Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa DRC walioko Zambia waamua kurejea nyumbani kwa hiari

Mkimbizi kutoka DR Congo akijiandaa kurejea nyumbani kutoka makazi ya wakimbizi ya Mantapala nchini Zambia
© UNHCR/Bruce Mulenga
Mkimbizi kutoka DR Congo akijiandaa kurejea nyumbani kutoka makazi ya wakimbizi ya Mantapala nchini Zambia

Wakimbizi wa DRC walioko Zambia waamua kurejea nyumbani kwa hiari

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani wakimbizi 5,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao walikimbilia nchi jiraniya Zambia miaka minne iliyopita kutokana na machafuko nchini wao wameamua kwa hiari kurejea nyumbani. 

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR jijni Geneva, Uswisi, Babar Baloch amewaeleza waandishi wa habari hii leo kuwa awamu ya kwanza ya wakimbizi 100 inaanza kuondoka leo Jumanne huku wengine katika siku zijazo.

Wakimbizi hao wanasafiri kutoka  makazi ya wakimbizi ya Mantapala jimboni Luapula nchini Zambia kuelelea mji wa Pweto jimbo la Haut-Katanga nchini DRC kufuatia hali ya usalama kuimarika na wanasafiri katika mazingira salama na ya kiutu.

Mwezi Oktoba mwaka huu, UNHCR ilifanya utafiti miongoni mwa wakimbizi kuhusu kurejea nyumbani ambapo 4,774 walisema wako tayari kurejea kwa hiari kupitia makubaliano ya utatu  yam waka 2006 ya kurejesha nyumbani wakimbizi kwa hiari baina ya UNHCR, serikali za Zambia na DRC.

Tayari wakimbizi wengine 20,000 walisharejea jimboni Haut-Katanga tangu mwaka 2018 kutoakana na  hali ya usalama kuimaika.

Bwana Baloch amesema UNHCR inashirikiana na mamlaka za DRC na wadau wa maendeleo kama vile CARITAS kusongesha miradi ya kufanikisha wakimbizi kutangamana vyema kwenye jamii zao, miradi kama vile ya kilimo, elimu na afya.

Takribani wakimbizi 18,000 kutoka DRC wanaishi sambamba na wazambia wakitegemea shughuli za kilimo kwenye makazi ya Mantapala huko Zambia, makazi yaliyoanzishwa mwaka 2018 kuhifadhi wakimbizi hao waliokimbia mapigano ya kikabila na mapigano kati ya vikosi vya usalama DRC na waasi kusini mashariki mwa DRC mwaka 2017.
Usafiri wa wakimbizi na virago vyao umetolewa na UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP na wakifika DRC watapatiwa kiasi cha fedha kuanza upya maisha yao.

Katika kituo cha mapokezi wilayani Chiengi, UNICEF imeandaa malazi kwa wakimbizi wanaorejea wakisubiri mchakato wa uhamiaji kabla ya kufika nyumbani huku huduma za kupima virusi vya Corona au COVID-19 nazo zikilitolewa na kwenye makazi ya Mantapala kabla ya kuanza safari.

Zambia inahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi 103,028 ambapo kati yao hao 63,681 wanatoka DRC.