Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwani watumika kujenga nyumba za bei nafuu nchini Mexico

Mwani wa Sargassum umeharibu baadhi ya fukwe safi zaidi za Mexico.
UNDP Mexico/Emily Mkrtichian
Mwani wa Sargassum umeharibu baadhi ya fukwe safi zaidi za Mexico.

Mwani watumika kujenga nyumba za bei nafuu nchini Mexico

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP nchini Mexico linafadhili miradi ya maabara za wabunifu wanaopatia majawabu changamoto za kijamii zitokanazo na  matatizo yanayowazunguka. Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa kusafisha fukwe za bahari na uchafu unaokusanywa ukiwemo mwani aina ya Sargusssum, kutumika kutengeneza nyumba. 

Video ya UNDP inaonesha maji yakipiga fukwe ya baharí ya Riviera Maya, maji hayo ya bahari yanakuja na lundo la mwani na mfanyabiashara Omar Sánchez aliona fursa ya kufanya usafi na mwaka 2015 aliingia mkataba na hoteli zilizopo ufukweni kwa ajili ya kusafisha, mkataba ambao uliwanufaisha takriban familia 300 zilizopata ajira ya kusafisha mwani huo wa Sargassum.

Sánchez anasema “Tatizo la mwani wa sargassum ni kubwa. Kwa uzoefu wangu, nimeliona likikua na kukua na kukua kila mwaka.” 

Mfanyabiashara huyo alikuwa akikusanya na kutupa mwani huo lakini baada ya kujiunga na maabara ya UNDP inayolenga kuongeza kasi ya suluhisho zinazobuniwa na wanajamii ndipo alipopata wazo la kutotuoa mwani wa Sargassum bali kuuchakata na kutengeneza matofali ya kujengea nyumba na kuyapa jina la Sargablock. 

Sánchez nasema historia yake ndio ilimsukuma kupata wazo la matofali hayo wakati akiwaza kutafuta mbinu bora za kuisaidia jamii “ jambo la kwanza nililofanya ni kujiweka katika viatu vya wengine. Mama yangu alikufa na hakuwahi kuwa na nyumba yake mwenyewe. Kwa hivyo, nina nini kwa 'Casa Angelita'? Kwanza, nikafikieia wengine na kuanza na wazo la nyumba. Kutokuwa na nyumba ni kejeli ya maisha: Mimi nimekuwa bila makao na sasa nimepata fursa hii ya kusaidia watu wengine.” 

Kampuni yake kwa siku inauwezo wa kutengeneza matofali 1,000 na maono haya ya Sanchez yanamuwezesha kutoa nyenzo ya ujenzi wa gharama nafuu, kujenga nyumba za bei nafuu kwa wakazi wa eneo la Riviera Maya na kutimiza kiu ya familia nyingi ya kuishi katika nyumba zao wenyewe kwa staha. 

Kuhusu Maabara za kuongeza ubunifu za UNDP

Maabara za kuongeza ubunifu kwa wanajamii za UNDP zinasaidia wavumbuzi wenye shauku kama Omar kwa kuwaunganisha kwenye mfumo mpana wa uvumbuzi na kukuza suluhisho zao ili kuwatia moyo wengine.

Mtandao huu unajumuisha timu 91 za Maabara zinazoshughulikia nchi 115 na zinawalenga wavumbuzi wa ndani ya nchi ili kuunda maarifa yanayotekelezeka na yanayofikiria Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa karne ya 21.

Maabara hizo pia zinasaidia UNDP kufikiria upya Maendeleo Endelevu kwa karne ya 21 kwa kuongeza kasi ya kujifunza juu ya kile kinachofanya kazi na kisichofaa linapokuja suala la maendeleo endelevu, kujaribu njia mpya za kushughulikia changamoto za kijamii na mazingira na kuunda uwezo mpya kwa watoa maamuzi.

kuchunguza, kujaribu na kukuza mawazo mbalimbali yanayolenga kutafuta suluhu za kuimarishana ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa.