Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na Wasichana ndio wahamiaji wengi zaidi katika Mashariki na Pembe ya Afrika - Ripoti ya IOM 

Wanawake wanasubiri msaada wa chakula katika kituo cha usambazaji huko Afgoye, Somalia.
UN Photo/Tobin Jones
Wanawake wanasubiri msaada wa chakula katika kituo cha usambazaji huko Afgoye, Somalia.

Wanawake na Wasichana ndio wahamiaji wengi zaidi katika Mashariki na Pembe ya Afrika - Ripoti ya IOM 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wanawake na wasichana wameelezwa kuwa ndio idadi kubwa ya wahamiaji Mashariki na Pembe ya Afrika wakiwa ni asilimia 50.4 ya wahamiaji wote ikilinganishwa na wanaume na wavulana, ambao ni asilimia 49.6, jambo ambalo ni la kipekee katika ukanda huo kwa mujibu wa takwimu za kikanda zilizotolewa leo na ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM) iliyotolewa leo jijini Nairobi, Kenya.  

Wakati uhamiaji katika maeneo mengine ya bara unawahusisha wanaume zaidi, ripoti yenye jina A Region on the Move 2021, inaonesha wanaume na wavulana wana asilimia 49.6 pekee katika Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika. Ripoti inakwenda mbali zaidi kuonesha karibu asilimia 60 ya idadi ya wahamiaji katika eneo hili ni wakimbizi na wanaotafuta hifadhi. Wanawake ndio wanaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, kwani wana uwezekano mkubwa wa kuhamishwa kwa nguvu, wakati wanaume wana uwezekano mkubwa wa kuhama kawaida kutafuta nafasi za ajira. Kwa ujumla, mmoja kati ya wahamiaji wanne katika bara la Afrika wanaishi katika eneo hilo, inaeleza ripoti hiyo ya IOM iliyotolewa leo jijini Nairobi nchini Kenya. 

IOM inaeleza kuwa mizozo na ukosefu wa usalama vinasalia kuwa vichochezi vikubwa vya watu kuhama katika eneo hilo. Kulikuwa na watu milioni 13.2 waliohamishwa kwa lazima katika eneo hilo mwaka 2021, wakiwemo wakimbizi wa ndani, IDPs, milioni 9.6 na wakimbizi milioni 3.6 na wanaotafuta hifadhi. 

Vilevile ripoti inaeleza kuwa tofauti na ukanda mwingine wowote duniani, nchi kadhaa za Mashariki na Pembe ya Afrika, pamoja na kuwa kivutio kikuu cha wakimbizi na waomba hifadhi wanaokimbia migogoro na kutafuta usalama na kazi, pia ni nchi kuu ambako wakimbizi na waomba hifadhi wanatoka. Sudan Kusini ni mojawapo ya mifano hiyo. Mnamo mwaka wa 2021, nchi hiyo ilikuwa na wakimbizi na watafuta hifadhi 325,000, wakati karibu wakimbizi milioni 2.3 wa Sudan Kusini na wanaotafuta hifadhi walihifadhiwa nje ya nchi. Ukweli huu wa kipekee unaonesha jinsi mtiririko wa wakimbizi unapatikana ndani ya eneo hili. 

Ukame, hasa nchini Somalia, Ethiopia na Kenya, pia imekuwa sababu kuu inayochochea uhamiaji na watu kuhama katika eneo hilo. Nchi hizi zimekuwa zikikumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne na hali hizi za kipekee zinafanana na hali iliyoonekana wakati wa njaa ya mwaka 2010-2011 na dharura ya ukame 2016-2017 katika Pembe ya Afrika. 

Ripoti hiyo pia inafichua kuwa usafirishaji haramu wa watu unatia wasiwasi kwa IOM kubaini visa 3,000 vya usafirishaji haramu wa binadamu kutoka eneo hilo, katika muongo mmoja uliopita. Watu wengi waliosafirishwa walitambuliwa kuwa wanatoka Kenya, Uganda na Ethiopia huku wanawake na wasichana wakiwa walioathirika zaidi kwa asilimia 78, ikilinganishwa na wanaume na wavulana asilimia 22. 

"Tunapoendelea kuelekea kuimarisha msingi wa ushahidi wa utawala bora wa uhamiaji katika ngazi zote na ndani ya mfumo mpana wa Umoja wa Mataifa," anasema Mohammed Abdiker, Mkurugenzi wa IOM wa Kanda ya Mashariki na Pembe ya Afrika, akiongeza kwa kusema, "tunatumai kuwa matokeo ya pamoja ya kuwepo uelewa bora zaidi wa ukubwa wa changamoto tunazokabiliana nazo na dhamira mpya ya kushirikiana katika kukusanya data sahihi na zilizogawanywa, hivi karibuni kutasababisha sera za uhamiaji za hali ya juu na zenye msingi wa ushahidi, ulinzi bora wa haki za wahamiaji na usaidizi bora kwa wale wanaohitaji. " 

A Region on the Move ni mfululizo wa ripoti kuu kwa ukanda wa Mashariki na Pembe ya Afrika ambao unalenga kunasa mienendo ya uhamiaji na kutoa uchanganuzi unaozingatia ushahidi ambao unaboresha uelewa wa IOM wa uhamaji katika eneo hili na kukuza matumizi ya kimfumo ya data ili kuongoza usaidizi na mjadala kwa ngazi ya sera.