Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua ombi la dola milioni 124 kukabili changamoto ya afya na njaa pembe ya Afrika

Mtoto huyo wa kike kutoka Ethiopia mwenye umri wa miaka 13 amelazimika kuacha shule na kuozwa kwa mtu asiyemfahamu ili kusaidia familia yake kukabiliana na ukame
UNICEF/UN0651314/Pouget
Mtoto huyo wa kike kutoka Ethiopia mwenye umri wa miaka 13 amelazimika kuacha shule na kuozwa kwa mtu asiyemfahamu ili kusaidia familia yake kukabiliana na ukame

WHO yazindua ombi la dola milioni 124 kukabili changamoto ya afya na njaa pembe ya Afrika

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO leo limezindua ombi la takribani dola milioni 124 kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya haraka ya afya kwenye pembe ya Afrika hadi mwezi Desemba mwaka huu.

Shirika hilo linasema janga la chakula na afya kwenye eneo hilo ni ukweli wa kutisha na hakuna fedha za kutosha kulinda raia.

Dkt Ibrahima Fall, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO akihusika na dharura amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa njaa humdhoofisha mtu lakini magonjwa yanamuua hivyo “ndio maana WHO imeimarisha hatua zake katika nchi saba zilizoathirika zaidi ambazo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda na lengo ni kuhakikisha watoto wenye utapiamlo mkali wanaendelea kupata huduma wanayohitaji.”

Mkanganyiko wa ukosefu wa chakula, njaa na janga la afya

Amefafanua kuwa mchanganyiko kwa ongezeko la ukosefu wa uhakika wa chakula, njaa na utapiamlo vinasababisha dharura na kukwamisha kutambuliwa kwa dharura za kiafya kwa kuwa “dharura ya kiafya inaongezeka lakini fursa ya kupata matibabu inazidi kuwa ndogo.”

Ameongeza kuwa fedha zitakazopatikana pia zitasaidia kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa iwapo magonjwa ya mlipuko kama vile surua, kipindupindu na homa ya uti wa mgondo inatokea.

Tuchukue hatua sasa badala ya kusubiri watu wafe ndio tuamke

Dkt. Fall ambaye alikuwa akizungumza kwa njia ya video kutoka Dakar, Senegal, amesema WHO inapaswa kuchukua hatua sasa ili kuepusha watu kufariki dunia.

Akifafanua Zaidi kuhusu hatua hii ya sasa, Sophie Maes ambaye ni Meneja wa WHO wa uratibu wa matukio, ukame na ukosefu wa uhakika wa chakula, amezungumza kwa njia ya video kutoka Nairobi, Kenya akisema “kitengo kidogo kimeanzishwa Nairobi ili kuhakikisha hatua katika nchi hizo saba (7) zinasaidiwa na zinafanyika kwa mtiririko.”