Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka mitano ya mgogoro wa Rohingya changamoto bado zinaendelea:UN

Katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh watoto wamekusanyika katika kituo cha muda cha kusomea kinachotoa msaada wa kisaikolojia na shughuli za kuburudisha
© UNICEF/Rashad Wajahat Lateef
Katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh watoto wamekusanyika katika kituo cha muda cha kusomea kinachotoa msaada wa kisaikolojia na shughuli za kuburudisha

Miaka mitano ya mgogoro wa Rohingya changamoto bado zinaendelea:UN

Amani na Usalama

Ikiwa ni miaka mitato tangu kuzuka mgogoro wa Rohingya uliowalazimisha zaidi ya watu 700,000 kufungasha virago nchini Myanmar na kuingia Bangladesh, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaha suluhu ya kudumu na jumuishi ili kusaidia kumaliza madhila kwa wakimbizi wa Rohingya.

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini New York Marekani Guterres amesema takriban Warohingya milioni 1 bado wanapata hifadhi nchini Bangladesh bila kuwa na matarajio ya kurejea nyumbani huku wengine zaidi ya 150,000 wengi wakiwa ni Waislam wanaendelea kuishi makambini kwenye jimbo la Rakhine.
Na kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Februari 2021 hali ya kibinadamu, haki za binadamu na hali ya usalama nchini Myanmar kwenyewe imezorota sana na haraka na hivyo kusababisha mazingira kuwa mabaya zaidi kwa wakimbizi kurejea.


Ushiriki ni muhimu

“Katibu Mkuu anabainisha matarajio yasiyopingika ya mustakabali jumuishi kati ya makabila mengi na makundi ya kidini nchini humo na kusisitiza kwamba ushiriki kamili na wenye ufanisi wa watu wa Rohingya ni sehemu ya muhimu ya suluhu ya mgogoro unaoongozwa na Myanmar". Imesema taarifa yake.
Imeongeza kuwa "Ufikiaji mkubwa wa kibinadamu na maendeleo kwa Umoja wa Mataifa na washirika wake kwenye maeneo yaliyoathirika ni muhimu. Wahusika wa uhalifu wote wa kimataifa uliofanywa nchini Myanmar wanapaswa kuwajibika. Haki kwa waathiriwa itachangia mustakabali endelevu na shirikishi wa kisiasa kwa nchi hiyo na watu wake.”

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono vitani, Pramila Patten akiwa Cox Bazar
Picha ya Letitia Anderson
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono vitani, Pramila Patten akiwa Cox Bazar

Ukatili wa kingono ukomeshwe na kuwajibishwa

Kwa upande wake mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo Pramila Patten, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kushikamana na watu wa jamii ya Rohingya na kutaka juhudi ziimarishwe katika masuala ya haki na uwajibishwaji kwa ajili ya manusura wa ukatili wa kingono.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis Bi.Patten amesema mgogoro huo unaingia mwaka wa tano katika wakati ambao dunia inapitia misukosuko mingi iliyosababishwa na vita vya silaha na operesheni za kijeshi ambazo zimesambaratisha maisha, mifumo ya afya, uchumi na jamii. 
Pia amepongeza ukarimu wa serikali ya Bangladesh kwa wakimbizi wa Rohingya.

Kuongezeka kwa mgogoro

Akizungumza mjini Geneva Uswis, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu (OHCHR), Michelle Bachelet, amesema kuwa vikosi vya Tatmadaw vya Myanmar vimedumisha na hata kuzidisha operesheni dhidi ya raia katika maeneo ya makaazi ya Kusini-Mashariki, Kaskazini-Magharibi na Kati, miezi 18 tangu walipopindua utawala uliochaguliwa kidemokrasia.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN Photo/Antoine Tardy
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

Matumizi ya nguvu za anga na makombora dhidi ya vijiji na maeneo ya makazi "yameongezeka", mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, huku pia akionya kwamba ongezeko la ghasia za hivi majuzi huko Rakhine kwenye makavazi ya kihistoria ya zamani ya kabila la Rohingya - linaweza kuvuruga utulivu katika eneo hilo ambalo ni eneo la mwisho la nchi lenye tulivu na kwamba linaweza lisiepuke kuzuka upya kwa vita.
Jamii za Rohingya mara kwa mara zimenaswa kati ya Tatmadaw na wapiganaji waasi wa jeshi la Arakan au wamekuwa wakilengwa moja kwa moja katika operesheni. 
Zaidi ya watu milioni 14 wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Ukarimu wa Bangladesh
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Noeleen Heyzer, akiongeza sauti yake leo amesema wakati wa ujumbe wake wa siku nne nchini Bangladesh kuangazia kumbukumbu hiyo ya kutisha, amesisitiza kwamba "hatuwezi kuruhusu hili kuwa mgogoro uliosahaulika".

Mkimbizi wa kabila la rohingya akiwa jimboni Aceh, Indonesia
© UNHCR/Jiro Ose
Mkimbizi wa kabila la rohingya akiwa jimboni Aceh, Indonesia

Katika kile kilichoelezwa kuwa "mijadala yenye tija, amemshukuru Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina kwa uongozi wake na ameonyesha shukrani za kina za Umoja wa Mataifa kwa watu na Serikali ya Bangladesh kwa mchango wao mkubwa.
"Ukarimu wa Bangladesh na jumuiya zinazowahifadhi wakimbizi wa Rohingya katika wakati wao wa mahitaji unaonyesha hitaji muhimu la kujitolea zaidi kimataifa na kikanda katika kugawana mzigo na kuhakikisha kuwa Warohingya hawasahauliki," Mjumbe Maalum Heyzer amesema.
"Nitaendelea kutetea uongozi bora wa nchi katika kanda katika kuunga mkono Bangladesh na kutumia ushawishi wao na Myanmar ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kurejea kwa hiari, salama na kwa heshima."
Amesisitiza kuwa watu wa Rohingya wanaendelea kufanya safari za hatari za nchi kavu na baharini ambazo zinawaweka kwenye unyanyasaji wa uhalifu ikiwa ni pamoja na biashara haramu ya binadamu na unyanyasaji wa kijinsia, na kusisitiza kwamba hatimaye ni jukumu la Myanmar kuweka mazingira mazuri ya kurudi kwa hiari, salama, heshima na uendelevu Myanmar ka wakimbizi wote na wale waliohamishwa kwa lazima.