Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na IOM wapazia sauti kuepusha baa la njaa Somalia

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, (mwenye skafu ya buluu) akizungumza na wanawake wa Somalia wakati wa ziara yake ya siku  nne nchini humo.
IOM
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, (mwenye skafu ya buluu) akizungumza na wanawake wa Somalia wakati wa ziara yake ya siku nne nchini humo.

UNICEF na IOM wapazia sauti kuepusha baa la njaa Somalia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Somalia linahitaji fedha zaidi ili kufanikisha matibabu ya watoto waliokumbwa na utapiamlo uliokithiri, wakati huu ambapo watoto wengine wameripotiwa kufariki dunia na vituo vya matibabu ya watoto vimefurika, wengine wakipatiwa matibabu wakiwa kwenye sakafu.

Msemaji wa UNICEF James Elder amewaeleza waandishi wa habari Geneva, Uswisi hii leo kuwa idadi ya watoto Somalia wa umri wa kati ya miezi 6 hadi 59 wanaotarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali imeongezeka kutoka 386,000 mwaka 2011 hadi 513,550  mwaka huu huku ombi la fedha za kufanikisha operesheni za shirika hilo Pembe ya Afrika ikiwemo matibabu na mnepo kwa jamii ziweze kuhudumia watoto wao bado limefadhiliwa kwa asilimia tatu pekee.

Bwana Elder amesema ongezeko hilo la watoto wanaougua utapiamlo uliokithiri linamaanisha kuwa watoto wengine 127,000 wako hatarini kufariki dunia iwapo hawatopata matibabu.

Nchini Somalia, UNICEF inapatia watoto wenye utapiamlo huduma za virutubisho ili kuboresha afya zao.
UNICEF/Ismail Taxta
Nchini Somalia, UNICEF inapatia watoto wenye utapiamlo huduma za virutubisho ili kuboresha afya zao.

Kuhara na surua vyatishia uhai wa watoto Somalia

“Watoto wenye utapiamlo uliokithiri wako hatarini mara 11 zaidi kufariki dunia kutokana na kuhara na surua kuliko watoto wenye lishe bora, magonjwa ambayo amesema yanaongezeka kwa kasi kubwa kwenye  ukanda huo ambao uko hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu, milipuko ya magonjwa imeongezeka kukishukiwa wagonjwa 8,400 wa kuhara kupindukia na wagonjwa shukiwa 13,000 wa surua.

Bwana Elder amesema magonjwa yote hayo yana kinga lakini kile wanachoshuhudia kwa watoto ni kiza kinene ambacho hawajawahi kuona katika karne ya sasa.

“Tunataka mabadiliko makubwa ili baa la njaa lisitokee tena, wahisani watoe ahadi za muda mrefu kusaidia faimilia zilizoathirika ili ziweze kujijenga mnepo dhidi ya janga la tabianchi,” amesema afisa huyo wa UNICEF.

Wasomali wanaathiriwa na janga ambalo hawajasababisha- IOM

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM limesema Naibu Mkurugenzi wake Mkuu Amy Pope amemaliza ziara ya siku nne nchini humo na kujionea hali halisi ya wananchi wakihaha kujikimu na maisha kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ambayo wao hawajasababisha. 

Mtoto akichota maji kwenye chanzo ambacho kinamaji kidogo kutokana na ukame uliokausha maziwa huko Dollow Somalia
© UNICEF/Sebastian Rich
Mtoto akichota maji kwenye chanzo ambacho kinamaji kidogo kutokana na ukame uliokausha maziwa huko Dollow Somalia

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Mogadishu, mji mkuu wa Somalia imemnukuu Bi.Pope akisema kuwa, muda unakwenda kasi kwa Somalia na kwamba bila msaada wa haraka baa la njaa litakuwa dhahiri katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo mwezi ujao wa Oktoba.

Kwa mujibu wa Bi. Pope, “hali ya Somalia inahitaji hatua ya dharura kutoka jamii nzima ya kimataifa, mshikamano na usaidizi. Jamii nilizokutana nazo zimeathiriwa vibaya na mabadiliko ya tabianchi. Mamilioni hawana chakula na maji ya kutosha. Mamia ya maelfu ya wasomali wanaweza kufariki dunia.”

Mwaka 2011 baa la njaa lilitangazwa Somalia na watu 250,00  walikufa. IOM inasema hali ya sasa ya ukame tayari imesababisha vifo vya watoto 730, lakini takwimu halisi inaweza kuwa ya juu, kwa kuwa watu milioni 7.8 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.