Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marais wa EAC wana nia ya kutatua changamoto za DRC - Dkt. Mathuki

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki akihojiwa na Leah Mushi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
UN NEWS/ Anold Kayanda
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki akihojiwa na Leah Mushi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa

Marais wa EAC wana nia ya kutatua changamoto za DRC - Dkt. Mathuki

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki amesema wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha Amani inapatikana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC kwakuwa nchi huyo ni mwanachama kamili wa jumuiya hiyo hivyo anastahili kusaidiwa kwenye masuala ya usalama.

Katika Mahojiano aliyofanya na Leah Mushi akiwa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani anapohudhuria mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 Dkt Mathuki amesema pamoja na kupokea ombi kutoka Serikali ya DRC ya kupeleka majeshi Mashariki mwa nchi hiyo lakini hilo litafanyika pale tu iwapo mazungumzo yatashindikana.

Dkt Mathuki amesema “Wakati nilipotembelea kinshasa ilikuwa miongoni mwa majukumu yangu ni pamoja na kusaini mkataba wa SOFA baina ya DRC na jumiya ya Afrika Mashariki, mkataba huu unaruhusu majeshi ya nchi wanachama kwenda DRC kwa ajili ya kuwasaidia kuhakikisha wana amani na kuondoa shida ambazo zipo nchini humo.”

Mkataba huu wa SOFA unaeleza wajibu na majukumu ya jeshi la kikanda wakiwa katika eneo la DRC na uwezeshaji na usaidizi utakaotolewa na Serikali ya nchi mwanachama kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazotumika katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo ameeleza kuwa pamoja na kusaini mkataba huo lakini walikubaliana kuwa na njia mbili za kumaliza mzozo wa Mashariki mwa DRC

“La kwanza na muhimu zaidi ni la kidiplomasia na kisiasa, na hii inamaanisha tunakaa chini na kufanya mazungumzo kwa pamoja kuona hali ipoje, nini kifanyike, na kuelewesha shida gani hasa ipo na jinsi ya kuiondoa changamoyto zinazowakabili wananchi walioko DRC.”

Anasema Kikao cha Baraza la Marais wa Afrika Mashariki kilipokaa kilimteua Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta na kumpa jukumu la kuwa mwezeshaji na kusikiliza pande zote wananchi wale wanao onekana kama ni waasi na wengine na kuwaleta pamoja na kuona namna ya kumaliza mzozo nchini DRC.

“Suala la pili la kutumia jeshi ni wakati ambapo suala la usuluhishi kwa njia ya amani limeshindikana kabisa na diplomasia imeonekana haiwezekani na hapo ndipo serikali zitaketi nakuona jinsi ya kumaliza changamoto.”

Akizungumza jijini New York Marekani Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Felix Tshisekedi ambaye alikuwa miongoni mwa marais waliozungumza siku ya kwanza ya ufunguzi wa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu katika hotuba yake alizungumzia pamoja na mambo mengine ombi lake kwa Nchi za Afrika Mashariki kupeleka wanajeshi Mashariki mwa nchi hiyo eneo ambalo kwa zaidi ya miaka 20 limekuwa na mzozo.

“Kupelekwa kwa jeshi la Kanda ya Afrika Mashariki, ambacho sheria na Kanuni zake za ushiriki zimesainiwa hivi karibuni tarehe O8 Septemba huko Kinshasa, DRC na serikali ya DRC, na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, kwa upande mmoja, na, kwa upande mwingine  na jeshi la DRC, FARDC na kamanda wa kikosi hicho cha kikanda.”

Biashara itafanyika kukiwa na Amani

Katibu Mkuu huyo wa Afrika Mashariki amesema wanachama wote wanataka kuwe na amani ukanda mzima ili waweze kufanya biashara na wananchi waweze kuingia na kutoka katika nchi hizo kwa amani na usalama.

“Mimi nina furahia kwa sababu viongozi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Marais wako na lengo na nia safi ya kufanya kazi kwa pamoja na kuondoa changamoto zile zilizopo nchini DRC. Na suala hili la amani litawezekana kukiwa na utashi wa kisiasa na nikitazama kwa macho ya ndani naona Marais wote wapo tayari kufanya kazi kwa pamoja na kuona watu wa Mashariki mwa DRC wapo sawa.”

Mchakato wa DRC kuwa wanachama kamili wa EAC

Kikao cha Marais wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Machi 2022 kilipitisha ombi la DRC kujiunga rasmi na Jumuiya hiyo na wakaipa miezi sita ili wakazungumze na wananchi wao kupitia Bunge na seneti ili kupata baraka kabla ya kujiunga rasmi.

Dkt. Mathuki anasema kabla hata ya miezi sita kukamilika DRC ilikamilisha mchakato wote na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika. “ Wiki ya kwanza ya mwezi Julai DRC waliniletea vithibitisho vyote kuwa wameshalipeleka suala hilo bungeni, wa meshalipeka seneti na wakaweka nyaraka zote katika ofisi ya Katibu Mkuu. Na Tarehe 22 mwezi Julai katika kikao cha Baraza la Marais wa jumuiya DRC walihudhuria kama wanachama kamili.”

Katibu Mkuu huyo amesema anajivunia kuona jumuiya ya Afrika Mashariki inazidi kukuwa na sasa ina wanachama nane ambao ni Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC ambaye ndio mwanachama mpya.