Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inarudi nyuma katika juhudi za kutokomeza njaa:FAO/IFAD

 FAO na washirika wake waliwasilisha tani 262 za mbolea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kusaidia uzalishaji wa chakula.
© FAO/Michael Tewelde
FAO na washirika wake waliwasilisha tani 262 za mbolea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kusaidia uzalishaji wa chakula.

Dunia inarudi nyuma katika juhudi za kutokomeza njaa:FAO/IFAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani FAO na mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD leo wameonya kwamba dunia inarudi nyuma badala ya kusonga mbele katika jitihada za kutokomeza njaa na utapiamlo. 

Onyo hilo limetolewa leo mjini Roma Italia kwenye ufunguzi wa kongamano la kimataifa la muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia (2019-2028-UNDFF) linalofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia leo 19 Septemba hadi 22 Septemba. 

Akizungumza kwa njia ya video katika hotuba yake ya ufunguzi mkurugenzi mkuu wa FAO  QU Dongyu amesema  idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa iliongezeka mwaka 2021, na inakabiliwa na hatari ya kuongezeka zaidi hasa miongoni mwa walio hatarini zaidi, ambao karibu asilimia 80 wanaishi vijijini na ni wakulima wadogo wa familia. 

 "Wakulima wa familia wanapaswa kuwa katika kitovu cha juhudi za kubadilisha mifumo ya chakula na kilimo ikiwa tunataka kufanya maendeleo ya kweli katika kutokomeza njaa,".  

Bwanda QU ameongeza kuwa “Kilimo cha familia ndiyo njia kuu ya kilimo katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea na ina jukumu la kuzalisha asilimia 80 ya chakula cha dunia.”  

Pia amebainisha kuwa Pamoja na kwamba wao ndio wazalishaji wa chakula lakini mara nyingi, wakulima hao wa familia wanahaha kulisha familia zao wenyewe. 

Tangu kuzinduliwa kwake miaka mitatu iliyopita, muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia umekuwa ukikuza sera jumuishi na uwekezaji ili kusaidia wakulima wa familia, na FAO imekuwa ikisaidia utekelezaji wa kitaifa wa zana na miongozo ya kimataifa ya kuimarisha kilimo cha familia,  ameongeza bwana. Qu. 

Pia ametanabaisha kuwa FAO inaandaa jukwaa la “Maarifa ya Kilimo kwa Familia” ili kuwezesha kubadilishana uzoefu, uvumbuzi na maarifa maalumu. Aidha, mfumo wa mkakati wa FAO 2022-31 unajumuisha eneo la kipaumbele la kazi linalolenga kusaidia vyema wazalishaji wadogo wa chakula na kutoa matokeo madhubuti. 

Ni fursa ya kuwasaikia wahusika 

Kongamano hilo lililoandaliwa kwa Pamoja na FAO na IFAD mashirika hayo yamesema ni fursa ya kusikia kutoka kwa wadau mbalimbali na kufanya majadiliano ili kubaini sera za kipaumbele na maeneo ya kiufundi ambayo yataunda ajenda ya UNDFF kwa kipindi kijacho cha utekelezaji na kusaidia kwa ufanisi zaidi wakulima wa familia na kilimo cha familia duniani kote. 

Kwa mujibu wa FAO na IFAD malengo makuu ya kongamano hilo la kimataifa ni kutoa muhtasari wa jumla wa mwelekeo wa sera na umuhimu wa kilimo cha familia katika utekelezaji wa SDGs na ajenda ya sasa ya maendeleo ya kimataifa, kuonyesha matokeo yaliyopatikana katika miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji, na kuelekeza upya ajenda ya UNDFF kulingana na changamoto za mifumo ya sasa ya chakula na kilimo kwa kubadilishana uzoefu na mafunzo waliyojifunza kutokana na utekelezaji wake mashinani. 

Washiriki  wa kongamano hilo ni pamoja na wawakilishi wa serikali, mashirika ya serikali, wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wakulima wa familia na mashirika yao, mashirika ya kiraia katika ngazi ya kimataifa, kikanda na kitaifa, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs, sekta binafsi, vyombo vya habari na wanazuoni.