Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusisubiri takwimu kamilifu kusaidia manusura wa ukatili wa kingono Ukraine- Pramila

Wanawake na watoto wakipanda treni kwenye kituo cha Lviv nchini Ukraine ili kuhamishiwa maeneo mengine yenye usalama,
© UNICEF/Nikita Mekenzin
Wanawake na watoto wakipanda treni kwenye kituo cha Lviv nchini Ukraine ili kuhamishiwa maeneo mengine yenye usalama,

Tusisubiri takwimu kamilifu kusaidia manusura wa ukatili wa kingono Ukraine- Pramila

Amani na Usalama

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo Pramila Patten amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo na kutaja aina ya vitendo vya ukatili wa kingono vilivyoripotiwa nchini Ukraine wakati huu ambapo zaidi ya siku 100 zimepita tangu Urusi kuvamia taifa hilo la Ulaya.

Bi. Patten ametaja vitendo hivyo kuwa ni ubakaji ikiwemo kubakwa kwa magenge, watu kulazimishwa kuwa uchi, watu kulazimishwa kushuhudia wake, waume au watoto wao wakibakwa, ujauzito baada ya kubakwa na tishio la kubakwa.

Mwakilishi huyo amewaeleza wajumbe hao waliokutana kujaidli ukatili wa kingono kwenye mizozo, hususan Ukraine, ya kwamba taarifa hizo alipatiwa na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine wakati wa ziara yake nchini humo.

“Mwendesha mashtaka Mkuu huyo alinijulisha kuwa kati ya tarehe 24 Februari hadi 12 mwezi Aprili mwaka huu, simu mahsusi ya kitaifa ya kupokea taarifa za ukatili majumbani, usafirishaji haramu binadamu na ubaguzi wa kijinsia ilipokea simu kuhusu matukio hayo,” amesema Bi. Patten.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo Pramila Patten  akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Ukraine
UN /Eskinder Debebe
Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo Pramila Patten akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Ukraine

Wanabakwa wanawake, wanaume, wasichana na wavulana

Kama hiyo haitoshi, amesema  hadi tarehe 3 mwezi huu wa Juni, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, ilipokea ripoti za matukio 124 yanayodaiwa kuhusisha ukatili wa kingono dhidi ya wanawake, wanaume, wasichana na wavulana kwenye maeneo ya Chernihiv, Dnipropetrovsk, Donetsk, Kharkiv,  Kherson, Kyiv, Luhansk, Mykolaiv, Vinnytsia, Zaporizhzhia, Zakarpattia, na Zhytomyr. 

Ametanabaisha kuwa mara nyingi manusura wa vitendo hivyo huhofia unyanyapaa na hivyo idadi inaweza kuwa kubwa zaidi.

“Vita ikiwa inaendelea, katu si wakati mzuri wa kuchukua takwimu. Lakini iwapo tutasubiri takwimu sahihi na basi tutachelewa,” amesema Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono vitani.

Mambo 5 ya kuzingatia

Ametaja mambo makuu matano ya kuzingatiwa ili kukabili ukatili wa kingono unaoendelea Ukraine: Mosi, kuimarisha utawala wa sheria na uwajibikaji wa vitendo hivyo. Pili kuimarisha uwezo wa vikosi vya ulinzi na usalama katika kuzuia ukatili wa kingono. 

Tatu, kuhakikisha manusura wa ukatili wa kingono pamoja na watoto wao wanapatiwa huduma za kina ikiwemo afya ya uzazi, kisaikolojia na kuwajumuisha tena kwenye jamii. Nne, kuendelea na mchakato wa kusitisha usamaka na kuhakikisha suala la ukatili wa kingono linajumuishwa kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Tano, kuhakikisha suala la usafirishaji haramu wa binadamu kwa lengo la kuwatumikisha kingono au kuwatumbukiza kwenye ukahaba linashughulikiwa.

Sherrie Westin, Rais wa taasisi ya Global Impact katika  Sesame workshop
UN
Sherrie Westin, Rais wa taasisi ya Global Impact katika Sesame workshop

Sesame Workshop yataja hatua inazochukua

Akihutubia mkutano huo, Sherrie Rollins Westin kutoka taasisi ya Sesame Workshop inayotoa mafunzo kwa watoto wakiwemo walioko kwenye vita na mizozo, amesema wako mstari wa mbele kusaidia watoto nchini Ukraine kwa kutambua kuwa, “kipindi muhimu zaidi cha mtoto ni kati ya umri wa kuzaliwa hadi miaka mitano. Tunashirikiana na Wizara ya Elimu na mipango yetu inaendana na mipango ya kitaifa.”

Ufaransa iko kidete na UNFPA

Akichangia mada hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Nicolas de Rivière amesema wanaguswa sana ripoti za ukatili wa kingono na iwapo zitathibitishwa, wahusika wafikishwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake. 

“Tuna hofu juu ya hatari zinazokabili wakimbizi wa ndani, na tunaunga mkono hatua za kuepusha usafirishaji haramu wa binadamu. Manusura wa ukatili wa kingono lazima walindwe na tunaunga mkono hatua za shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA,” amesema Balozi de Rivière.