Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia DRC: Guterres azungumza na Rais Tshisekedi na kuomba radhi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Ghasia DRC: Guterres azungumza na Rais Tshisekedi na kuomba radhi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhusu tukio la walinda amani wa Umoja huo kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO kuua raia na kujeruhi wengine mpakani mwa nchi hiyo na Uganda.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane  Dujarric ameeleza hayo leo jijini New York, Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu ametoa salamu za rambirambi na pia ameomba radhi kwa tukio la jana ambalo lilihusisha walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kasindi mpakani mwa DRC na Uganda,” amesema Bwana Dujarric.

Amesema Katibu Mkuu amemjulisha Rais Tshisekedi kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kwenye suala la amani na kuratibiana na kushirikiana na jeshi la DRC, FARDC kutatua hali ya sasa na kuleta utulivu mashariki mwa taifa hilo la maziwa makuu.

“Mazungumzo ya dhati na ya kweli yanahitajika,” amesema Katibu Mkuu akiongeza “na kwa hilo kufanyika tunataka kuondoka DRC kwa kikundi cha M23 bila masharti yoyote na vikundi vyote vilivyojihami vikomeshe aina zote za ghasia.”