Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pakistan: WFP inafanya kazi ya kupanua msaada wa chakula huku mafuriko mabaya yakiendelea

WFP inasambaza chakula kwa jamii zilizoathiriwa na mafuriko ya monsuni huko Balochistan, Pakistan.
© WFP/Balach Jamali
WFP inasambaza chakula kwa jamii zilizoathiriwa na mafuriko ya monsuni huko Balochistan, Pakistan.

Pakistan: WFP inafanya kazi ya kupanua msaada wa chakula huku mafuriko mabaya yakiendelea

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) linaiunga mkono Pakistan wakati nchi hiyo inakabiliana na athari za mafuriko ambayo yameripotiwa kuua zaidi ya watu 1,000 na kusababisha wengine milioni 33 kuwa wakimbizi wa ndani, limesema leo shirika hilo la Umoja wa Mataifa. 

Kupitia mamlaka yake ya kitaifa ya kudhibiti maafa, serikali ya Pakistani ambayo imetangaza dharura ya kitaifa inaongoza hatua za usaidizi katika kuratibu tathmini na kuelekeza misaada ya kibinadamu kwa watu walioathirika. 

Tangu mwezi Juni mwaka huu 2022, mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa ya Monsoon yameleta uharibifu mkubwa kote nchini Pakistan, na kusababisha "changamoto kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa,” kulingana na Julien Harneis, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini humo. 

Mratibu huyo ametoa wito wa "kugawana mizigo na kuonyesha mshikamano" wa kimataifa kutokana na janga hilo la mabadiliko ya tabianchi." 

Kwa mujibu wa duru za habari, theluthi moja ya nchi inaweza kuachwa chini ya maji wakati hali ya hewa ya monsoon inaendelea, na idadi ya vifo huenda ikaongezeka huku mito mingi ikipasua kingo zake, na kusomba barabara na madaraja, huku jamii nyingi za maeneo ya kaskazini mwa milimani zikikatwa na kuachwa bila mawasiliano. 

Mafuriko nchini Pakstan
UN Photo/WFP/Amjad Jamal
Mafuriko nchini Pakstan

Changamoto za kufikia waathirika 

WFP imeombwa kusaidia katika kukabiliana na dharura, na wafanyakazi wake wanashirikiana na mamlaka na wadau wengine kupanua wigo msaada wa chakula. 

Lengo ni kufikia karibu watu nusu milioni katika mikoa iliyoathirika vibaya ya Balochistan, ambapo shirika hilo tayari linasaidia karibu watu 42,000, na mkoa wa Sindh.

Hata hivyo, usambazaji umesitishwa kwa sasa kwani maji ya mafuriko yanaleta vikwazo vya ufikiaji kote nchini. 

Maji pia yametatiza maisha na uwezo wa watu kuishi katika majimbo ya Khyber Pakhtunkhwa na Punjab. 

Zaidi ya madaraja 100 na baadhi ya kilomita 3,000 za barabara zimeharibiwa au kusambaratishwa, karibu mifugo 800,000 wa mashambani wameangamia, na ekari milioni mbili za mazao na bustani zimesambaratishwa.

Mamilioni ya watu sasa wamefurushwa kutoka makwao kutokana na mafuriko nchini Pakistan.
WFP
Mamilioni ya watu sasa wamefurushwa kutoka makwao kutokana na mafuriko nchini Pakistan.

Ombi la ufadhili la UN 

Bwana Harneis ameonya kuwa hali ya kibinadamu inatarajiwa kuwa mbaya zaidi, huku magonjwa na utapiamlo vikitarajiwa kuongezeka pamoja na idadi ya wilaya zinazoripoti kuwa zimeathirika. 

Umoja wa Mataifa unatazamiwa kuzindua ombi la dola milioni 161 kwa Pakistan kesho Jumanne. 

Ufadhili huo utatoa msaada muhimu wa chakula na pesa taslimu kwa karibu watu milioni moja kwenye wilaya zilizoathirika katika majimbo ya Balochistan, Sindh, Punjab na Khyber Pakhtunkhwa. 

Zaidi ya dola milioni 34 zinahitajika haraka ili kuwezesha kuongeza kasi ya shughuli za kusambaza misaada ya kibinadamu.