Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa UN unaokoa maisha ya maelfu DPRK: Lowcock

Msaidizi wa Katibu mkuu katika masuala ya kibindamu  na dharura Mark Lowcok akitembelea miradi ya kilimo ya FAO kusini mwa Hwanghae, Korea kaskazini
OCHA/Anthony Burke
Msaidizi wa Katibu mkuu katika masuala ya kibindamu na dharura Mark Lowcok akitembelea miradi ya kilimo ya FAO kusini mwa Hwanghae, Korea kaskazini

Msaada wa UN unaokoa maisha ya maelfu DPRK: Lowcock

Msaada wa Kibinadamu

Baada ya kutembelea miradi mbalimbali inayosaidiwa na Umoja wa Mataifa jimboni Hwanghae Jamhuri ya watu wa Korea au DPRK, msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, amesema msaada huo unabadili maisha ya maelfu ya watu.

Mark Lowcock amekuwa ziarani DPRK ili kuelewa mahitaji ya kibinadamu, kufahamu msaada unaotolewa na Umoja wa Mataifa na kuchagiza msaada zaidi kwa ajili ya watu wa taifa hilo.

Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali kikiwemo kituo cha kulelea watoto, kukutana na maafisa wa serikali , jumuiya ya wahisani na wadau wa misaada ya kibinadamu, Lowcock wakati akihitimisha ziara hiyo ya siku tatu leo mjini Pyongyang, amewaeleza waandishi wa habari kuwa mtihani unaolikumba taifa hilo ni mkubwa

 SAUTI YA MARK LOWCOCK 

“Jamhuri ya watu wa Korea ina changamoto nyingi , lakini mimi najikita na masuala ya kibinadamu , na masuala hayo muhimu ya kibinadamu ni utapia mlo, maji salama na usafi, na madawa ya kuokoa maisha na vifaa vingine vya hospital kama niliyozuru.”

 Ameongeza kuwa ingawa hatua kubwa zimepigwa katika masuala ya afya lakini kuna upungufu mkubwa wa dawa na vifaa akitolea mfano hospital ya jimbo la Sinchon ambayo ina wagonjwa 140 wa kifua kikuu lakini ina dawa za kutibu wagonjwa 40 pekee .

Amesema asilimia 20 ya watoto wa chini ya miaka 5 nchini humo wamedumaa na takribu nusu ya watoto wote vijijini hawana fursa ya kupata maji salama ya kunywa. Kwa mantiki hiyo amesema

SAUTI YA MARK LOWCOCK 

“Umoja wa Mataifa unajaribu kukusanya dola milioni 111 ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu katika maeneo ambayo nimeyazungumzia, afya, maji na usafi na uhakika wa chakula kwa watu takriban milioni 6. Muda mfupi kabla sijaanza ziara yangu tulipata asilimia 10 ya fedha hizo kutokana na msaada wa ukaribmu wa serikali za Sweden, Uswis na Canada, lakini bado tunasalia na pengo kubwa la ufadhili.”

Watu wa DPRK wamekabiliwa na madhila kwa miaka 20 sasa na Umoja wa Mataifa unataka kuona madhila hayo yanakoma. Mkuu huyo wa OCHA amerejea wito wake kwamba ufadhili zaidi unahitajika kuokoa maisha ya watu hao kwani umepungua kwa kiasi kikubwa tangu 2012, na kwa mwaka huu ni asilimia 11 tu ndiyo iliyopatikana katika jumla ya dola milioni 111 zinazohitajika.