Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha mwani baharini kimenitoa kwenye nyumba ya tope – Amiri wa Kibuyuni, Kwale - Kenya

Amiri Juma Amiri mkulima huyu wa mwani akiwa na mwani aliovuna kutoka shambani kwake baharini kufuatia mradi unaofadhiliwa na taasisi ya utafiti wa majini na viumbe vya  bahari ya Kenya.
UN/ Kenya
Amiri Juma Amiri mkulima huyu wa mwani akiwa na mwani aliovuna kutoka shambani kwake baharini kufuatia mradi unaofadhiliwa na taasisi ya utafiti wa majini na viumbe vya bahari ya Kenya.

Kilimo cha mwani baharini kimenitoa kwenye nyumba ya tope – Amiri wa Kibuyuni, Kwale - Kenya

Ukuaji wa Kiuchumi

Moja ya malengo ya Mkutano wa bahari unaoendelea Lisbon, Ureno, ni kujadili namna ambavyo dunia inaweza kuendelea kunufaika kiuchumi kutokana na uwepo wa bahari. Ajenda hiyo inakuwa muhimu kwa kuwa tayari ni dhahiri baharí imekuwa mkombozi wa kiuchumi kwa watu wengi duniani. Mfano wa wazi ni Amiri Juma Amiri, mkazi wa kijiji cha Kibuyuni katika Kaunti ya Kwale huko Pwani ya Kenya, mkulima wa zao la mwani ambalo hulimwa baharini.

"Mimi katika hii kazi ya mwani nilikuwa siifanyi.Nilikuwa ninafanya kazi ya uvuvi." Ndivyo anavyoanza kueleza mzee Amiri Juma Amiri, mkazi wa kijiji cha Kibuyuni katika Kaunti ya Kwale huko Pwani ya Kenya. Wakati Bwana Amiri akifanya shughuli za uvuvi, mkewe alikuwa analima mwani baharini, lakini nguvu zikamtupa mkono, hapo ndipo bwana amirí akaingia kusaidia na amejikuta amekuwa kinara wa kilimo cha mwani kama anavyoeleza akisema, "katika wale wakulima ninaweza kusema ni mtu wa kwanza au wa pili kwa ile kulima zaidi." Bwana Amiri akiwa amesimama si mbali kutoka katika ufukwe wa bahari ya hindi na mkononi akiwa ameshika mimea ya mwani iliyofungwa kwa kamba ambazo huisaidia mimea hiyo kuelea kwenye maji, anasema uvuvi ulikuwa haumlipi kwa kiwango anachofaidika nacho katika ukulima wa mwani, "kule baharini katika uvuvi naona mapato yake ni madogo kwa sababu yalikuwa hayakidhi mahitaji yangu katika familia. Ukienda pwani (kuvua samaki) utapata kula, utapata mambo mambo mengine kidogo lakini kuhusu mambo kama ugonjwa, kuhusu mambo ya kusomesha watoto, yalikuwa kidogo yananisumbua." Lakini sasa mambo yamebadilika, "ninapata pesa za mwani ninasomesha (ada za shule)," Anasema Bwana Amiri akiongeza kuwa, sasa ikitokea mambo ya kuugua, anaweza kujihudumia kwa kulipia gaharama na ikitokea mambo yamekuwa magumu zaidi, "nikienda kwa kile kikundi chetu pia ninaweza kusaidiwa nikajisaidia na mimi." Faida anazozipata mzee Amiri kutokana na kilimo hiki cha baharini si hizo pekee, hakika mwani umembadilishia maisha yake "nilikuwa ninaishi nyumba ya matope...nilikuwa ninaishi nyumba ya matope. Lakini nilipoanza kilimo cha mwani hiki, mwaka wa kwanza ule kuuza mwani niliuza tani tatu na nusu. Nilipouza, nilipopata zile pesa niliamua kuuza nyumba ya jiwe na sasa hivi niko na nyumba ya jiwe inaenda chumba cha tatu sasa. Kila nikivuna ninaongeza chumba. Kwa hivyo kwa upande wangu mimi huu mwani, ndio umeniwezesha zaidi kuliko yale mambo ya uvuvi." Mwani ni aina ya mimea inayoota na kukua kwenye maji na inapokomaa na kuvunwa inatumika katika matumizi mbalimbali ya binadamu na wanyama miongoni ikiwa ni kusindika vyakula, dawa na mbolea.