Mahojiano: Csaba Kőrösi, Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi amesema dunia hivi sasa inakumbwa na machungu na matatizo makubwa kutokana na ukosefu wa imani na kwamba “wakati tunapanga kuhusu kuchungua hatua kusongesha dunia mbele kutoka katika changamoto hizi lukuki, kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi vita ya Ukraine na uhaba wa chakula,” atatumia mamlaka yake kuongoza chombo hicho cha UN ili kusaidia kurejesha imani miongoni mwa mataifa na kuimarisha imani kwa mfumo wa kimataifa.
Akiwa na fikra hizo, Bwana Kőrösi, ambaye ni raia wa Hungary amesema, miongoni mwa hatua atakazochukua ni kuwa na vikao vya kando na wanadiplomasia wa UN ambavyo vitakuwa vya wazi zaidi na visivyo rasmi ili kujadili masuala magumu.
Habari za UN: Kila mwaka mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huanza kwa tukio la Rais wa mkutano unaomalizika kukabidhi rungu la Mwenyekiti kwa RAis wa Mkutano unaoanza. Kiuhalisia, rungu hili lina uzito gani kwako na nini unadhani itakuwa ni maamuzi au hatua muhimu zitakazopitishwa kwa kugonga rungu hili wakati wa mkutano huu wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa?
Kőrösi: Uzito wa rungu hili si wa uhakika sana, licha ya utukufu wa ulikotoka. Hata hivyo uzito ambao rungu hili unabeba kisiasa na kiroho utakuwa mkubwa zaidi kwa sabbau dunia iko kwenye majanga mazito. UN inatathmini hayo majanga. UN imegawanyika hii leo kama ulivyo ulimwenguni wenyewe. Kwa hiyo, kile ambacho tunapaswa kufanya kimsingi ni kutatua baadhi ya masuala makubwa yanayotugawanya. Ina maana, ushughulikiaji wa majanga, na UN inapaswa kusaidia nchi wanachama kuwa na matarajio hayo. Ina maana marekebisho. Maamuzi yote makubwa ambayo yanaweza kupitia lensi za ushughulkiaji wa majanga na marekebisho yatakuja kupitia rungu hili.
Habari za UN: Umedokeza suala la kupata majawabu kupitia ushirikiano endelevu na Sayansi, kama ndio kauli mbiu ya mkutano wa 77 wa Baraza Kuu. Wakati mshikamano na uendelevu ni maneno yaliyozoeleka, na Sayansi ni jambo jipya kwenye kanuni hiyo. Ni vipi umepenga kutambulisha hilo kwenye mipango ya kazi wakati wa mkutano huu wa UNGA77.?
Kőrösi:Iwapo hautajali, ningependa kugusia yote ambayo hatuyafahamu.
Majawabu, kwa sababu tuna mikataba mingi ya kimataifa, makubaliano mengi, malengo mengi na mipango lukuki ya hatua za kuchukua. Lakini tuko dhaifu kwenye utekelezaji na huu ni wakati wa utekelezaji. Ni wakati sio tu wa hatua zaidi, bali pia hatua zaidi za marekebisho.
Mshikamano: Ukosefu wa usawa unaongezeka duniani miongoni mwa wengi na kwa miaka mingi. Ndani ya nchi na baina ya nchi. Na iwapo tutaruhusu ukosefu huu wa usawa uendelee kukua, bila shaka utachochea msuguano zaidi, mvutano zaidi na mizozo na majanga. Lazima tuchukue hatua tutatue. Na jambo muhimu zaidi ni kutimiza ahadi zetu, ahadi zetu ndani ya nchi zetu, na baina ya nchi kupitia uhusiano wa kimataifa. Iwapo tutaangusha jamii zetu, dunia nzima itateseka. Tusisahau kuwa: Tutasimama pamoja au Tutaanguka pamoja.
Uendelevu: Ni kuhusu marekebisho. Ni kuhusu uwajibikaji. Ni kuhusu kuangalia mbele. Je ni aina gani ulimwengu tulio nao leo ? Kesho utakuwa vipi? Aina gan iya dunia tunaachia watoto na wajukuu wetu? Na uwajibikaji uko hapa na sasa. Uendelevu unamaanisha kuwa tunajumuisha maoni katika masuala magumu. Marekebisho yanawezekana pale tu iwapo ujumuishaji wa mambo unafanyika kiuhalisia.
