Wahamiaji 11,500 husafiri kila mwezi kutoa Pembe ya Afrika kwenda Yemen:IOM

14 Februari 2020

Kwa wastani, watu 11,500 walipanda meli kila mwezi kutoka Pembe la Afrika kwenda Yemen mnamo mwaka 2019, na kuifanya njia ya uhamiaji kupitia baharini kuwa iliyokuwa na pilika nyingi zaidi duniani kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Takwimu zilizokusanywa na mfumo wa IOM wa ufuatiliaji wa uhamiaji (DTM) na kuchapishwa leo zinaonyesha kwamba zaidi ya watu 138,000 walivuka ghuba ya aden na kuingia nchini Yemen mwaka jana huku zaidi ya wahamiaji na wakimbizi 110,000 walivuka bahari ya Mediterrania na kuingia barani Ulaya katika kipindi hichohicho.

Huu ni mwaka wa pili mfululizo IOM inasema kuwa safari za Mashariki zimekuwa nyingi zaidi ya zile za kupitia Mediterrania. Kwa mwaka 2018 watu takriban 150,000 walifanya safari hizo.

IOM inasema “karibu asilimia 90 ya waliowasili Yemen mwaka 2019 walilenga kuendelea na safari hadi kwenye Ufalme wa saudia , na wengi hutokea katika majimbo ya Oromoa, Amhara na Tigray na takribani asilimia 92 ya watu hao ni raia wa Ethiopia.”

Kwa mujibu wa Mohammed Abdiker mkurugenzi wa Pembe ya afrika wa IOM “wakati majanga katika bahari ya Mediterrabnia yaliripotiwa wafanyakazi wa Iom wanashuhudia kila uchao ukatili na madhila yanayowakabili vijana kutoka Pembe ya afrika mikoni mwa wahalifu na wasafirishaji haramu wa binadamu wakitumia fursa ya ndoto na matumaini yao ya kutaka kusaka mustakabali bora.”

Ameongeza kuwa sio tu kwamba vita vinavyoendelea Yemen kwa miaka mitano sasa havijapunguza idadi ya safari hizo bali pia sheria na sera zinazobana wahamiaji  wasio na vibali Ukanda wa Ghuba hazijawaogopesha. Mmoja wa wahamiaji waliopitia safari hizo za hatari amesema “Kufika Yemen wasafirishaji haramu walitujaza wahamiaji 280 kwenye boti moja, hakukuwa na hewa ya Oksijeni na watu wengine waliamua kujiua kwa kujitosa baharini”

IOM inasema wahamiaji hao wengi wao hawajui kuhusu hali ya usalama Yemen ambako wanakabiliwa na hali mbaya ya ulinzi ikiwemo mapigano yanayoendelea au mateso na ukatili ikiwemo utekwaji, mateso kwa ajili ya kulipa kikombozi na usafirishaji haramu wa binadamu.

Hata hivyo IOM inasema njia pekee ya ulinzi kwa wahamiaji hao ni kuanzishwa kwa mfumo wa kisheria wa uhamiaji.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter