Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina miaka 90 na nimekuwa mkimbizi Bangladesh mara tatu: Zahra 

Gul Zahar, ajuza mwenye umri wa miaka 90 akisikiliza Qu'ran kupitia simu ya kiganjani kwenye kambi ya wakimbizi wa kabila la Rohingya nchini Bangladesh.
UNifeed Video
Gul Zahar, ajuza mwenye umri wa miaka 90 akisikiliza Qu'ran kupitia simu ya kiganjani kwenye kambi ya wakimbizi wa kabila la Rohingya nchini Bangladesh.

Nina miaka 90 na nimekuwa mkimbizi Bangladesh mara tatu: Zahra 

Amani na Usalama

Kuwa mkimbizi ni suala moja, kuwa ajuza mkimbizi ni suala lingine lakini kulazimika kuikimbia nchi yako mara tatu kwa sababu ya machafuko ni sawa na kuweka msumari wa moto juu ya kidonda. Hayo ndiyo yaliyomsibu Bi. Zahra Gul mwenye umri wa miaka 90 , mkimbizi wa wa Rohinya kwa mara ya tatu ambaye sasa anaishi kambini Katupalong  nchini Bangladesh..

Hebu tafakari unakuwa ajuza tena wa miaka 90, na tangu ujana wako hadi sasa uzeeni unafungasha virago tu  kukimbia machafuko kisa na mkasa, ambatana na Flora Nducha kwenye makazi ya wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh.

Nje ya kibanda kilichojengwa kwa maplastiki ya shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kambini Katupalong Cox’s Bazar, ameketi ajuza  wa miaka 90 Zahar Gul raia wa Myanmar, muislamu kutoka kabila la Rohingya, anasilikiza Quran kupitia simu ya mkononi.

Hi ni mara ya tatu anaishi ukimbizi katika maisha yake. Kwanza alifungasha virago 1978, kisha 1999 na kwa mara ya tatu Agosti 2017  alilazimika kukimbilia tena Bangladesh baada ya Kijiji chao kuchomwa moto.

Gul Zahar akiwa kambini huko Bangladesh. Simulizi nyingi ni machungu aliyopitia nchini mwake Myanmar.
UNifeed Video
Gul Zahar akiwa kambini huko Bangladesh. Simulizi nyingi ni machungu aliyopitia nchini mwake Myanmar.

“Jeshi la Myanmar lilitutesa hi indio sababu tumekuja hapa, tunatumai kwamba Bangladesh tutaweza kupata amani.”

Zahar anaishi kambini hapa na wakimbizi wengine takriban 6000 kutoka Myanmar na  familia yake akiwemo  mwanaye wa kiume Oli Ahmad mwenye umri wa miaka 43

“Nilikuwa na miaka 18 tulipokimbilia hapa Bangladesh kwa mara ya kwanza. Tuliishi makambini kwa miaka minne, kisha tukarejea Myanmar, sasa miaka 25 baadaye tumerejea tena.”

Hata hivyo Zahar na familia yake hawajaukatia tamaa usemi wa wahenga kwamba “nyumbani ni nyumbani”

Nitarejea tena endapo kutakuwa na amani nchini mwetu, kila kitu changu, nyumba yangu viko huko, nitakufa kwa amani nikiwa huko.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hivi sasa kuna wakimbizi zaidi ya Laki Tisa wa Rohingya walioko Bangladesh na idadi inaongezeka kila uchao.

 

TAGS: Rohingya, Myanmar, wakimbizi, Katupalong, Cox’s Bazar