Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani nusu ya watu wenye njaa duniani ni watoto

Watoto wakipata mlo wa mchana shuleni nchini Burundi.
WFP/Hugh Rutherford
Watoto wakipata mlo wa mchana shuleni nchini Burundi.

Takribani nusu ya watu wenye njaa duniani ni watoto

Utamaduni na Elimu

Watoto wenye umri wa kwenda shuleni ndio wanaathirika zaidi na janga la sasa la ukosefu wa chakula duniani, hali inaleta madhara makubwa kwenye elimu yao na uwezo wao wa kufidia muda wa masomo waliopoteza wakati wa janga la COVID-19 lililosababishwa kufungwa kwa shule.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Roma, Italia na wadau wa elimu duniani likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, Ubia mpya wa maendeleo barani Afrika- NEPAD, na mashirika mengine yanayohusika na elimu, ikiwemo Kamisheni ya Elimu duniani, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu.

Hali iko vipi?

WFP inakadiria kuwa tangu mwanzo wa mwaka huu janga la chakula duniani limetumbukiza watoto wengine milioni 23 wenye umri wa chini ya miaka 18 katika hali ya ukosefu mkubwa wa chakula. Nyongeza hiyo inafanya watoto wasio na chakula duniani kufikia milioni 153, hii ni saw ana nusu ya watu wote milioni 345 wenye uhaba mkubwa wa chakula duniani. Takwimu hizo ni kutoka mataifa 82.

Maandalizi ya mlo wa mchana kwa wanafunzi 307 katika shule ya Dame Marie kusini-magharibi mwa Haiti
UN Haiti/Daniel Dickinson
Maandalizi ya mlo wa mchana kwa wanafunzi 307 katika shule ya Dame Marie kusini-magharibi mwa Haiti

Madhara ya baadaye

Taarifa hiyo inasema kama hali iko hivyo, mustakabali wa mamilioni ya watoto wenye umri wa kwenda shule uko mashakani, watoto ambao ndio kwanza wamerejea shuleni baada ya janga la COVID-19 kusababisha shule kufungwa.

Benki ya Dunia inakadiria kuwa idadi ya watoto wenye umri wa miaka 10 katika nchi zinazoendelea ambao hawajui kusoma na kuandika imeongezeka kutoka asilimia 53 hadi asilimia 75.

Gordon Brown anasema “kama ambavyo kila mzazi na mwalimu anatambua kuwa njaa ni kikwazo kikubwa cha kujifunza kwa ufanisi, na ongezeko la njaa miongoni mwa watoto wanaokwenda shule ni tishio halisi katika kujikwamua kielimu. Kwa watoto wanaokwenda shule wakiwa na njaa, tayari kuna jawabu tena la gharama nafuu, mlo shuleni, hebu tulitumie."

Mlo shuleni ni jawabu rahisi na fanisi

Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifai, UNGA77  ukianza, wadau wa elimu wanataka kutumia fursa hiyo kupigia chepuo miradi ya milo shuleni ambayo ilivurugwa wakati wa janga la COVID-19. Makadirio yanaonesha kuwa kila mwaka dola bilioni 5.8 zitahitajika ili kufikishia watoto milo shuleni.

Taarifa hiyo inasema mpango huo utakuwa suluhu kwa changamoto nyingi za watoto kuwa na njaa, ikiwemo kupatia majibu miradi ya huduma za afya ya mama na mtoto, kusaidia watoto wasio shuleni na kuongeze uwekezaji wa hifadhi ya jamii.

Carmen Burbano, Afisa wa WFP kuhusu miradi ya milo shuleni amesema, “mamilioni ya watoto wanaishi na madhara ya majanga ya kukosa chakula na kujifunza. Na wakati huo huo, uhusiano kati ya njaa na fursa zinazopotea za kujifunza unahitajika kupatiwa kipaumbele kwenye ajenda za kimataifa, program za mlo shuleni zinaweza kuondoa uhusiano huo.”

Watoto nchini Haiti wamepanga mstari kupata mlo wa bure unaotolewa na WFP
UN Haiti/Daniel Dickinson
Watoto nchini Haiti wamepanga mstari kupata mlo wa bure unaotolewa na WFP

Amesema kutowekeza kwenye program za mlo shuleni “pengine ni moja ya uamuzi mbaya zaidi ambao serikali na wahisani wanaweza kufanya sasa.”

Rwanda na Benin zinachukua hatua

Nchini Rwanda, program ya mlo shuleni imeleta manufaa ambapo kwa sasa chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame, mradi wa kitaifa wa mlo shuleni umeongezeka kutoka kufikia watoto 660,000 hadi watoto milioni 3.8 katika kipindi cha miaka miwili.

Nchini Benin, Rais Patrice Talon ameahidi kuongeza bajeti yam lo shuleni kutoka dola milioni 79 hadi dola milioni 240 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.