto wa kike wakielimishwa , wakipatiwa huduma wanaostahili na wakiwezeshwa kutambua haki zao za binadamu basi wanaweza kufikia uwezo wao na kuifanya dunia kuwa mahala bora pa kuishi kwa ajili yao na jamii zao kwa ujumla kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Lakini kufanikisha hayo yote watoto wa kike wanahitaji muongozo na miongoni ambao ni jukumu la kila mtu kuhakikisha wanaupata.

Miongoni mwa wanaotimiza wajibu huo ni mwandishi wa vitabu na mwanaharakati wa kimataifa wa kuleta mabadiliko Yejide Aina kutoka nchini Nigeria.

Mwandishi mbobevu wa vitabu

Kitabu kilichoandikwa na Yejide Aina kwa jina Personal Agility au 'Wepesi Binafsi' wa mto wa kike kuyaelewa mazingira au mambo haraka.
Yejide Aina

Yedije ni mwandishi mbobevu na mbali ya kitabu chake hiki kipya ambacho ni mahsusi kwa ajili ya mtoto wa kike wa zama hizi za kidijitali kinachoitwa “5 Tips on personal Agility for today’s Girl” kikimaanisha vidokezo vitano muhimu vya kumfanya mtoto wa kike kushamiri na maisha yake kuwa mepesi, ameshaandika vitabu vingine vine lakini hapa anaanza kwa kutueleza kuhusu kitabu hicho kipya “Kitabu 5 Tips on personal Agility for today’s Girl kilizaliwa ili kumuelimisha na kumuinua mtoto wa kike , kumsaidia kuweka njia na muongozo wa kufanya ndoto zake kutimia. Naweza kukielezea kama mwongozo wa kuwapa mafunzo viongozi wasichana.”

Na je kwa nini Yejide ameamua kujikita na mtoto wa kike? “Kujikita na mtoto wa kike ni muhimu sana kwa sababu naamini kwamba wakati fikra za mtoto wa kike zimeelimika, maisha yake yanabadilika, huu ni wakati muafaka kwa wasichana kuanza kuwa na fikra za juu. Pili unapoinua hali za kiuchumi za wasichana na wanawake unachokifanya ni kuinia hali za kiuchumi za familia, na unapoinua hali za kiuchumi za familia kwa ujumla unainua jamii, unainua taifa zima na binadamu wote wanafaidika na hilo.”

Kitabu kilichoandikwa na Yejide Aina kwa jina Personal Agility au 'Wepesi Binafsi' wa mtoto wa kike kuyaelewa mazingira au mambo haraka.
Yejide Aina

Videkozo vitano muhimu

Yejide pia anaendesha shule mtandaoni iitwayo Illuminator Academy ambapo lengo ni lele lile kuhakikisha elimu na ujumbe unamfikia mtoto wa kike kama ilivyo kwenye kitabu hiki chenye vidokezo vitano. Anafafanua kidokezo kimoja baada ya kingine ambavyo mosi ni “Ukuaji wa kifikra. Msichana anatakiwa kuwa tayari kujifunza vitu vipya na kuelewa kwamba fursa mara nyingi zimejificha katika changamoto. Kidokeze cha pili ni kuwa na maono ya maisha yako, ni swali kama nini leongo lako katika maisha. Kidokezo cha tatu ni kukumbatia mabadiliko, usiyakubali tu mabadiliko lakini uyakumbatie ikimaanisha kubeba wajibu wa ubunifu na uvumbuzi wako katika maisha”

Tweet URL

Yejide ameendelea kufafanua kuwa kidekezo cha nne ni “Upekee wako, nakipenda sana kidokezo hiki namaanisha karama na kipaji ulichopewa na Mungu ni kitu kilicho cha kipee kwako hivyo unapaswa kukimiliki. Kisha nazungumzia watu walio karibu nawe. Kila wakati hakikisha unazungukwa na watu wenye fikra chanya watu ambao wanakuhamasisha na hiyo inabadili kila kitu. Na kujipunguzia mzigo hicho ni kidokezo cha tano ambacho kinamsongesha mbele kila mtoto wa kike maishani, kitakupa utulivu na safari isiyo na vizingiti maishani na ukikikosa itakuchelewesha.”

Na kwa watoto wote wa kike hii leo siku yao Yejide ana ujumbe maalum “Mustakbali wako ni sasa sio miaka 20 ijayo au miaka 30 ijayo , kesho yako inaanza ndani yako. Una haki ya kupata elimu bora, una haki ya kuwa na afya njema, una haki ya kusikilizwa, una haki ya usawa na una haki ya kuishi bila ukatili. Unapaswa kupewa fursa ya uongozi na kiti kwenye meza ya maamuzi, na haya yanapaswa kufanyika kwa kukuweka kuwa kitovu cha mabadiliko.”

Na ili kuhakikisha ujumbe wa kitabu chake kws ajili ya mtoto wa kike unawafikia wengi popote walipo, Yedije ametafsiri kitabu hicho kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili.