Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kutokomeza ubaguzi wa kimfumo dhidi ya watu wenye asili ya Afrika zatekelezwa vipande vipande

Waandamanaji washiriki katika maandamano ya Black Lives Matter huko Paris, Ufaransa.
Unsplash/Thomas de Luze
Waandamanaji washiriki katika maandamano ya Black Lives Matter huko Paris, Ufaransa.

Hatua za kutokomeza ubaguzi wa kimfumo dhidi ya watu wenye asili ya Afrika zatekelezwa vipande vipande

Haki za binadamu

Hatua za kutokomeza ubaguzi wa kimfumo dhidi ya watu wenye asili  ya Afrika zinatekelezwa vipande vipande licha ya serikali mbalimbali duniani kutangaza hatua za kumaliza kitendo hicho dhalimu, imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa itakayowasilishwa mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu Jumatatu ijayo.

Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema harakati zinazoongozwa na watu wenye asili ya Afrika, zikiungwa mkono na watu wengine zimeongeza uelewa wa mifumo ya kibaguzi na asili yake na kuchagiza hatua za kutokomeza.

“Lakini bado kuna hitaji la dharura la hatua za kina kuvunja mifumo ya kuendeleza ubaguzi wa rangi iliyoota mizizi katika maeneo mbalimbali ya maisha,” imesema ripoti hiyo.

Ni kwa mantiki hiyo Kaimu Kamishna Mkuu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Nada Al-Nashif ametaka serikali zioneshe Zaidi utashi wa kisiasa na kuongeza hatua hasa kwa kutekeleza mapendekezo ya msingi yaliyotolewa kwenye Ajenda ya OHCHR kuelekea Mabadiliko yenye Marekebisho kwa ajili ya Haki ya watu wenye rangi mbalimbali na Usawa.

Hatua zinachukuliwa lakini si kamilifu

“Kumekuweko baadhi ya hatua katika nchi mbalimbali kushughulikia ubaguzi wa rangi, lakini kwa kiasi kikubwa ni vipande vipande. Hatua hizo hazikidhi hatua za kina zinazohitajika kuvunja mifumo ya kibaguzi ya kitaasisi iliyojikita Pamoja na ubaguzi kwenye jamii,” amesema Bi. Al-Nashif.

Mathalan iripoti inaelezea hatua za kimataifa, kitaifa na kijamii ikiwemo nchini  Marekani ambako kumepitishwa Agizo la Serikali la kusongesha hatua wajibivu, fanisi na za haki kwenye udhibiti wa uhalifu kwenye sheria ya taifa: kupitishwa kwa Sheria dhidi ya takwimu kwa misingi ya rangi ya mtu nchini Canada,: mikakati nchini Sweden ya kutathmini kitendo cha polisi kufuatilia watu kikabila; ukusanyaji wa takwimu za sensa nchini Argentina kunakoruhusu mtu kujitambulisha kuwa na asili ya Afrika.

Bi. Al-Nashif anasema kipimo cha maendeleo kinapaswa kuweko kwa mabadiliko chanya kwa maisha na uzoefu wa watu wenye asili ya Afrika. Hivyo serikali lazima zisikilize watu wenye asili ya Afrika, ziwashirikishe kwa kina na zichukue hatua sahihi kujibu hofu zao.”

Ripoti inaonya kuwa bado watu wenye asili ya Afrika katika mataifa mengi wanakumbwa cha changamoto ya kupata  huduma za afya, chakula cha kutosha, wanakabiliwa na umaskini, hawana hifadhi ya jamii, haki, wanatoweshwa na wanakumbwa na ghasia.

Kesi zinafunguliwa lakini hazina hitimisho

“Kule ambako kuna takwimu, zinaonesha kuendelea kuweko kwa viwango vya juu vya watu wenye asili ya Afrika kuuawa na polisi na familia zinaendelea kukumbwa na vikwazo katika kusaka haki ya kufuatilia vifo vya wapendwa wao.”

Ripot imejikita katika matukio 7 ya vifo vya waafrika kwenye mikono ya polisi,: George Floyd na Breonna Taylor nchini Marekani;  Adama Traoré nchini Ufaransa; Luana Barbosa dos Reis Santos na João Pedro Matos Pinto nchini Brazil; Kevin Clarke nchini Uingereza; na Janner (Hanner) García Palomino wa Colombia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ingawa kumekuweko na maendeleo kwenye uwajibishaji wa kesi hizo lakini, “kwa bahati mbaya hakuna kesi hata moja ambayo imekamilika, huku familia zikiendelea kusaka haki, ukweli na hakikisho la kwamba vitendo hivyo havitarejelewa tena na wahusika washtakiwe.”

Bi. Al-Nashif ametoa wito kwa serikali kuongeza juhudi zao maradufu ili kuhakikisha kuna uwajibika na kutatua mazingira yahusianayo na kifo cha mtu mwenye asili ya Afrika kwenye mifumo ya usimamizi wa sheria na vile vile zichukue hatua kukabili fikra zinazochochea na kuendelea ubaguzi wa kimfumo.