Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Hali ya kawaida imerejea lakini bado tete

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini.

DRC: Hali ya kawaida imerejea lakini bado tete

Amani na Usalama

Kaimu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Kassim Diagne amezungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka mji mkuu Kinshasa na kusema hali ya kawaida angalau imerejea lakini bado ni tete baada ya mamlaka kutoa wito kwa waandamanaji kusitisha vitendo hivyo sambamba na jeshi la serikali, FARDC kuimarisha usalama.

Hatupuuzi njia zozote za kufikia amani

“Katu hatupuuzii njia zozote za kufikia suluhu,” amesema Bwana Diagne huku akisisitiza kuwa MONUSCO inapanga kuchunguza mauaji ya walinda amani wake watatu, lakini pia kufanya uchunguzi wa pamoja na serikali ya DRC kuhusu chanzo cha shambulio hilo lililosababisha vifo vya raia wapatao 15 wakati wa maandamano hayo.”

Ameongeza ya kwamba, "hatuna ushahidi kwamba wanajeshi wa MONUSCO waliwafyatulia risasi raia, lakini, tena, tunataka kufanya uchunguzi na serikali ili kubaini milio hii ya risasi ilitoka wapi, na tuna uwezo wa kufanya hivyo.”

Kuna makundi mawili ya waandamanaji

Bwana Diagne amedokeza kuwa maandamano jimboni Kivu Kaskazini yamechochewa na kampeni potofu dhidi ya MONUSCO.

“Kuna makundi mawili ya waandamanaji, wale wanaotaka mjadala wa amani na kundi lingine ni waporaji,” amefafanua.

Kwa mujibu wa MONUSCO na serikali ya DRC kundi la pili la waporaji lilijumuisha pia vikundi vilivyojihami. Kundi hilo lilifyatulia risasi walinda amani na kwa hivyo lazima wafikishwe mbele ya sheria.

Mchakato wa MONUSCO kuondoka DRC unaendelea

Bwana Diagne amesema waandamanaji wa amani wanataka MONUSCO iondoke DRC ambapo amefafanua kuwa, « tunaendelea na mchakato tena kwa amani na mchakato huo unaendelea.”

Amebainisha kuwa mkakati wa kuondoka na jukwaa la kufanikisha hilo tayari umeshafanyika kwa ushirikiano wa serikali.

 Sio tu kwamba MONUSCO ilijiondoa katika jimbo la Tanganyika tarehe 30 Juni, lakini ujumbe huo umeongezeka kutoka uwepo wa maeneo  zaidi ya 12 mwaka 2002 hadi kubakia katika maeneo mitatu tu leo.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa operesheni za ulinzi wa amani Jean-Pierra Lacroix anatarajiwa kuwasili DRC Ijumaa wiki hii kwa ziara ya siku mbili ambako atatembelea Kinshasa na Kivu Kaskazini.