Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 13 wanakabiliwa na njaa kali Pembe ya Afrika 

Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka
FAO/IFAD/WFP/Michael Tewelde
Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka

Watu milioni 13 wanakabiliwa na njaa kali Pembe ya Afrika 

Tabianchi na mazingira

Pembe ya Afrika inakabiliwa na hali ya ukame mkali zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1981, ambao unawaweka takriban watu milioni 13 kote Ethiopia, Kenya na Somalia katika hali ya kukabiliwa na njaa kali katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limeonya leo kupitia taarifa yake iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya. 

WFP inaeleza kuwa misimu mitatu ya mvua ambayo haikuwa mizuri mfululizo imeharibu mazao na kusababisha vifo vya mifugo mingi isivyo kawaida. Uhaba wa maji na malisho unalazimisha familia kutoka katika nyumba zao na kusababisha kuongezeka kwa migogoro kati ya jamii. Utabiri zaidi wa mvua za chini ya wastani unatishia kuwa mbaya na kuongeza hali mbaya katika miezi ijayo. 

Mkurugenzi wa Kanda katika Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki ya WFP, Michael Dunford anasema, "mavuno yanaharibiwa, mifugo inakufa, na njaa inaongezeka huku ukame wa mara kwa mara ukiathiri Pembe ya Afrika. Hali inahitaji hatua za haraka za kibinadamu na usaidizi thabiti ili kujenga uthabiti wa jamii kwa siku zijazo.” 

Ukame umeathiri wafugaji na wakulima kote kusini na kusini-mashariki mwa Ethiopia, kusini-mashariki na kaskazini mwa Kenya na kusini-kati mwa Somalia. “Madhara hayo yanaongeza machungu katika ongezeko la bei za vyakula, mfumuko wa bei, na mahitaji ya chini ya nguvu kazi katika kilimo, hali inayozidisha ugumu zaidi kwa uwezo wa familia kununua chakula. Viwango vya utapiamlo pia vinasalia kuwa juu katika eneo lote na vinaweza kuwa vibaya zaidi ikiwa hakuna hatua za haraka zitachukuliwa.” WFP inaonya. 

Katika nchi tatu zilizoathiriwa na ukame, WFP inatoa msaada wa kuokoa maisha wa chakula na lishe kwa jamii zilizoathirika. Zaidi ya hayo, misaada ya fedha taslimu kutoka WFP na mipango ya bima inasaidia familia kununua chakula ili kuweka mifugo yao hai au kuwafidia hasara zao. 

“Mahitaji yakiwa yanavyoongezeka katika Pembe ya Afrika, usaidizi wa haraka ni muhimu ili kuepuka janga kubwa la kibinadamu, kama lile ambalo ulimwengu ulishuhudia mwaka 2011 wakati watu 250,000 walikufa kwa njaa nchini Somalia.” Inaeleza WFP ambayo wiki hii imezindua Mpango wake wa Kikanda wa Kukabiliana na Ukame kwa Pembe ya Afrika, ikitoa wito wa dola za Marekani milioni 327 ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya watu milioni 4.5 katika kipindi cha miezi sita ijayo na kusaidia jamii kustahimili majanga makubwa ya tabianchi.