Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2021 watoto takribani milioni 10.4 watakabiliwa na utapiamlo uliokithiri-UNICEF  

Mtoto mwenye umri wa miezi saba, huko Yemen, akipimwa mzingo wa mkono ili  kuangalia utapiamlo. Mzozo unaoendelea umesababisha ukosefu mkubwa wa chakula kote nchini, na kuacha maelfu ya watoto wakiwa na utapiamlo uliokithiri..
UNICEF/Motaz Fuad
Mtoto mwenye umri wa miezi saba, huko Yemen, akipimwa mzingo wa mkono ili kuangalia utapiamlo. Mzozo unaoendelea umesababisha ukosefu mkubwa wa chakula kote nchini, na kuacha maelfu ya watoto wakiwa na utapiamlo uliokithiri..

Mwaka 2021 watoto takribani milioni 10.4 watakabiliwa na utapiamlo uliokithiri-UNICEF  

Afya

Wakati mwaka 2021 unakaribia, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, lina wasiwasi kuhusu afya na ustawi wa watoto milioni 10.4 wanaokadiriwa kuugua utapiamlo uliokithiri mwaka ujao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, kaskazini mashariki mwa Nigeria, Sahel ya Kati, Sudan Kusini na Yemen. Hizi ni nchi au kanda ambazo zinakabiliwa na majanga mabaya ya kibinadamu wakati pia zikikabiliwa na ongezeko la ukosefu wa chakula, janga hatari la corona. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietha Fore anasema, "kwa nchi zinazohangaika na matokeo ya mizozo, majanga na mabadiliko ya tabianchi, COVID-19 imegeuza shida ya lishe kuwa janga linalokaribia. Familia ambazo tayari ziko katika hali ya kuhangaika kulisha watoto wao na wao wenyewe sasa wako kwenye ukingo wa njaa. Hatuwezi kuwaacha wahanga waliosahaulika wa mwaka 2020." 

Taarifa hiyo ya UNICEF ikieleza kuhusu nchi moja moja, imesema , katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, watoto wanaokadiriwa kuwa milioni 3.3 chini ya miaka mitano watakabiliwa na utapiamlo uliokithiri mwaka ujao wa 2021, ikijumuisha na takribani watoto  milioni 1 wenye utapiamlo mkali uliokithiri. Takwimu hizi za kutisha zinatokana na ukosefu wa usalama unaoendelea, matokeo ya kijamii na kiuchumi ya janga la COVID-19, na ufikiaji mdogo wa huduma muhimu kwa watoto na familia zilizo katika mazingira magumu. 

Kaskazini mashariki mwa Nigeria, zaidi ya watoto 800,000 wanatarajiwa kuugua utapiamlo uliokithiri pamoja na karibia watoto 300,000 wenye  utapiamlo mkali uliokithiri ambao wako karibu na hatari ya kifo. 

Katika kaskazini magharibi mwa Nigeria, hali ya lishe ni mbaya zaidi. Jimbo la Kebbi linakabiliwa na kiwango cha utapiamlo sugu cha asilimia 66, zaidi ya asilimia 20 juu kuliko Jimbo la Borno kaskazini mashariki. Katika Jimbo la Sokoto, pia kaskazini magharibi mwa Nigeria, karibu asilimia 18 ya watoto wanakabiliwa na udumavu na asilimia 6.5 wanakabiliwa na udumavu uliokithiri. 

Nchini Sudan Kusini, utafiti kuhusu uhakika wa chakula uliotolewa mapema mwezi huu ulionesha kuzorota zaidi kwa uhakika wa chakula, na karibu watu milioni 7.3 sawa na asilimia 60 ya idadi ya watu  wote, wanatarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mnamo mwaka 2021. Inakadiriwa kuwa watoto milioni 1.4 nchini humo wanatarajiwa kuugua utapiamlo mkali mwaka ujao wa 2021, idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2013. Wakati huo huo, idadi ya watoto wanaougua utapiamlo uliokithiri inatarajiwa kuongezeka kutoka karibu watoto 292,000 mwaka huu hadi zaidi ya watoto 313,000 mnamo 2021. 

Kuongezeka kwa ukosefu wa usalama wa chakula nyumbani na utapiamlo mkali miongoni mwa watoto kunachangiwa na mizozo na ukosefu wa usalama unaoendelea, na ufikiaji mdogo wa lishe muhimu, huduma ya afya na maji, huduma za usafi wa mazingira na kujisafi. Mafuriko katika maeneo mengine katika mwaka huu wa 2020 yameongeza kiwango cha juu cha utapiamlo mkali kati ya watoto. 

Katika nchi za Sahel ya Kati yaani Burkina Faso, Mali na Niger, kuongezeka kwa mizozo, kukosa makazi na majanga ya hali ya hewa yataacha watu wanaokadiriwa kuwa milioni 5.4 wakihangaika kukidhi mahitaji yao ya chakula ya kila siku katika msimu ujao. Ukosefu mkubwa wa chakula umeongezeka kwa asilimia 167 nchini Burkina Faso, asilimia 34 nchini Mali na asilimia 39 nchini Niger, ikilinganishwa na wastani wa miaka mitano. 

Idadi ya watoto wanaougua utapiamlo uliokithiri inaweza kuongezeka kwa asilimia 21 hivi karibuni. Hii italeta idadi kamili ya watoto wenye utapiamlo katika nchi hizo tatu kufikia milioni 2.9, pamoja na watoto 890,000 wanaougua utapiamlo mkali. 

Kote nchini Yemen, zaidi ya watoto milioni 2 chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri, pamoja na karibia watoto 358,000 wenye utapiamlo mkali idadi ambayo inatarajiwa kuongezeka. Katika wilaya 133 kusini mwa Yemen, nyumbani kwa watoto milioni 1.4 chini ya miaka mitano, uchambuzi wa hivi karibuni unaonesha ongezeko la karibu asilimia 10 kwa watoto walio na utapiamlo mkali kati ya Januari na Oktoba 2020. Hii ni pamoja na ongezeko la zaidi ya asilimia 15 karibu watoto 100,000 katika visa vya utapiamlo mkali. Uchambuzi kama huo unakamilishwa kwa kaskazini mwa Yemen na matokeo ya kutisha yanatarajiwa huko pia. 

Katika nchi hizi zote na kwingineko, UNICEF inawahimiza wahusika wa kibinadamu na jamii ya kimataifa kupanua haraka upatikanaji na msaada wa lishe, afya na maji na huduma za usafi wa mazingira kwa watoto na familia.