Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres azungumza na Tshisekedi kuhusu kuibuka tena kwa M23 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini.

Guterres azungumza na Tshisekedi kuhusu kuibuka tena kwa M23 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Félix Tshisekedi Tshilombo ambapo wamejadili masuala kadhaa ikiwemo hali ya amani mashariki mwa Taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika. 

Taarifa ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema suala la kuibuka tena kwa waasi wa kikundi cha M23 jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC limejadiliwa sambamba na athari zake kwa raia na ufikishaji wa misaada wa kibinadamu. 

Katibu Mkuu amekaribisha juhudi za Rais Tshisekedi za kuimarisha ushirikiano na nchi kwenye ukanda huo katika kuimarisha amani na maendeleo. 

Halikadhalika amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za amani na ulinzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ukanda mzima. 

M23 wanashambulia raia 

Hivi karibuni kumekuwepo na matukio kadhaa ya mashambulizi  yanayodaiwa kufanywa na kikundi cha waasi cha M23 mashariki mwa DRC. 

Tarehe 29 mwezi uliopita wa Machi, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, Bintou Keita alijulisha Baraza la Usalama juu ya ongezeko la mashambulizi kutoka vikundi vya waasi ikiwemo M23. 

Alisema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kumekuweko na ongezeko la shughuli za kikund icha M23 huko Kivu Kaskazini na kwamba katika tukio moja waliendesha shambulizi hatari lililolenga raia karibu na eneo la Rutshuru. 

Kutokana na ongezeko hilo MONUSCO imekuwa ikifanya doria za ufuatialiaji ambapo katika doria moja iliyokuwa inafanyika kwa helikopta, kwenye eneo linalosadikiwa kuweko waasi wa M23, helikopta ilianguka na walinda amani walipoteza maisha.