Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza kwa wasichana ni kuwekeza katika mustakabali wetu wa pamoja:Guterres 

Kuwapa wasichana fursa kuongoza kwa kuwafanya kitovu cha mabadiliko ni njia mojawapo ya kuwekeza katika kuamini uwezo wa wasichana
© UNFPA Burkina Faso/Théo
Kuwapa wasichana fursa kuongoza kwa kuwafanya kitovu cha mabadiliko ni njia mojawapo ya kuwekeza katika kuamini uwezo wa wasichana

Kuwekeza kwa wasichana ni kuwekeza katika mustakabali wetu wa pamoja:Guterres 

Wanawake

Katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike leo mkuu wa Umoja wa Mataifa ameiita kumbukumbu hiyo kuwa ni sherehe ya "maisha na mafanikio ya wasichana duniani kote". 

Antonio Guterres kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii yam toto wa kike duniani amesema "Wasichana wanaposaidiwa kutambua haki zao za kibinadamu, wanaweza kufikia uwezo wao na kufanya ulimwengu kuwa bora kwao na jamii zao". 

Ameendelea kusema kwamba Watoto wa kike wanapoweza kuwa shuleni, "Wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha yenye afya, yenye tija na yenye kuridhisha". 

Wasichana wanaposaidiwa wanaweza kufikia uwezo wao na kuufanya ulimwengu kuwa bora - Mkuu wa UN 

Kwa upatikanaji sahihi wa huduma za afya, "wanakua na kujiamini zaidi na uhuru wa miili yao  na wasichana wanapoelewa haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi bila tishio la unyanyasaji wana uwezekano mkubwa wa kukaa salama na kuripoti ukatili". Ameongeza Katibu Mkuu. 

Changamoto kubwa 

Hata hivyo, Bwana Gutereres amesema wasichana wanaendelea kukabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa za haki yao ya kupata elimu, ustawi wao wa kimwili na kiakili, na kuwa salama dhidi ya ukatili. 

Kutokana na elimu yao kuvurugika kwa kulazimishwa kukimbia majumbani mwao kutokana na migogoro, na kukosa uwezo wa kutekeleza haki zao za kingono na uzazi, janga la COVID-19 limefanya mizigo iliyopo kuwa mibaya zaidi, na limeondoa mafanikio muhimu yaliyopatikana katika muongo mmoja uliopita. 

Manusura wa tetemeko la ardhi nchini Afghanistan wakihudhuria darasa katika kituo cha kijamii kinachosaidiwa na UNICEF kwenye wilaya ya  Gayan District, jimboni Paktika
© UNICEF/Mark Naftalin

Wito wa kupata elimu 

Bwana Guterres ameeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea kutengwa kwa wasichana kuanzia shule ya upili nchini Afghanistan, akielezea kuwa sio tu “Kunawaathiri kwa kiasi kikubwa wasichana hao bali taifa zima ambalo linahitaji sana nguvu na michango yao. Hebu waacheni wasichana wasome", amewahimiza tena viongozi wa Taliban. 

Katibu Mkuu amesisitiza haja ya sasa zaidi ya wakati mwingine wowote kufufua upya dhamira ya kufanya kazi pamoja ili wasichana waweze kufurahia na kutumia haki zao, kushiriki kikamilifu na sawa katika jamii zao. 

"Kuwekeza kwa wasichana ni kuwekeza katika maisha yetu ya baadaye," amesema. 

Na kutoa wito kwamba "Katika siku ya kimataifa ya mtoto wa kike, tuongeze juhudi zetu ili kuhakikisha wasichana kila mahali wanakuwa na afya, elimu na salama". 

Muongo mmoja baadaye 

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Umoja wa Mataifa unasema, kumekuwa na ongezeko la umakini katika masuala ambayo ni muhimu kwa wasichana kwa upande wa serikali, watunga sera na umma kwa ujumla pamoja na fursa zaidi za sauti zao kusikika katika jukwaa la kimataifa. 

Kura ya maoni ya UNICEF inaripoti kuwa watoto na vijana wanasalia na matumaini na wenye mawazo ya kimataifa zaidi ikilinganishwa na vizazi vikubwa.
© UNICEF/Raphael Pouget

Hata hivyo, ameongeza kuwa uwekezaji katika haki za wasichana bado una kikomo huku wakiendelea kukabiliana na changamoto nyingi za kutimiza uwezo wao, ambazo zinafanywa kuwa mbaya zaidi na migogoro ya wakati mmoja ya mabadiliko ya tabianchi, COVID-19 na changamoto za kibinadamu. 

Licha ya hayo, Umoja wa Mataifa unashikilia kwamba pamoja na shida, huja uwezo, ubunifu, ukakamavu, na ustahimilivu. 

Wasichana vigori milioni 600 duniani kote wameonyesha mara kwa mara kwamba kutokana na ujuzi na fursa, wanaweza kuwa wabadilishaji wa maendeleo katika jamii zao, na kurejesha nguvu kwa wote, wakiwemo wanawake, wavulana na wanaume. 

Kulingana na Umoja wa Mataifa "Wasichana wako tayari kwa muongo mmoja wa kuongeza kasi mbele. Ni wakati wetu sote kuwajibika pamoja na wasichana na kuwekeza katika siku zijazo zinazoamini katika uharaka wao, uongozi na uwezo wao". 

Matumaini yameanza kujitokeza 

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake UN Women limesema, katika kipindi cha miaka 10 k​umeshuhudiwa ongezeko la wasichana waliovutiwa na masuala ya kimataifa na wanashiriki katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDGs kuanzia kwenye mabadiliko ya tabianchi, elimu, afya ya akili, ukatili wa kijinsia mpaka masuala ya uzazi salama na haki za wasichana. 

Ushiriki wao huu na uchechemuzi umechangia katika kuelimisha jamii katika ngazi ya mashinani