Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya sasa inapitia janga kubwa: Tuirekebishe kwa mustakabali wa watoto

Sidonie, mwenye umri wa miaka 10, akiwa mbele ya darasa la shule yake ya msingi Kitambo iliyoko mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kinshasa.
© UNICEF/Josue Mulala
Sidonie, mwenye umri wa miaka 10, akiwa mbele ya darasa la shule yake ya msingi Kitambo iliyoko mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kinshasa.

Elimu ya sasa inapitia janga kubwa: Tuirekebishe kwa mustakabali wa watoto

Utamaduni na Elimu

Ingawa msemo wa haki ya binadamu umezoelekea, hakuna haki ya binadamu yoyote ambayo imetolewa bure bila kupiganiwa, vivyo hivyo inapaswa kuwa kwa elimu, amesema Leonardo Garnier, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkutano wa Ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu duniani, mkutano unaoanza Ijumaa hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Kufahamu msingi wa kauli hiyo, 

Mkutano huo wa ngazi ya juu unafanyika kwa siku tatu ambapo Bwana Garnier akiwa ni mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu mkutano huo anasema ni dhahiri shairi elimu inapitia janga mahsusi na gumu.

Elimu yenyewe hata wanaoipata bado hawajifunzi kinachofaa

Akihojiwa na UN News jijini New York, Marekani kuelekea mkutano huo, ametaja changamoto zinazokumba mfumo wa elimu hivi sasa.

Changamoto kwanza ni kuipata. Mamilioni ya watoto hawako shuleni.

Na hata kwa wale walioko shuleni, changamoto ni kile wanachojifunza na wanajifunza vipi.

Anasema wengi walio shuleni hawajifunzi hata yale mambo ya msingi. Na hata wakijifunza, je wanachojifunza kinafaa? Je wanajifunza wanachohitaji kujifunza kwa dunia ya sasa inayobadilika, halikadhalika uchumi tunamoishi.”

Sharon Dipio (si jina lake halisi) akirejelea masomo nyumbani kwao wilaya ya Adjumani nchini Uganda. Sharon ni mmoja wa wanufaika wa vilabu vya Elimu kwa Wasichana vinavyofadhiliwa na mfuko wa David Beckham.
© UNICEF/Maria Wamala
Sharon Dipio (si jina lake halisi) akirejelea masomo nyumbani kwao wilaya ya Adjumani nchini Uganda. Sharon ni mmoja wa wanufaika wa vilabu vya Elimu kwa Wasichana vinavyofadhiliwa na mfuko wa David Beckham.

Amesema maswali hayo ndio msingi wa mkutano huo wa ngazi ya juu, maswali ambayo yasipojibiwa kwa kufanyia marekebisho mfumo wa elimu, Dunia itarudia kilichotokea miaka ya themanini, ikiwemo kupunguza bajeti za elimu na watoto wengi kutokuwa shuleni.

Katika mazingira kama hayo, watoto “watapoteza kwa ajira ambayo wanaweza kufanya, lakini pia aina ya wakazi wa dunia ambao watakuwa katika dunia ya sasa. Hawatakuwa tayari kuishi pamoja kwenye dunia yenye changamoto nyingi, kukwepa mizozo na kukabili changamoto kama hizi za sasa za tabianchi.”

Elimu ni haki ya msingi lakini ni nadra sana kupatikana bila kupiganiwa

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Garnier anasema kinachotakiwa ni elimu inayowezesha watoto kukabiliana na changamoto hizo.

“Tunataka elimu ya kukabili hayo kwa sababu tunapenda kusema ujumuishaji ni haki ya binadamu lakini tukumbuke hakuna haki ya binadamu imepatikana kwa neema tu.”

Bwana Garnier amesema wale wanaoenguliwa katika elimu watapigania haki yao, kwa hiyo viongozi wa kisiasa lazima wasikilize na wachukue hatua.