Habari za UN: Ni kwa vipi basi sayansi inaimarisha hizo juhudi?
Kőrösi: Nchi wanachama wanahaha na kuporomoka kwa imani ya umma kwa serikali, mganyiko baina ya nchi, baina ya jamii. Na bila shaka, itakuwa vigumu mno kusaka majawabu ya kiitikadi. Na hilo si jukumu letu. Jukumu letu ni kusaka majawabu yenye Ushahidi, Ushahidi thabiti ambao unaweza kutusaidia kusonga mbele. Sayansi inawea kutupatia Ushahidi wa aina hiyo.
Lakini ni vema sana kuelewa: hatutaki wanasayansi watueleze kile tunapaswa kufanya, la hasha! Tunataka wanasayansi watuoneshe mbadala ulioko na kile ambacho kitatokea kutokana na kuchukua hatua na kutochukua hatua. Sayansi inapaswa kualikwa ili kuleta msaada. Sayansi inapaswa kuwa muunga mkono. Lakini uamuzi wetu wa kisiasa hatma yake ni mikononi mwa nchi wanachama. Na wajibu huo uko mikononi mwa nchi wanachama.
Habari za UN:Kwa hiyo unatarajia kutumia mifano ya mifumo ya UNm mashirika kama lile la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO na wengineo, jamii ya kimataifa au sio?
Kőrösi:Hakika! Tungependa kutumia ufahamu na ushauri kutoka mashirika ya UN ambayo yamekuwa yakifanya kazi kwa kina na ambayo yameshiriki kwa kina kwenye Sayansi. Lakini inaweza isitosheleze wakati huu. Tungependa kujenga na kuwa na mashauriano ya mara kwa mara na taasisi za kisayansi, za kidini na za kibiashara, za kifedha ili zitushauri jinsi ya kushughulikia changamoto kubwa zinazokuja kwenye ajenda za nchi wanachama. Na sio tu ushauri lakini pia kuhakikisha ushauri wao unaweza na lazima ufikia nchi wanachama.
Tungependa pia kuwa na mikutano midogo midogo ya mashauriano wakati wa asubuhi, au wakati wa kahawa na makundi madogo ya nchi wanachama, mabalozi, wanawake katika mazingira yasiyo rasmi. Hii lengo lake ni kuona ni ushauri uliowasilishwa na jamii ya wanasayansi, wafanyabiashara na una maslahi gani kwa nchi wanachama. Huu utakuwa ni mjadala bila wajibu wowote.
Habari za UN: Uliahidi kuwa ofisi yako itasongesha maadili ya tamaduni na lugha tofauti. Ni kwa vipi utatekeleza hilo?
Kőrösi: Kuhusu tamaduni mbalimbali, haya ni maadili ya pamoja, ni urithi wa pamoja kwetu sote. Tunatoka mataifa tofauti yenye tamaduni tofauti, na mila tofauti. Kwa pamoja, kile tunachowakilisha ni urithi wa binadamu wote. Iwapo hata kipande kimoja kitapotea, basi sote tumepotea. Kwa hiyo nitafuatilia katika njia mbalimbali, na katika fursa mbalimbali. Iwe kwenye matukio ya kando, maonesho, au matukio maalum, nitasihi nchi wanachama: leteni tamaduni zenu, shirikisheni nchi nyingine wanachama.
Kuhusu lugha tofauti tofauti, sote tunafahamu kuna lugha sita rasmi kwenye Umoja wa Mataifa. Tunafahamu pia ni kanuni zipi za kutumia hizo lugha. Na tunafahamu ni zoezi la gharama sana. Lakini kwa kadri ninavyofahamu, nitashinikiza matumizi ya lugha hizo sita katika ngazi zote kwa usawa. Na kama inawezekana, hebu na tumulike lugha nyingine duniani kote kwa sababu zinabeba utamaduni, zinabeba urithi wa pamoja wa utamaduni.