Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya ukame Somalia yazidi kufurusha wananchi, UNHCR yasihi msaada zaidi

Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia

Hali ya ukame Somalia yazidi kufurusha wananchi, UNHCR yasihi msaada zaidi

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR, linaimarisha usaidizi wake kwa maelfu ya wananchi wa Somalia waliokimbia makazi yao kutokana na ukame mkali uliokumba taifa hilo kufuatia kukosekana kwa mvua kwa vipindi vitatu mfululizo.

Mifugo inakufa, halikadhalika mazao yananyauka, imesema UNHCR kupitia msemaji wake mjini Geneva, Uswisi, Boris Cheshirkov akiongeza kuwa, “mbinu za watu kukabiliana na hali hiyo ya ukame zimefikia ukomo, na maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao ili kusaka msaada wa chakula, malazi na maji safi na salama.”

Wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Machi pekee, zaidi ya watu 17,000 katika ukanda wa kusini wa Bay nchini Somalia wamekimbia makazi yao kutokana na ukame, na hivyo kuungana na wengine makumi ya maelfu waliokimbia makazi yao nchini kote Somalia kati ya mwezi Januari na Februari mwaka huu.

“Iwapo mwenendo wa sasa utaendleea, wasomalia 500,000 watakuwa wamekimbia makazi yao kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Machi,” amesema Bwana Cheshirkov.

Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani Somalia

Waathirika ni watoto, wazee na wajawazito

Wengi wao hao ni watoto, wazee, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha watoto. Familia zinawasili maeneo ya mijini au kwenye makazi ya muda yaliyoko kwa ajili ya wakimbizi wa ndani, ambako mazingira ni duni na hakuna rasilimali za kutosha kuwezesha kukidhi mahitaji ya wanaowasili hivi sasa.

UNHCR inasema watoto wengi wameacha shule kusaidia familia zao kujipatia kipato cha siku au wanakwenda kusaka maji na malisho ya mifugo.

Familia zinatenganishwa na kuna hatari ya watoto kuozwa katika umri mdogo, ukatili wa kingono na manyanyaso.

Kile kinachofanyika sasa

UNHCR inasema hivi sasa inashirikiana na wadau wa masuala ya kibinadamu kufikisha misaada inayohitajika ambapo hadi sasa mahema, vifaa vya kujisafi na vingine muhimu vimewasilishwa kwa watu 36,000 walioathiriwa na ukame na kati yao hao 24,000 wako majimbo ya Galmudug na Puntland ambako hali ni mbaya zaidi.

UNHCR inasisitiza udharura kwa uwekezaji wa haraka ili kujenga mifumo ya kusaidia wale wenye uhitaji zaidi kwa kuwa bila uwekezaji huo “kutakuweko na machungu zaidi, watu kufa na ongezeko la ukimbizi wa ndani.”

Mwaka huu wa 2022, UNHCR imesema inahitaji dola milioni 157.5 ili kuwasilisha misaada ya muhimu zaidi na ulinzi kwa watu milioni 2.9 walio wakimbizi wa ndani Somalia, wakimbizi 40,000 wanaorejea na wakimbizi wapya 15,000 waliowasili kutoka Ethiopia na mataifa mengine.

Hata hivyo tangu tarehe 1 mwezi huu wa Machi ni asilimia 5 tu ya ombi hilo ndio limetolewa.