Teknolojia ya kuchuja maji kwenye mabwawa ya samaki yaongeza kiwango cha kamba 

5 Agosti 2022

Nchini Thailand, neema imerejea tena kwa wafugaji wa Kamba wadogo baada ya teknolojia mpya ya kuchuja maji na kulisha viumbe hao kusaidia kuondoa changamoto waliyopata awali ya milipuko ya magonjwa kutokana na uchafu wa maji kwenye mabwawa wanayofugia. 
 

Mradi unatekelezwa kwenye jimbo la Khiri Khan nchini Thailand kwenye mabwawa ya kisasa ya ufugaji samaki, mfugaji akitembea kwenda kuvua samaki kwa kutumia wavu unaonin’ginizwa kwenye njia anamopita, iliyojengwa kwa wavu juu ya mabwawa hayo.

Samaki wamenasa nyavuni na kando ni mashine maalumu yenye magurudumu ya chuma na mfumo wa kutumia hewa inayopuliza maji . Inapita juu ya maji kwa lengo la kuchuja uchafu.

Awali kabla ya teknolojia hii, walitumia siku hadi 10 kusafisha maji ambayo yanachafuliwa si tu na mabaki ya vyakula vya kamba hawa wadogo bali pia uchafu wa haja zao kubwa. Uchujaji usiokuwa fanisi hapo awali ulisababisha milipuko ya magonjwa na mabwawa kufungwa.

Kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo wamepatiwa mashine hii ya kuchuja uchafu, halikadhalika mfumo wa kisasa wa kupatia samaki chakula badala ya kumwaga kwenye bwawa.
Kirana Leesakulpran, mama wa watoto wawili na ambaye amekuwa akifuga samaki aina ya Kamba kwa zaidi ya miaka 30 anasema, “tangu tuanze kutumia teknolojia hii, tunapata kamba wengi zaidi, faida imeongezeka na maisha ya ukulima ni endelevu zaidi.”

Nchini Thailand zaidi ya watu milioni 23, takribani asilimia 34 ya watu wote hawana uhakika wa kupata chakulia na FAO kupitia mradi wa kusaidia uchumi utokanao na shughuli za baharini na majini, inasaidia Thailand kuongeza tija kwenye ufugaji samaki kwa kudhibiti pia uvuvi wa kibiashara.

Theerapong Thammasara ni mvuvi mdogo ambaye anaona mabadiliko ya kiwango cha uvuvi kabla na baada ya mradi na anasema, “nadhani ni kwa sababu ya kanuni zote zinazotekelezwa. Meli kubwa za uvuvi haziruhusiwi kufika maili tatu kutoka pwani. Na kuna sheria kuhusu ukubwa wa nanga. Hizi ni sababu ya kurejea tena kwa vibua.”

Ama hakika katika soko tuliloingia kupitia video ya FAO, vibua ni wakubwa na wengi na bila shaka lengo la kutokomeza uhaba wa chakula na lishe bora litafikiwa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter