Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yapongeza Thailand kwa sheria ya vifungashio vitupu vya Sigara

Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.
Maggie Murray-Lee
Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.

WHO yapongeza Thailand kwa sheria ya vifungashio vitupu vya Sigara

Afya

Serikali ya Thailand imechukua hatua thabiti zaidi ya kudhibiti uvutaji wa sigara kwa kuanzisha vikasha vya sigara visivvyokuwa na maandishi au picha yoyote, hatua ambayo imepongezwa na shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Kwa hatua hiyo inayofuatia bunge kupitia sheria wiki iliyopita kuhusu vikasha vitupu, Thailand inakuwa nchi ya kwanza siyo tu barani Asia bali pia miongoni mwa  nchi za kipato cha chini na kati kuwa na vikasha vya aina hiyo vya sigara.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Asia kusini na mashariki Dkt. Poonam Khetrapa ameiita hatua hiyo ya Thailand kuwa ni ya kijasiri dhidi ya matumizi ya tumbaku, bidhaa ambayo amesema matumizi yake yanasababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.

Sheria hiyo mpya inaongeza nguvu katika sheria ya mwaka huu ya udhibiti wa tumbaku Thailand ambayo inataka sigara iuziwe mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 20, na pia inapiga marufuku uuzaji wa sigara moja moja, inapiga marufuku matangazo ya sigara pamoja na kampuni za sigara kufadhili matukio.

Vifungasho vitupu vya sigara vinazuia matumizi ya nembo, rangi, na picha na kinachotakiwa ni jina la sigara pekee, hatua ambayo inaendana na mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa tumbaku, FCTC.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya Thailand, ifikapo mwaka 2019 vifungashio vya bidhaa zote za tumbaku vitakuwa vitupu kwenye nchi hiyo ambayo  wavutaji tumbaku ni milioni 11.

Hivi sasa duniani kote uvutaji wa tumbaku husababisha vifo vya watu miioni 7 kila mwaka, kiwango ambacho ni sawa na nusu ya watumiaji wote.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.