Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma ya choo nyumbani yaleta nuru kwa kaya huko Accra ,Ghana

Choo kipya nyumbani kwa Agnes Djakwei kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra, mradi huu ni wa Benki ya Dunia.
Video ya Benki ya Dunia
Choo kipya nyumbani kwa Agnes Djakwei kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra, mradi huu ni wa Benki ya Dunia.

Huduma ya choo nyumbani yaleta nuru kwa kaya huko Accra ,Ghana

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya makazi duniani, ujumbe ukiwa Zingatia pengo lililoko, usimwache  nyuma mtu yeyote au eneo lolote, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema ukuaji wa miji lazima uende sambamba na uwekezaji siyo tu wa kuhakikisha kila mtu ana uwezo wa kupata nyumba ya  kuishi bali pia huduma muhimu kama vile za kujisafi, jambo ambalo huko nchini Ghana miradi inayowezeshwa na Benki ya Dunia imesaidia kaya ambazo zamani zilisubiri choo cha umma kisicho kisafi kujisaidia sasa zina huduma hiyo majumbani.

 

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Agnes Djakwei, mkazi wa moja ya vitongoji vya mji mkuu wa Ghana, Accra, ambaye ni mfanyabiashara mdogo na kutokana na ugonjwa anaonekana kwenye video ya Benki ya Dunia akijikongoja kuketi kwenye kiti ili aendelee na mapishi.

Bi. Djakwei anakumbuka machungu ya ukosefu wa choo akisema, “tulipokuwa hatuna choo nyumbani, tulitumia choo cha umma kilichoko eneo la Leshie au Akpesee. Foloni ilikuwa ndefu na ilitutia hofu na tulikuwa tunalipa fedha na wakati mwingine hatuna fedha. Ndio maana watu wengine walijisaidia haja kubwa kwenye mifuko halafu wanatupa kwenye pipa la taka. Sasa pipa la taka lisipopelekwa jalalani, unabakia nalo.”

Mkazi huyu wa jiji la Accra, anasema hali ilikuwa mbaya zaidi usiku, iwapo tumbo likivuruga akisema, unasali ukiomba kukuche! Kitandani unatetemeka.”

Ameenda mbali akisema na hata vyoo vya umma kuna wakati ni vichafu kwa kuwe watu wengine hawasafishi kwa maji wakishatumia, na hii ni hatari kwa afya.

Hata hivyo mradi wa Benki ya Dunia wa kusaidia GAMA ambayo ni mamlaka ya majisafi na majitaka ya jiji la Accra, Ghana ulileta nuru ambapo kupitia mradi huo kampuni ziliwezeshwa ujenzi wa vyoo katika jamii na kaya zikachangia gharama kidogo.

Sasa Bi. Djakwei ana choo nyumbani kwake na anasema, sasa hivi hatuko tena kwenye hatari ya magonjwa. Tunashukuru Mungu tuna choo nyumbani. Ukiugua tumbo, huna wasiwasi. Unaamka unaenda chooni na kutoka. Ni choo chako, unakitumia na kukisafisha mara kwa mara. Ni vema kila kaya kuwa na choo chake. Nashauri kila kaya iweke akiba ya fedha na hatimaye iwe na choo nyumbani.”