Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC sasa ni mwanachama rasmi wa jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais wa DRC Félix Tshisekedi  akihutubia Baraza Kuu kutoka Kinshasa
UN WebTV
Rais wa DRC Félix Tshisekedi akihutubia Baraza Kuu kutoka Kinshasa

DRC sasa ni mwanachama rasmi wa jumuiya ya Afrika Mashariki

Amani na Usalama

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC sasa imejiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa mwanachama wa saba. Rais wa DRC Tshisekedi aliye ziarani Kenya kwa siku mbili ametia rasmi saini mkataba wa uanachama.

Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ndiyo nchi kubwa zaidi kwenye eneo lililo kusini mwa jangwa la sahara Na ya pili barani Afrika. Jumuiya ya Afrika Mashariki iliasisiwa mwaka 1967 , ikasambaratika baada ya miaka kumi na kufufuliwa upya mwaka 2000.

Pindi baada ya hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya Nairobi kukamilika katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dr Peter Mathuki amelezea manufaa ya DRC kuwa mwanachama. "Ukiangalia ukubwa wa Afrika Mashariki sasa ni kubwa kuliko bara ya Ulaya na ukiangalia soko la watu milioni tatu, hiyo ni soko ambayo tunaweza kujivunia. Pili sasa wananchi wanauwezowa kutoka nchi moja hadi nyingine bila kusema hii ni nchi moja hadi nyingine. Kwa sasa tunatumia kitambulisho kusafiri kutoka kwa nchi moja hadi nyingine. DRC wakishakuwa na vitambulisho watakuwa wanasafiri kwa urahisi katika jumuiya na hiyo itaimarisha uwiano na uhusiano mwema zaidi."

Nchi nyingine ambazo zinaunda muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni  Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda, na makao makuu yake yapo Arusha, Tanzania.