Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kombora la hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini linatishia amani na usalama - UN

Khaled Khiari ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa masuala ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki kwenye Idara ya Siasa ya Umoja wa Mataifa, akihutubia Baraza la Usalama.
UN /Rick Bajornas
Khaled Khiari ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa masuala ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki kwenye Idara ya Siasa ya Umoja wa Mataifa, akihutubia Baraza la Usalama.

Kombora la hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini linatishia amani na usalama - UN

Amani na Usalama

Siku mbili baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK kurusha kombora la masafa marefu kupitia anga la Japan, hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao kuhusu tukio hilo ambapo jamii ya kimataifa imetakiwa kuimarisha juhudi zake kutokomeza vitisho vya nyuklia.

Khaled Khiari ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa ametoa wito huo wakati akihutubia Baraza hilo Jumatano alasiri juu ya hatua za Umoja wa Mataifa kufuatia tukio hilo, sambamba na hofu yake kwa hali ya kibinadamu nchini DPRK ambayo hujulikana pia kama Korea Kaskazini.

Kombora hilo la masafa marefu lilirushwa kutoka jimbo la kaskazini la Jagang siku ya Jumatatu asubuhi ya saa za Korea Kaskazini na likavuka eneo la ardhi la kilometa 4,500 na umbali angani wa kilometa 970.

Mara ya mwisho kwa Korea Kaskazini kurusha kombora la masafa marefu kupita Japani ilikuwa tarehe 15 mwezi Septemba mwaka 2017.

Katibu Mkuu wa UN alaani

Bwana Khiari amerejelea kauli ya jumanne ya Katibu Mkuu wa UN ya kulaani tukio hilo la DPRK.

“Hiki ni kitendo cha hovyo na ni ukiukwaji dhahiri wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uzinduzi huu unatishia kuchochea kuendelea kwa mvutano kewnye ukanda huu na kwingineko,” amenukuu Bwana Khiari.

Amesema inatia hofu sana kwamba DPRK kwa mara nyingine tena inapuuza uzingatiaji wa kimataifa wa usalama wa safari za anga na majini.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres alisihi Korea Kaskazini kusitisha mara moja vitendo vya kuleta vurugu.

Ametoa wito kwa taifa hilo la barani Asia kurejea katika mashauriano kuelekea kuachana na kuendeleza nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Sheria mpya DPRK yatia hofu

Bwana Khiari amezungumzia jambo lingine linalotia hofu hivi sasa ni kwamba “Korea Kaskazini imezindua mifumo ambayo yenye sifa za makombora ya masafa mafupi katika matukio manne ya hivi karibuni.”

Mwezi uliopita, shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, liliripoti kuweko kwa viashiria vya mtambo wa majaribio ya nyuklia wa Punggye-ri kuwa na shughuli na kujiandaa kufanikisha jaribio la nyuklia.

Amesema IAEA inaendelea kufuatilia shughuli za ujenzi kwenye mtambo wa nyuklia wa Yongbyon pamoja na dalili ya kwamba mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 5 ulikuwa unafanya kazi.

Halikadhalika Katibu Mkuu ameeleza wasiwasi kufuatia kitendo cha DPRK cha kupitisha sheria mpya kuhusu sera ya nyuklia.

“Wakati baadhi ya nchi zinategemea silaha za nyuklia kwa ajili ya usalama, silaha za nyuklia zinatishia uwepo wa binadamu. Kuendelea kuweko kunahatarisha hali isiyotakiwa ya kuendeleza silaha au matumizi mabaya. Lazima tuimarishe jitihada zetu za kutokomeza silaha za nyuklia,” amesema Bwana Khiari.

Fanikisha misaada ya kibinadamu

AWakati huo huo, Bwana Guterres ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu DPRK akitaka Jamii ya kimataifa ifanikishe upelekaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo.