Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban wakimbizi 6,000 wa DRC warejea nyumbani kutoka Zambia kwa msaada wa UNHCR

Mkimbizi kutoka DR Congo akijiandaa kurejea nyumbani kutoka makazi ya wakimbizi ya Mantapala nchini Zambia
© UNHCR/Bruce Mulenga
Mkimbizi kutoka DR Congo akijiandaa kurejea nyumbani kutoka makazi ya wakimbizi ya Mantapala nchini Zambia

Takriban wakimbizi 6,000 wa DRC warejea nyumbani kutoka Zambia kwa msaada wa UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, likishirikiana na serikali za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamewasaidia karibu wakimbizi 6,000 wa DRC kurejea nyumbani kwa hiyari tangu Desemba mwaka 2021. 

Wakimbizi hao walikimbia mapigano ya kisiasa na kikabila katika eneo la Kusini Mashariki mwa DRC mwaka 2017 na kupata hifadhi ya usalama nchini Zambia. 

Kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR iliyotolewa na msemaji wake Boris Cheshirkov mjini Geneva Uswisi hii leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari , wakimbizi hao wameelezea shauku na kufurahi ya kurejea nyumbani na wanatarajia kuungana tena na familia na marafiki na kuanza maisha yao upya. 

Ni chaguo la hiyari 

Shirika hilo la wakimbizi limesema wakimbizi hao wamepewa nyaraka za kurudi nyumbani kwa hiyari na wamepatiwa huduma za haraka za uhamiaji, vipimo vya afya, ulinzi, chakula na maji kabla ya kuondoka. 

Taarifa inasema miongoni mwa wakimbizi hao watoto ni asilimia karibu 60. 

Kwa watoto waliozaliwa nchini Zambia UNHCR imesema walipewa vyeti vya kuzaliwa kama uthibitisho wa utambulisho wao.  

Wizara ya elimu imetoa hati za uhamisho kwa watoto wa shule, na kuwawezesha kuendelea na masomo nchini DRC. 

Wale wenye mahitaji maalum wanasaidiwa na walezi kutoka wizara ya maendeleo ya jamii na huduma za jamii ya Zambia, ili kuhakikisha wanasafiri kwa usalama na kiutu. 

Naomi mwenye umri wa miaka 22, ni mkimbizi kutoka DRC anaishi kambini Mantapala nchini Zambia pamoja na watoto wake na mama yake mzazi.
WFP/Andy Wiggins
Naomi mwenye umri wa miaka 22, ni mkimbizi kutoka DRC anaishi kambini Mantapala nchini Zambia pamoja na watoto wake na mama yake mzazi.

Urejeshwaji wa hiari wa wakimbizi kutoka makazi ya Mantapala katika jimbo la Luapula Zambia hadi Pweto katika jimbo la Haut-Katanga nchini DRC ulianza Desemba 2021.  

Wakimbizi hao wamekuwa wakisafirishwa kwa mabasi katika misafara ya kila wiki ya takriban watu 600 hadi kituo cha mpakani cha Lunkinda.  

Wakati baadhi ya maeneo ya nchi yanasalia kuwa na ukosefu wa usalama, mikoa mingine kama Haut-Katanga imekuwa imara na tulivu na hivyo kuruhusu wakimbizi kurudi nyumbani. 

Wakimbizi zaidi kujerea nyumbani 

Zaidi ya wakimbizi 11,000 wa Kongo wamesajiliwa kurejea DRC ifikapo mwisho wa 2022 kufuatia tamko la kuimarishwa kwa usalama katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Haut-Katanga. 

Katika kituo cha usafiri cha UNHCR huko Pweto (DRC), ambapo waliorejea wanapatiwa malazi kwa siku mbili, mamlaka ya Congo inatoa nyaraka ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wachanga na vyeti vya shule ili kuwaruhusu kuunganishwa haraka na kupata huduma.  

Mshirika wa afya wa UNHCR pia anawafanyia uchunguzi wa matibabu na wagonjwa wenye mahitaji maalum wanapokea matibabu ya msingi. 

Wanaorejea pia hupokea usaidizi wa pesa taslimu ili kusaidia kulipia gharama za msingi wanapofika nyumbani.  

Na fedha hizi zinashughulikia usafiri hadi wanakoenda, usafi na vifaa vya nyumbani, na usaidizi wa awali wa kukodisha nyumba.  

Kulingana na ukubwa wa familia, wanapatiwa mgao wa mwezi wa chakula kama kunde, unga wa mahindi, mafuta na chumvi. 

Pia usaidizi mwingine wa ujumuishwaji katika jamii kama kuwasaidia Watoto kuandikishwa shule unatolewa. 

UNHCR kuendelea kushirikiana na wadau 

UNHCR imesema itaendelea kushirikiana na serikali ya DRC na mamlaka za kitamaduni, ambao ni washirika muhimu katika kuunganishwa tena kwenye jamii kwa wakimbizi hao makwao, hasa kwa uandikishaji wa watoto shuleni, usalama, upatikanaji wa ajira na utoaji wa nyaraka muhimu za kiraia. 

Urejeshwaji makwao kwa hiari wa wakimbizi wa Congo unafanywa kwa msingi wa makubaliano ya pande tatu yaliyotiwa saini mwaka 2006 na UNHCR, serikali za Zambia na DRC. 

Zaidi ya Wacongo 18,000 wameishi katika makazi ya Mantapala ambapo walipata ujuzi wa kujikimu ikiwa ni pamoja na kilimo, ufundi useremala na mafunzo ya ufundi mwingine. 

Kulingana na zoezi la uhakiki wa nchi nzima, Zambia inahifadhi wakimbizi 95,677, wanaotafuta hifadhi na wakimbizi wa zamani.  Hawa ni pamoja na wakimbizi 60,236 kutoka DRC.  

Takriban watu milioni moja za raia ya Congo bado wanahifadhiwa katika nchi jirani. 

Mahitaji ya kifedha ya UNHCR kwa Zambia mwaka huu ni dola milioni 24.4 na dola milioni 225.4 kwa DRC.  

Kufikia Septemba 20, hata hivyo, mahitaji hayo yamefadhiliwa kwa asilimia 23 tu kwa Zambia na asilimia 35 kwa DRC.